Sibtain katika Qur'ani na Hadithi
Hassanain katika Aya inayosema: Mtume ameamini yaliyoteremshwa kwake kutoka kwa Mola wake, na Waumini vile vile
Assalaam Alaykum wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu inayokutangazieni kutoka mjini Tehran. Tunakukaribisheni katika kipindi kingine cha Sibtain katika Qur'ani na Hadithi, hii ikiwa ni sehemu ya nne ya kipindi hiki. Kipindi cha leo kitajadili moja ya Aya za Kitabu kitakatidu cha Qur'ani inayosema: Mtume ameamini yaliyoteremshwa kwake kutoka kwa Mola wake, na Waumini vile vile. Wote wamemuamini Mwenyezi Mungu, na Malaika wake, na Vitabu vyake na Mitume wake. Hatutafautishi baina ya yeyote katika Mitume wake (2:285).
Tunapasa kuzingatia hapa nukta hii muhimu na ya dharura wapenzi wasikilizaji kwamba, si kila wakati ambapo majina ya watu wanaokusudiwa katika Aya tukufu za Qur'ani, akiwemo Mtume Mtukufu (saw) na Ahlu Beit wake watoharifu (as), hutajwa moja kwa moja, ila ni kwamba ni Riwaya zinazofafanua maana ya kuteremshwa Aya hizo ndizo hutafsiri, kuelekeza na kutufafanulia makusudio ya Aya hizo. Riwaya na Hadithi hizo huweka wazi na kutaja moja kwa moja majina ya watu waliokusudiwa kwenye Aya hizo. Ukweli huu haupatikani katika vitabu na marejeo ya Mashia pekee bali unapatikana pia katika vitabu na marejeo ya Waislamu wa madhehebu zote za Kiislamu, na hilo linatokana na wingi wa Hadithi hizo na kukubalika kwake na Waislamu wote na hasa wasomi miongoni mwao.
Na Aya tukufu tunayoijadili pamoja na ile inayifuata ambayo ni Aya ya mwisho ya Surat al-Baqarah zinatajwa kuwa miongoni mwa Aya bora na tukufu zaidi katika Qur'ani Tukufu, kwa mujibu wa wafasiri wa Qur'ani, kutokana na kuwa zimebeba ujumbe mzito unaojumuisha ukamilifu na saada na vilevile kutoa muhtasari wa Sura hiyo kwa njia ya kuvutia mno. Aya hizi zina fadhila na taathira muhimu kama zinavyoashiria ukweli huo Hadithi za Mtume Mtukufu, na zimewekwa chini ya Arshi kutokana na utukufu wazo mbele ya Mwenyezi Mungu.
***********
Na sasa ndugu wasikilizaji, tungependa kujua kwa pamoja maana na makusudio ya Ayah hii takatifu. Aya hii inasema bayana na kuthibitisha ukweli kwamba Mtume Mtukufu na Waumini wameamini kile amabcho kiliteremshwa kwao kutoka kwa Mola wao. Mtume na waumini wengine wanazungumziwa mahsusi katika Aya hii kutokana na umuhimu wa Imani kwa Mwenyezi Mungu na kwamba utume na ujumbe wake ndio njia ya kumfikia Yeye Mwenyezi Mungu na kuwa yeye Mtume ndiye wa kwanza kati ya Waumini. Suala hilo pia linaashiria udharura wa kuzingatiwa imani yake na wakati huohuo ni alama ya heshima na utukufu alionao Mtume (saw) mbele ya Mungu Muumba. Madhumuni ya yaliyoteremshwa kwake, ni yale yote aliyoteremshiwa kupitia Wahyi ikiwa ni pamoja na maarifa, hukumu za kisheria, sunna na mambo mengineo. Na kauli ya Mwenyezi Mungu inayosema: Wote wamemuamini Mwenyezi Mungu, na Malaika wake, na Vitabu vyake na Mitume wake, inabainisha hali ya Mtume na Waumini vile vile kutoa ufafanuzi zaidi baada ya kulizungumzia suala hilo kwa ujumla. Inasisitiza umuhimu na utukufu wa imani. Kufikia hapa wapenzi wasikilizaji, bado hatujawafahamu Waumini waliokusudiwa katika Aya hii. Je, ni nani hao? Je, ni waumini wote au ni watu maalumu katika waumini? Jibu la maswali haya liko wazi kabisa katika Hadithi inayofuata na ambayo imenukuliwa na fakihi wa Kihanafi al-Muwafiq bin Ahmad al-Makki al-Khawarazmi katika kitabu chake cha Maqtal al-Hassan (as) na katika kitabu cha msomi wa Kishafii' as-Sheikh Muhammad bin Ibrahim al-Hamuwaini al-Juwaini katika kitabu chake cha Faraid as-Simtain fii Fadhail al-Murtadha wal Batul wa as-Sibtain katika upokezi wao wa Riwaya inayomalizikia kwa Huraith Abu Sulami, mchungaji wa ngamia za Mtume (saw). Anasema kwamba alimsikia Mtume Mtukufu (saw) akisema: 'Usiku ule wa Miiraj (alipopaishwa Mtume kwenda