Jun 22, 2022 06:46 UTC
  • Hassanain (Imam Hassan na Hussein (as)) katika Aya ya Mubahala 1

Assalaam Alaykum wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inayokutangazieni kutoka mjini Tehran. Tunakukaribisheni tena katika kipindi hiki ambapo kwa leo tutajadili Aya nyingine inayozungumzia utukufu wa Ahlul Bait (as), yaani Watu wa Nyumba Tukufu ya Mtume wa Mwenyezi Mungu Subhanahu wa Taala.

Mwenyezi Mungu alimuhutubu Mtume wake Muhammad al-Mustafa (saw) akiwa katika hali ya mubahala (kulaaniana na Watu wa Kitabu/Wakristo) kwa kumwambia: Watakaokuhoji katika haya baada ya kukufikia elimu hii waambie: Njooni tuwaite watoto wetu na watoto wenu, na wanawake zetu na wanawake zenu, na sisi wenyewe na nyinyi wenyewe, kisha tuombe kwa unyenyekevu tutake laana ya Mwenyezi Mungu iwashukie waongo.

Kwanza, ndugu wasikilizaji tunapasa kujua maana ya neno Mubahala lililotumika katika Aya hii kwa maana ya kuomba kwa unyenyekevu. Inasemekana kuwa maana yake halisi ni kukusanyika sehemu fulani watu wanaojadiliana kuhusu suala fulani la kidini, na kisha kumuomba Mwenyezi Mungu kwa unyenyekevu ili apate kudhalilisha, kulaani na kumuadhibu anayesema uongo kuhusiana na suala hilo. Mubahala hufanyika kwa lengo la kubatilisha madai ya uongo, kwa sababu huo huwa ni uwanja wa mjadala muhimu na nyeti ambao haumuruhusu mtu yoyote kuropokwa na kutamka maneno yasiyo na msingi wala mantiki. Ni katika mubahala huo ndipo Mtume Mtukufu (saw) alipata kuthibitisha ukweli wa utume wake na kuthibitisha madai yasiyo na ukweli ya waongo na wapotovu. Mtume (saw) aliwafikishia Manaswara yaani Wakristo wa Najran ujumbe wa kufanya nao Mubahala kama alivyoamrishwa na Mwenyezi Mungu. Hata hivyo Wakristo hao hawakuharakisha jambo hilo bali walimwomba Mtume muhala wa kwenda kushauriana na wakubwa wao wa kidini kuhusiana na suala hilo. Mtume aliwapa fursa ya kufanya hivyo nao wakawa wamefikia uamuzi fulani. Je, uamuzi huo ulikuwa ni upi?

Walisema: 'Iwapo Muhammad (saw) atakuja akiwa ameandamana na watu wengi wanaopiga makelele na mayowe kwa lengo la kututia hofu, tutajadiliana na kulaaniana naye lakini iwapo atakuja akiwa na watu wachache tu wa Nyumba yake na watoto wake wadogo, tutajiepusha kujadiliana naye.' Walishanga kumwona Mtume (saw) akiwa amefika mahala pale kiwa ameandamana na watu wanne tu wa Nyumba yake. Je, walikuwa nani hao, na ni kwa nini aliwachagua hao tu bila ya kuwajumuisha watu wengine?

****************

Ndugu wasikilizaji, Mtume Mtukufu (saw) alituma pambizoni mwa Bara Arabu na nje ya bara hilo jumbe ambazo zilikuwa zikiita watu katika mambo matatu: Kuitikia dini tukufu ya Mwenyezi Mungu, kufunga mkataba na Uislamu au kujitayarisha kwa ajili ya vita. Miongoni mwa jumbe hizo ni ule ujumbe uliotumwa kwa maaskofu wa Wakristo wa eneo la Najran. Waliandaa kongamano ambalo lilichukua muda mrefu kumalizika. Kisha wakafika kwa Mtume wakiwa na wakuu wao kwa ajili ya kuchunguza na kuhakiki utume wa Mtume Muhammad al- Mustafa (saw), baada ya kuwa tayari walikuwa wamesoma jina na sifa zake katika vitabu vya Adam, Seth, Ibrahim, Musa na Isa (as). Kando ya jina la Mtume (saw) kulikuwa na majina ya watukufu wengine na miongoni mwa maneno ya Mwenyezi Mungu yaliyokuwa yameandikwa kwenye vitabu hivyo ni:  Huyu ni Ahmad, Bwana wao na Bwana wa viumbe wangu. Nilimteua kutokana na elimu yangu, nikatoa jina lake kutokana na jina langu; mimi ni Mahmoud (anayehimidiwa) naye ni Muhammad, na huyu mwingine ni ndugu na Wasii wake nimemteua apate kumsaidia. Nimejaalia baraka na utoharifu wangu kwenye kizazi chake. Na huyo ni Bibi (mkuu/mbora) wa wanawake na kumbusho la Ahmad, Nabii wangu. Na wawili hawa ni watoto na warithi wao na vyanzo hivi vinavyong'ara na kumeremeta ni waliobakia na warithi wao. Na katika maandiko mengine: Jina lake ni Ahmad mteule kutoka katika kizazi cha Ibrahim, na Mustafa kutoka katika kizazi cha Ismail………. Kizazi chake kitatokana na bibi aliyebarikiwa na mkweli, atapata kutokana na bibi huyo binti ambaye naye atazaa watoto wawili (vijana wawili, Hassan na Hussein) ambao watakuwa mabwana watakaouawa shahidi. Nitajaalia kizazi cha Ahmad kutokana na bibi huyu. Basi heri kwa wawili hao na wale watakaowapenda, watakaoshuhudia zama zao na kuwanusuru!'

