Apr 28, 2022 06:13 UTC
  • Mchango wa Maulamaa wa Kishia Katika Uislamu (44)

Ni matumaini yangu kuwa, hamjambo wapenzi wasikilizaji na karibuni katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Mchango wa Maulamaa wa Kishia Katika Uislamu

 

Kipindi kilichopita kilianza kumzungumzia Sayyid Muhammad Mahdi Tabataba'i Najafi ambaye ni mashuhuri kwa jina la Allama Bahr al-Ulum, fakihi, mpokezi wa hadithi na arif mkubwa wa Kishia. Alizaliwa katika siku ya Eidul Fitr mwaka 1155 Hijria huko Karbala huko Iraq. Tulieleza kwamba, siku moja wakati wa somo kuendelea, Mirza Khorasani ambaye alikuwa ameshangazwa mno na akili na maarifa ya hali ya juu ya mwanafunzi wake alimhutubu kwa kumwambia: Kwa hakika wewe ni bahari ya elimu.". Ni kuanzia kipindi hicho, ndipo msomi huyo akaondokea kuwa mashuhuri kwa jina la Sayyid Bahrul Ulum, lakabu ambayo alibakia nayo mpaka mwishoni mwa umri wake. Sehemu ya 44 ya mfululizo huu juma hili itaendelea na maudhui hii.

Sayyid Bahrul Ulum

 

 Allama Bahrul Ulum siyo tu kwamba, alikuwa ameibuka na kuondokea kuwa msomi na mwanazuoni aliyebobea kielimu na usimamiaji mambo kwa njia sahihi, bali kwa hakika alikuwa mfano wa kuigwa wa mtu aliyekamilika kwa mujibu wa maadili ya Kiislamu na mtindo wa maisha ya kidini. Alimu huyu mtajika kutokana na kuwa na daraja ya juu kimaanawi, taqwa, uchajimungu na kumtambua Mwenyezi Mungu aliondokea kuheshimiwa mno na Maulamaa wa Kishia. Heshima hiyo ilikuwa kubwa kiasi kwamba, kutokana na usafi wa matendo na amali alitambuliwa kama mtu aliyekaribia daraja ya Umaasumu (ya kutotenda dhambi). Tabia njema ya Sayyid Bahrul Ulum pamoja na kuishi vyema na watu kwa hakika lilikuwa jambo la kusifiwa na kuthaminiwa mno.

Tawadhui na unyenyekevu wake ulikuwa kwa namna maalumu kwa watu maalumu na wa kawaida na wakati huo huo alikuwa na haiba ya aina yake. Upole na huruma yake kwa wahitaji na watu wasiojiweza ulikuwa mkubwa mno. Allama Bahrul Ulum alikuwa mkimya sana na daima alikuwa katika hali ya kutafakari na kufikiri. Alipokuwa akisema kitu, basi hilo lilikuwa likiambataNA na kumtaja na kudhukuru Mwenyezi Mungu. Wakati wa mchana alikuwa akijishughulisha na kufundisha na kushughulikia mahitaji ya wasiojiweza ya Waislamu na wakati wa usiku alikuwa akijisomea na kufanya ibada.

Allama Bahrul Ulum alikuwa akila kidogo na kulala kwa masaa machache mno. Wakati mwingi ilikuwa ikitokea kwamba, baada ya nusu ya usiku alikuwa akitembea kwa miguu kutoka Najaf mpaka mjini Kufa ili wakati wa munajati na dua za usiku awe katika Msikiti wa Kufa. Baada ya Swala ya Alfajiri alikuwa akirejea Najaf na kabla ya kufanya chochote alikuwa akienda kufanya ziara katika Haram ya Imam Ali bin Abi Twalib (as).

Mbali na kubobea na kutabahari katika elimu za Kiislamu, Allama Bahrul Ulum alikuwa na ufahamu na umahiri wa aina yake kwa vyanzo na misingi ya kiitikadi ya dini nyingine. Ni kutokana na sababu hiyo ndio maana alikuwa na nguvu isiyo na mithili katika midahalo na wapinzani na katika kuthibitisha kwamba, Uislamu ni dini ya haki.

 

Kama ambavyo Allama Bahr al-Ulum alikuwa akizingatia na kulipa umuhimu mno suala la malezi na kuitakasa nafsi yake, alikuwa akilipa kipaumbele maalumu pia suala la kuwalea kinafsi wanafunzi wake. Daima alikuwa akiwashajiisha wanafunzi kuswali Swala ya usiku. Inasimuliwa kuwa, siku moja Allama Bahr al-Ulum alisimamisha na kusitisha kufundisha kutokana na kuwa wanafunzi walikuwa hawalipi umuhimu suala la Swala ya Usiku na akawahutubu kwa kuwaambia: Kwa nini mimi sisikii minong’ono na vilio vyenu wakati wa Swala za usiku?  Wanafunzi wale waliathirika mno baada ya kusikia maneno yale na  kuanza kutekelea Suna ya kuswali Swala ya Usiku. Baada ya ada hii kudhihirika na kuibuka na kuleta mageuzi baina ya wanafunzi, mwalimu huyu alianza tena kufundisha na kuendelea na darsa zake kama kawaida.

