Apr 24, 2022 02:22 UTC
  • Jumapili tarehe 24 Aprili 2022

Leo ni Jumapili tarehe 22 Ramadhani 1443 Hijria sawa na Aprili 24 mwaka 2022.

Siku kama ya leo miaka 1470 iliyopita kwa mujibu wa mahesabu ya wanahistoria wengi, iliasisiwa kwa mara ya kwanza taasisi ya kuandika na kutarjumu vitabu duniani hapa nchini Iran. Uamuzi huo ulichukuliwa na Khosrow Anushirvan, mfalme wa Sasani nchini hapa. Taasisi hiyo ilijengwa sambamba na maktaba na vilikamilishwa kujengwa mwaka huo huo. Vitabu tofauti vilikusanywa kutoka maeneo mbalimbali ya dunia kwa ajili ya kutarjumiwa na mfalme huyo alimtuma daktari wake kwenda nchini India kwa ajili ya kukusanya vitabu kwa ajili ya shughuli hiyo.

Siku kama ya leo miaka 1170 iliyopita, alifariki dunia Ibn Majah, mpokezi wa Hadithi na mfasiri mashuhuri wa Qur’ani wa Kiislamu. Ibn Majah alizaliwa mwaka 209 Hijria katika mji wa Qazvin nchini Iran. Alielekea katika nchi mbalimbali za Kiislamu ili kujifunza elimu ya Hadithi. Aliandika kitabu chake mashuhuri kwa jina la "Sunan Ibn Majah" baada ya kuhitimu masomo katika elimu ya Hadithi, kitabu ambacho ni moja kati ya vitabu sita vya Hadithi vyenye itibari vya Waislamu wa madhehebu ya Suni. Vitabu vingine vya Ibn Majah ni Tafsirul Qur'an na Tarikh Qazvin.

Katika siku kama ya leo miaka 751 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 24 April mwaka 1271, mtalii Marco Polo wa Venice alianza safari ya kihistoria ya kutembelea bara Asia. Kabla yake baba na ami yake walitembelea China kupitia njia ya Asia Ndogo na Iran. Baada ya kurejea ndugu wa Polo kutoka Ulaya, Marco Polo akifuatana na baba yake kwa mara nyingine walielekea China na kutembelea ardhi ya nchi hiyo na visiwa vya kusini mshariki mwa Asia. Baada ya kurejea nchini kwake, Marco Polo aliandika kumbukumbu ya safari iliyoitwa "Maajabu" kuhusiana na hali ya kijiografia ya ardhi za China, Turkemanistan, Mongolia na sehemu za kusini mashariki mwa Asia. Safari ya Marco Polo barani Asia ilichukua karibu miaka 20.

Marco Polo

Tarehe 24 Aprili mwaka 1916 kulianza harakati ya tatu ya raia wa Ireland kwa ajili ya kujipatia uhuru wao kutoka kwa serikali ya Uingereza. Harakati hiyo ilienda sambamba na kujiri kwa vita vikali vya kidini baina ya Waprotestanti na Wakatoliki. Vita hivyo vilimalizika kwa kufikiwa makubaliano baina ya David Lloyd George, Waziri Mkuu wa wakati huo wa Uingereza na kiongozi wa harakati ya raia wa Ireland waliokuwa wanataka kujitenga hapo mwaka 1922 Miladia.

Bwndera ya Ireland

Siku kama ya leo miaka 95 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 24 April mwaka 1927 chanjo ya B.C.G iligunduliwa. Chanjo hiyo iligunduliwa na madaktari wa kifaransa Albert Calmette na Guerin, baada ya kufanya uchunguzi wa miaka mingi. Chanjo ya B.C.G hutumika kukinga maambukizi ya ugonjwa wa kifua kikuu au TB. Kugunduliwa chanjo hiyo kumepunguza vifo vya watu wanaopatwa na ugonjwa wa TB duniani kote.

Na katika siku kama ya leo miaka 82 iliyopita, kwa mara ya kwanza kulianzishwa idara ya redio nchini Iran na kurushwa matangazo ya moja kwa moja. Awali kituo cha redio kilikuwa chini ya usimamizi wa Wizara ya Posta, Simu na Telegrafu. Miaka mitano baada ya kuanzishwa kituo cha redio mjini Tehran, hatua kwa hatua huduma hiyo ilipanuliwa katika miji mbalimbali hapa nchini. Lakini baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu 1979, zilianzishwa redio na televisheni kadhaa, zikiwemo zile za matangazo ya ng'ambo, zinazotangaza kwa lugha mbalimbali za kigeni ikiwemo Idhaa ya Kiswahili ya Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran iliyoanzishwa mwaka 1994.

 

Tags