mbinguni) Mwenyezi Mungu Mtukufu aliniambia: Mtume ameamini yaliyoteremshwa kwake kutoka kwa Mola wake. Nikauliza: Na Waumini vilevile (wameamini)? Akajibu: Umesema kweli ewe Muhammad! Hivyo umemteua nani kuwa khalifa wa umma wako? Akajibu: Mbora wao. Akauliza: Ali bin Abi Talib? Nikasema: Ndio, ewe Mola! Akasema: Ewe Muhammad! Nilitazama ardhini na nikakuteuwa wewe. Nilikupa jina ambalo lilitokana na moja ya majina yangu ili nisitajwe sehemu yoyote ile ila na wewe pia unatajwa hapo pamoja na mimi. Mimi ni Mahmoud na wewe ni Muhammad. Kisha nikatazama tena ardhini, na kumteua humo Ali, na nikamchagulia yeye vilevile jina linalotokana na majina yangu. Mimi ni Aali (wa juu zaidi) na yeye ni Ali. Ewe Muhammad! Mimi nimekuumba wewe, Ali, Fatwimah, Hassan na Hussein kutokana na mzuka wa nuru yangu. Niliweka wilaya yenu mbele ya watu (viumbe) wa mbinguni na ardhini, hivyo wale wanaoikubali huwa ni Waumini mbele yangu na wanaoikataa huwa ni katika makafiri. Ewe Muhammad! Hata kama mja miongoni mwa waja wangu ataniabudu hadi akazirai au akachoka kupita kiasi, mfano wa kiriba cha maji kilichochakaa (kikuukuu), lakini akawa anapinga wilaya yenu, kamwe sitamsamehe dhambi zake, hadi akubali wilaya yenu. Ewe Muhammad! Je, unataka kuwaona? Nikasema: Ndio. Akaniambia: Tazama upande wa kulia wa Arshi. Nikatazama huko na kuwaona Ali, Fatwimah, al-Hassan, al-Hussein, Ali bin al-Hussein, Muhammad bin Ali, Ja'ffar bin Muhammad, Musa bin Ja'ffar, Ali bin Musa, Muhammad bin Ali, Ali bin Muhammad, al-Hassan bin Ali na Mahdi wakiwa katika anga iliyojaa nuru huku wakiwa wamesimama wanaswali. Mahdi alikuwa katikati yao akiwa anang'ara mfano wa nyota inayomeremeta. Akasema (Mwenyezi Mungu Mtukufu): Ewe Muhammad! Hawa ndio Mahujja wangu na yule ndiye kiongozi anayetokana na Aali zako. Ewe Muhammad! Yeye ndiye Hujja wa wajibu (anayepaswa kufuatwa) kwa marafiki zangu (waja wema) na mlipiza kisasi kwa maadui zangu.'
*************
Haya wasikilizaji wapenzi ndio mambo yaliyonukuliwa na al-Juwayni as-Shafii' na Khawarazmi al-Hanafi na wawili hawa kunukuliwa na al-Qanduzi al-Hanafi katika kitabu chake cha Yanabiu al-Mawadda Lidhawi al-Qurba. Hadithi hii pia imenukuliwa na Ibn Shaadhan katika wanazuoni wa Kishia katika kitabu chake cha Manaqib al-Ma'tu kupitia njia za kisuni, kupitia mapokezi yanayomalizikia kwa Abu Sulami Mchungaji, na Sheikh at-Tousi katika kitabu chake cha al-Ghaiba, mtafiti na mfasiri mashuhuri wa Qur'ani Tukufu na as-Sayyid Hashim al-Bahrani katika tafsiri yake ya al-Burhan inayotegemea sana mapokezi ya Hadithi. Tukitizama kwa makini wapenzi wasikilizaji, katika baadhi ya vitabu vya wanazuoni mashuhuri wa Kiislamu tunaona kwamba Mtume Mtukufu (saw) alipouliza, na je, Waumini vilevile? Alikusudia kwamba hakuwa peke yake aliyeamini yale aliyoteremshiwa bali waumini wengine waliamini pamoja naye mambo hayo, akimkusudia Imam Ali na kizazi chake kitoharifu (as). Na tokea hapo mazungumzo yakawa ni juu ya watukufu hao (as) moja kwa moja. Hivyo Waumini wanaokusudiwa katika Aya tuliyotangulia kuisoma, ni watukufu hao wa Ahlul Beit wa Mtume kama tulivyoona katika Hadithi
tuliyoijadili, kwa sababu wao ndio misdaki halisi na ya wazi zaidi kuhusu waumini duniani.
Akiwa katika safari ya Miiraj, Mtume Mtukufu (saw) alifunuliwa na kudhihirishiwa mambo mengi ya ghaibu, ya baadaye na yale yanayohusiana na ujumbe wake ikiwa ni pamoja na kufahamishwa mawalii na makhalifa wake hata kabla ya kuumbwa kwao humu duniani, na hiyo ni moja ya dalili za kuthibitisha utume wake mtukufu kwa walimwengu.
Na hadi hapa wapenzi wasikilizaji, ndio tunafikia mwisho wa kipindi hiki cha Sibtain katika Qur'ani na Hadithi kwa juma hili. Basi hadi tutakapojaliwa kukutana tena juma lijalo, tunakuageni nyote kwa kusema, Wassalaam Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh.