Jumapili tarehe Mosi Mei 2022
Leo ni Jumapili tarehe 29 Ramadhani 1443 Hijria inayosadifiana na tarehe Mosi Mei mwaka 2022.
Siku kama ya leo miaka 795 iliyopita kwa mujibu wa kalenda ya Hijria, alizaliwa mwanazuoni mahiri wa Kiislamu katika mji wa Hillah Iraq, Ayatullah Jamaluddin Hassan bin Yusuf mwenye lakabu ya Allamah Hilli. Awali alisoma kwa baba yake na mjomba wake na akiwa katika rika la ujana alikuwa tayari amefanikiwa kufikia daraja za juu za elimu katika taaluma kama fikihi, usul Fikih, hadithi na kadhalika. Mwanazuoni huyo alikuwa hodari pia katika uga wa uandishi. Miongoni mwa vitabu vya Allamah Hilli ni Tadhkiratul al-Fuqahaaa, Irshadul Adh'han, na Kashful Murad. Alimu huyo aliaga dunia mwaka 726 Hijria.

Miaka 636 iliyopita, alifariki dunia Nassirddin Muhammad maarufu kwa Ibn Furat, faqih, mwanahistoria na khatibu wa nchini Misri. Ibn Furat alizaliwa mjini Cairo mwaka 735 Hijiria na kuanza masomo yake akiwa kijana mdogo. Msomi huyo alijikita sana katika masuala ya historia, kiasi cha kumfanya aandike vitabu mbalimbali katika uwanja huo. Miongoni mwa athari muhimu za Ibn Furat ni pamoja na kitabu kiitwacho ‘Taarikhud-Duwal wal-Muluuk’, kitabu ambacho kimeshamili historia na matukio ya karne ya sita Hijria.

Siku kama ya leo miaka 133 iliyopita yaani tarehe Mosi Mei 1889, ilitangazwa rasmi kuwa 'Siku ya Wafanyakazi Duniani'. Tarehe Mosi Mei 1886, zaidi ya wafanyakazi elfu 40 walifanya maandamano katika mji wa Chicago nchini Marekani kwa shabaha ya kudai haki zao. Wafanyakazi hao walitaka nyongeza za mishahara, kuboreshwa suhula za maeneo yao ya kazi na uadilifu kazini. Maandamano hayo yaliingiliwa na askari polisi, na matokeo yake yakawa ni idadi kadhaa ya wafanyakazi hao kuuawa na wengine kujeruhiwa.

Katika siku kama ya leo miaka 126 iliyopita, Naser al-Din Shah Qajar, mfalme wanne wa ukoo wa Qajar nchini Iran aliuawa na hivyo kuhitimisha kipindi cha giza cha miaka 50 cha historia ya Iran. Tukio hilo liliandaa uwanja wa kutokea Mapinduzi ya kupigania katiba. Naser al-Din Shah Qajar aliauawa kwa kupigwa risasi na Mirza Reza Kermani mpigania ukombozi. Reza Kerman alikuwa mmoja wa wafuasi wa Sayyid Jamal al-Din Asadabadi. Kipindi kirefu cha utawala wa Naser al-Din Shah Qajar kinahesabiwa kuwa kipindi muhimu cha historia ya Iran katika zama za utawala wa ukoo wa Qajar.
Siku kama ya leo miaka 107 iliyopita, sawa na tarehe Mosi Mei 1915, wakati wa Vita vya Kwanza vya Dunia yalitokea mapigano makali kati ya majeshi ya Urusi na Ujerumani katika eneo la Krakow lililoko nchini Poland. Jeshi la Ujerumani lililoyashinda majeshi ya Urusi kwenye Vita vya Kwanza vya Dunia mwaka 1914, katika vita hivyo kwa kutumia mizinga liliyashinda majeshi ya Urusi na hatimaye kulidhibiti eneo la Poland. Kushindwa kwa majeshi ya Urusi katika Vita vya Kwanza vya Dunia na hali kadhalika hali mbaya iliyokuwemo nchini humo, ni miongoni mwa sababu muhimu za kujiri mapinduzi ya Kikomonisti nchini humo mwaka 1917, na hatimaye nchi hiyo kujiondoa kwenye Vita vya Kwanza vya Dunia.

Na miaka 17 iliyopita katika siku kama hii, tarehe Mosi Mei 2004, nchi nyingine 10 za Ulaya zilijiunga na Umoja wa Ulaya na kufikisha jumla ya nchi 25 wanachama wa umoja huo. Nchi hizo ni Estonia, Latvia, Lithuania, Poland, Jamhuri ya Czeck, Slovakia, Hungary, Slovenia, Cyprus, na Malta. Licha ya kuwa kujiunga nchi hizo kulihesabiwa na jumuiya hiyo kuwa moja ya mafanikio, lakini kuna ufa wa kisiasa, kiuchumi na kijamii kati ya nchi wanachama wa zamani na wapya. Vilevile mwaka 2007, nchi za Romania na Bulgaria zilijiunga na umoja huo na jumla ya nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya kufikia 27.