Swala ya Usiku ni miongoni mwa Swala zenye fadhila kubwa na kuna hadithi nyingi ambazo zimenukuliwa katika vitabu vya kuaminika vya hadithi zinazohimiza na kutilia mkazo juu ya kuitekeleza Sunna hii. Swala ya usiku ni Swala muhimu zaidi ya mustahabu ambayo ina rakaa 11 na wakati wake ni baada ya nusu ya usiku mpaka  adhana ya Alfajiri. Kwa mujibu wa Aya ya Qur’ani isemayo:  

Na amka usiku kwa ibada; ni ziada ya sunna khasa kwako wewe.

Swala hii ya mustahabu ilikuwa wajibu kwa Bwana Mtume (saw). Katika hadithi inasisitizwa kuwa, Swala hii inaongeza sharafu na heshima ya muumini, ni kafara ya madhambi ya siku, inaondoa woga wa kaburini na inadhamini riziki ya mja. Na ndio maana imesisitizwa na kukokotezwa kwamba, kama mja hakupata fursa ya kuiswali kwa wakati wake, basi alipe qadhaa.

Kuna hekaya na simulizi nyingi zilizonukuliwa katika vitabu vya historia ambazo zinaeleza na kubainisha jinsi Sayyid Bahr al-Ulum alivyokuwa akisaidia watu wasiojiweza na wahitaji. Kama alivyokuwa babu yake yaani Amir al-Muuminina (as), Allama Bahr al-Ulum alikuwa pia akibeba mzigo uliokuwa umejaa bidhaaa za chakula katika giza la usiku huko Najaf ambapo alikuwa akipita katika mitaa na vichochoro vya mji huo na kugawa vyakula na fedha kwa masikini na wahitaji.

 

Inasimuliwa kuwa, usiku mmoja alimuita mmoja wa wanafunzi wake mahiri na kumlaumu sana akimwambia kwa nini hana taarifa za jirani yake asiye na uwezo. Allama Bahr al-Ulum alimwambia mwanafunzi wake, jirani yako masikini na mwenye kuhitaji usiku wa leo watoto wake wamelala pasi na kupata chakula cha usiku na wewe hujawashughuilikia! Mwanafunzi yule alimtaka radhi mwalimu wake, na huku akiwa amekumbwa na soni na haya nyingi alimwambia mwalimu wake, mimi sikuwa na habari kuhusu hali yake. Mwalimu wake akamwambia: Bila shaka hukuwa na taarifa zake, kwani ungekuwa unafahamu hali yake na ukala chakula cha usiku na kupuuza hilo, ungekuwa kafiri, lakini kile ambacho kinanitia wasiwasi mimi ni kwamba, kwa nini hukuwa na taarifa za ndugu yako Mwislamu? Unapaswa kufahamu na kuelewa hali ya ndugu yako Mwislamu. Kisha Allama Bahr al-Ulum akampatia mwanafunzi wake sinia lililokuwa limejaa chakula na kiwango fulani cha fedha na kumtaka alipeleke katika nyumba ya ndugu yule Muumini na akale pamoja naye chakula cha usiku na kisha amlipie madeni jirani yake yule.

Kuhusiana na makarama ya Sayyid Allama Bahr al-Ulum kumenukuliwa mengi lakini muhimu zaidi ni kwamba, alikuwa akikutana na Imam wa Zama Imam Mahdi (atfs) na hayo yanapatikana katika vitabu vyenye itibari.

Kaburi la Sayyid Bahrul Ulum

 

Mwishoni mwa umri wake, mwanazuoni huyo alipatwa na maradhi na hivyo kipindi fulani hakuwa na uwezo tena wa kufundisha bali alibakia nyumbani akijishughulisha na kujisomea na kuandika vitabu. Hatimaye tarehe 24 Mfunguo Tatu Dhul-Hija au Rajab mwaka 1212 mwanazuoni huyo aliaga dunia na kurejea kwa Mola wake akiwa na umri wa miaka 57. Mwanazuoni huyo amezikwa kando ya kaburi la Sheikh Tusi katika mji wa Najaf. Muda wa kipindi chetu kwa umefikia tamati, jiungeni nami katika sehemu nyingine ya mfululizo huu.

Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.