Apr 23, 2022 19:56 UTC
  • Jumamosi tarehe 23 Aprili 2022

Leo ni Jumamosi tarehe 21 Ramadhani 1443 Hijria inayosadifiana na tarehe 23 Aprili mwaka 2022.

Siku kama ya leo miaka 1403 iliyopita Ali bin Abi Talib AS mrithi wa Mtume Muhammad (saw) na mmoja wa Ahlul Bait wa Mtume, aliuawa shahidi. Siku mbili kabla ya kifo chake, Imam Ali bin Abi Twalib alipigwa upanga kichwani na mmoja wa Khawarij wakati alipokuwa katika sijda akimwabudu Mwenyezi Mungu msikitini katika Swala ya Alfajiri. Siku kama ya leo Imam Ali (as) aliaga dunia kutokana na majeraha makubwa aliyopata na hivyo kufikia matarajio yake makubwa ambayo alikuwa akiyatamani daima, yaani kuuliwa shahidi katika njia ya Mwenyezi Mungu SW. Kuuawa shahidi Imam Ali bin Abi Twalib (as) kulikuwa msiba mkubwa na usioweza kufidika kwa Uislamu na Waislamu.

Imam Ali (as) aliwausia wanawe na Waislamu ambao watafikiwa na wasia wake akisema: "Nawausia kumcha Mungu na kuwa na taratibu nzuri katika mambo yenu. Wajalini yatima na muwafanyie mema majirani zenu, kwani nilimsikia Mtume wa Allah (saw) akiusia kuwafanyia mema jirani hadi nikadhani atawarithisha. Shikamaneni na Qur'ani na msiache watu wengine wawatangulie mbele katika kutekeleza mafundisho yake. Itukuzeni Swala kwani ndiyo nguzo ya dini yenu.." Sala na salamu za Allah jiwe juu ya Imam Ali bin Abi Twalib na Aali zake watoharifu.

Siku kama ya leo ya tarehe 3 mwezi ordibehesht katika kalenda ya mwaka wa Kiirani ni siku ya kumuenzi Sheikh Bahauddin Muhammad Amili maarufu kwa jina la Sheikh Bahai, wmanazoni mkubwa wa taaluma mbalimbali za Kiislamu. Sheikh Bahai ambaye alikuwa ametabahari katika elimu nyingi kama fiqhi, nujumu, hadithi, tafsiri ya Qur'ani na hesabati alifariki dunia katika mji wa Isfahan nchini Iran. Alizaliwa mwaka 953 Hijria katika mji wa Baalabak huko Lebanon katika familia ya Kiirani. Baba yake alikuwa miongoni mwa mashekhe wakubwa wa zama hizo. Sheikh Bahai ameandika vitabu zaidi ya mia moja ikiwa ni pamoja na Tashrihul Aflak, Kashkul na Hablul Matin.

Katika siku kama ya leo miaka 406 iliyopita, aliaga dunia William Shakespeare, mshairi na mwandishi mashuhuri wa michezo ya kuigiza wa Uingereza. Shakespeare alianza kazi zake za usanii sambamba na kushiriki katika michezo ya kuigiza. Alipata umashuhuri mkubwa katika taaluma hiyo. Kazi zake za kisanii zilikuwa mchanganyiko wa sanaa iliyoakisi majonzi na vichekesho. Miongoni mwa kazi maarufu zaidi za Shakespeare ni Romeo and Juliet, Hamlet, King Lear na The Merchant of Venice. 

William Shakespeare

Tarehe 21 Ramadhani miaka 339 iliyopita alifariki dunia faqihi na mwanazuoni mashuhuri wa Kiislamu Sheikh Abu Jaafar Muhammad bin Hassan maarufu kwa jina la Sheikh Hurr al Aamili huko Jabal Amil nchini Lebanon. Alitokea kuwa miongoni mwa maulama na watafiti wakubwa wa Kiislamu. Sheikh Hurr al Amili ameandika vitabu vingi vya fiqhi na Hadithi na miongoni mwavyo ni kile cha Wasaailu Shia ambacho kina nafasi maalumu katika duru za elimu ya fiqhi.

Miaka 164 iliyopita katika siku kama ya leo alizaliwa mwanafizikia Max Plank wa Ujerumani ambaye pia alikuwa mtaalamu wa hisabati aliyebuni Nadharia ya Kwanta katika elimu ya fizikia. Mwaka 1918 Max Plank alitunukiwa tuzo ya fizikia ya Nobel kwa kugundua nadharia ya kwanta. Plank ambaye alikuwa mpinzani mkubwa wa dikteta wa zamani wa Ujerumani Adolph Hitler, alifanya utafiti mkubwa katika nyanja za mwendojoto (sayansi ya uhusiano wa joto na kazi za mitambo), fizikia nadharia, joto, mnururisho na nuru na kuandika vitabu kadhaa katika medani hiyo.

Max Plank

Katika siku kama ya leo miaka 30 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 23 Aprili 1992, alifariki dunia Satyajit Ray mwandishi na mtengeneza filamu mashuhuri wa India. Satyajit Ray alizaliwa mwaka 1921, na filamu zake za kijamii ziligusa zaidi hisia za jamii ya wananchi wa nchi hiyo, na kupelekea kupendwa zaidi na wananchi wa India.

Satyajit Ray

Na tarehe 23 Aprili miaka 27 iliyopita Shirika la Sayansi, Elimu na Utamaduni la Umoja wa Mataifa (UNESCO) liliitangaza siku hii ya kuwa Siku ya Kimataifa ya Kitabu na Haki za Mwandishi. Lengo la kutangazwa siku hiyo ni kuonesha umuhimu wa kitabu na haki za waandishi wa vitabu, kuhamasisha watu kusoma vitabu, kuwapongeza watu wanaoandika vitabu kwa ajili ya kukuza na kustawisha utamaduni wa jamii ya mwanadamu na vilevile kuunga mkono na kusaidia ustawi wa sekta ya kusambaza vitabu. Utamaduni wa kusoma vitabu umeshamiri zaidi katika dunia ya sasa hususan miongoni mwa tabaka la vijana kutokana na kusambaa zaidi vitabu vya elektroniki kupitia mitandao ya intaneti.