Jumanne tarehe 26 Aprili 2022
Leo ni Jumanne tarehe 24 mwezi mtukufu wa Ramadhani 1443 Hijria sawa na tarehe 26 Aprili mwaka 2022.
Siku kama ya leo miaka 733 iliyopita, alifariki dunia Qutbuddin Shirazi, tabibu, mwanahesabati, mwanafikizia na mwanafalsafa wa Kiirani katika mji wa Tabrizi huko kaskazini magharibi mwa Iran. Qutbuddin Shirazi alikuwa miongoni mwa wanafunzi wa mwanazuoni mashuhuri wa Kiislamu Khaja Nasiruddin Tusi. Alibobea pia katika elimu za mantiki na irfani. Alifanya hima kubwa kutafuta elimu ya tiba na alihudumu kwa miaka mingi kama tabibu katika hospitali ya Shiraz, kusini mwa Iran. Qutbuddin Shirazi alikuwa mtu wa kwanza kufanya uchunguzi kuhusu upinde wa mvua na kupata tafsiri ya kisayansi kuhusu suala hilo. Mwanazuoni huyo mkubwa wa Kiislamu ameandika vitabu vingi katika taaluma mbalimbali.
Tarehe 26 Aprili miaka 417 iliyopita lilichapishwa gazeti la kwanza kabisa duniani nchini Ufaransa. Mhariri mkuu wa gazeti hilo lililopewa jina la Relation alikuwa Johann Carolus. gazeti hilo liliendelea kuchapishwa kwa kipindi cha miaka 70. Hii leo maelfu ya magazeti huchapishwa kila siku katika pembe mbalimbali za dunia na Wajapani wanahesabiwa kuwa wasomaji wakubwa zaidi wa magazeti kuliko watu wa maeneo mengine ya dunia.
Siku kama ya leo miaka 97 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 6 Ordibehesht 1315 Hijria Shamsia, kituo cha kwanza cha matangazo ya redio na telegrafu kilianza kazi nchini Iran. Mwanzoni mwa kuanzishwa kwake, kituo hicho kilikuwa chini ya usimamizi wa Wizara ya Vita. Miaka iliyofuata vituo vya kurusha matangazo ya redio na telegrafu vilianzishwa katika miji mbalimbali ya Iran na idara hiyo ikakabidhiwa kwa Wizara ya Posta na Telegrafu.
Katika siku kama ya leo miaka 89 iliyopita, shirika la kuogofya la Gestapo la Ujerumani liliasisiwa. Shirika hilo liliasisiwa na Hermann Wilhelm Goering aliyekuwa mmoja wa maafisa wa juu wa Adolph Hitler kiongozi wa Wanazi wa Ujerumani. Shirika hilo lilikuwa ni polisi wa siri wa Kijerumani katika kipindi cha utawala wa Wanazi. Jukumu la German for Secret State Police, kama lilivyojulikaa pia, lilikuwa ni kuwafatilia, kuwatia mbaroni na kuwanyongwa watu waliokuwa wakimpinga Hitler na siasa zake za Kinazi. Kiongozi mashuhuri kabisa wa Gestapo alijulikana kwa jina la Heinrich Himmler na alianza kuwaongoza polisi hao wa siri wa Kijerumani mwaka 1934.
Siku kama ya leo miaka 58 iliyopita Jamhuri ya Muungano wa Tanzania iliundwa baada ya nchi mbili za Tanganyika na Zanzibar kuungana. Kabla ya kuungana huko Tanganyika na Zanzibar zilikuwa zikikoloniwa na nchi mbalimbali ambapo nchi mkoloni wa mwisho ilikuwa Uingereza. Tanganyika ilipata uhuru mwaka 1961 na Zanzibar mwaka 1963 baada ya mapambano ya wananchi ya kupigania uhuru dhidi ya mkoloni Muingereza. Julius Kambarage Nyerere alitoa wito wa kuungana Tanganyika na Zanzibar na ilipofika tarehe 26 mwezi Aprili mwaka 1964 nchi mbili hizo ziliungana na kuunda Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.Tanzania iko mashariki mwa Afrika na katika pwani ya Bahari ya Hindi huku ikipakana na Kenya, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Uganda, Rwanda, Burundi, Zambia, Malawi na Msumbiji.
Siku kama ya leo miaka 37 iliyopita Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilitoa azimio nambari 620 likilaani hatua ya Iraq ya kutumia silaha za kemikali. Baada ya utawala wa zamani wa Iraq kushambulia kwa mabomu ya kemikali makazi ya raia nchini Iran na kufuatia mashtaka yaliyowasilishwa na Iran, ujumbe wa Umoja wa Mataifa ulitumwa katika nchi za Iran na Iraq na ukatoa ripoti mbili ambazo zilieleza kuwa, utawala huo ulitumia mara kadhaa silaha za kemikali dhidi ya majeshi na raia wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Hii ilikuwa mara ya kwanza kwa Umoja wa Mataifa kukiri waziwazi kwamba, jeshi la Iraq lilitumia silaha za kemikali dhidi ya Iran. Katika kipindi chote cha vita vya miaka 8 vilivyoanzishwa na Iraq dhidi ya Iran, utawala wa Saddam Hussein uliua shahidi maelfu ya wanajeshi na raia wa Iran kutokana na kutumia silaha za gesi yenye kemikali. Kwa sababu hiyo Iran inatambuliwa kuwa mhanga mkubwa zaidi wa silaha za kemikali duniani baada ya Vita vya Pili vya Dunia.
Siku kama ya leo 36 iliyopita, kituo cha nguvu za nyuklia cha Chernobyl huko Ukraine ambacho kilikuwa kikidhamini sehemu kubwa ya nishati ya umeme ya nchi hiyo kiliripuka na kusambaza mada hatari za miale ya radioactive. Awali Russia ilikadhibisha habari ya kutokea mlipuko katika kituo hicho. Hata hivyo baadaye ililazimika kukiri kutokea mlipuko katika kituo hicho cha nguvu za nyuklia cha Chernobyl baada ya wingu kubwa la nyuklia lililosababishwa na mada za radioactive kuoneka waziwazi katika kituo hicho. Kasoro za kiufundi zilitajwa kuwa chanzo cha mlipuko huo. Katika tukio hilo, makumi ya maelfu ya watu waliathirika kwa namna tofauti ikiwemo kuongezeka maradhi mbalimbali. Mwaka 2000 Ukraine ilikifunga kabisa kituo cha nyuklia cha Chernobyl.
Siku kama ya leo miaka 26 iliyopita mwafaka na tarehe 26 Aprili mwaka 1996, mashambulizi ya kijeshi ya siku 16 ya utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Lebanon kwa jina la "Vishada vya Hasira" yalimalizika. Katika operesheni hiyo jeshi la utawala wa Israel lilifanya mashambulio ya nchi kavu, anga na baharini huko kusini na hata katika ya mji mkuu wa Lebanon, Beirut. Mbali na kuharibu maeneo mengi ya raia na miundo mbinu na taasisi za kiuchumi, utawala haramu wa Israel uliwaua shahidi raia 180 wa Lebanon na kujeruhi mamia ya wengine.