Pamoja na uthibitisho huo wote lakini ujumbe wa Wakristo hao ulifika mjini Madina kwa lengo la kuthibitisha jambo hilo. Mazungumzo yalikuwa marefu mno na hasa kuhusiana na Nabii Isa (as). Licha ya kupata uthibitisho na dalili za wazi kuhusiana na jambo walilokuwa wameenda kulihakiki lakini hawakukinaika na wakasalia kukanusha ukweli walioushuhudia kwa macho yao wenyewe. Hapo Mwenyezi Mungu akamteremshia Mtume (saw) Wahyi akimtaka afanya nao Mubahala, yaani kuomba dua kwa unyenyekevu mkubwa na kisha kulaaniana nao. Baada ya kuwasomea Aya ya Mubahala Mtume (saw) aliwaambia kuwa alikuwa ameamrishwa alaaniane nao kwa kuwa walikuwa wamekataa kuukubali ukweli na kuendelea kushikilia misimamo yao ya batili. Wakati ulipowadia, Mtume (saw) alitoka nje huku akiwa amejifunika shuka nzito. Hassan akafika mbele yake naye akamuingiza humo, kisha akafanya hivyo hivyo walipofika mbele yake Hussein, Fatwima na Ali (as). Mtume (saw) akaelekea mbele ya Wakristo akiwa na watu hao wa nyumba yake huku akiwa anasoma Aya ifuatayo: 'Hakika Mwenyezi Mungu anataka kukuondoleeni uchafu, enyi Watu wa Nyumba ya Mtume, na kukutakaseni baarabara, na Kusema: Ewe Mwenyezi Mungu! Hawa ni Ahli zangu.' Mkristo mmoja aliuliza: 'Ni nani hawa ambao wameandamana na Muhammad? Akaambiwa: Huyu ni mtoto wa ami yake na Wasii wake, Ali bin Abi Talib, huyu ni binti yake Fatwimah, na wawili hawa ni Hassan na Hussein.' Kisha Mtume (as) aliwaketisha Hassan na Hussein miguuni kwake, upande wa kulia na kushoto kwake na Ali mbele yake, naye Fatwima akawa nyuma yake.  Aliwaambia (saw): 'Nitakapoomba dua semeni Amin!' Mtume aliinua juu mikono yake mitakatifu na kuwataka wakuu wa Wakristo wafanya naye Mubahala kama alivyoamrishwa na Mwenyezi Mungu. Wakamuuliza Mtume (saw), ni nani hao aliokuwa ameandamana nao kufanya nao Mubahala naye akawajibu: 'Ni wabora wa watu wa ardhini na watukufu zaidi mbele ya Mwenyezi Mungu Mtukufu.' Huku akiwa anawaashiria Ali, Fatwimah, Hassan na Hussein (as). Mmoja wa wakuu hao wa Kikristo akamuuliza tena: 'Je, utafanya nasi mubahala ukiwa na watu hawa?' Mtume akajibu: 'Nam, si nimekujulisheni hilo kitambo? Ndio, naapa kwa yule aliyenipa utume kwa haki, nimeamrishwa nikubahilini (nikufanyieni Mubahala) kupitia watu hawa.' Baada ya kuyasikia hayo wakuu hao wa Kikristo walipatwa na hofu kubwa na rangi zao zikawa zimebadilika kutokana na wasiwasi uliowaingia. Walirejea haraka kwa wenzao ili kushauriana nao jambo la kufanya. Mundhar bin Alqamah aliwakumbusha mambo yaliyo kwenye vitabu vya mababu zao na sifa ambazo huandamana na Manabii ambazo walikuwa wameziona kwa Mtume (saw), na kuwanasihi wasifanye mubahala na Mtume Muhammad (saw), la sivyo, wasingelisalimika wao wala kaumu yao kutokana na adhabu ya Mwenyezi Mungu.

*********

Tunaendelea kujadili Riwaya ya Mubahala ambapo wanazuoni, wafasiri, wanahadithi na wanahistoria mashuhuri wa Kiislamu, bila kujali madhehebu na fikra zao wanasema kwamba Sayyid na Aqib (wakuu wa Kikristo) walipomuuliza Mtume kwa kusema: 'Ewe Abu Qassim! Utatubahili ukiwa na nani?', Naye akawajibu kwa kusema: 'Nitakubahilini kwa wabora wa watu wa ardhini na ambao ni watukufu zaidi mbele ya Mwenyezi Mungu', waliingiwa na hofu na woga mkubwa wakahisi ni kana kwamba ardhi ilikuwa inapasuka na kutaka kuwameza. Walirejea haraka kwa askofu wao na kumuuliza huku wakiwa wamechanganyikiwa: 'Je, unasema nini ewe Abu Haritha?' Aliwajibu bila kuwaficha kwa kusema: 'Nanaziona nyuso ambazo kama Mwenyezi Mungu ataombwa kupitia nyuso hizo, aondoe mlima kutoka sehemu ulipo, bila shaka atafanya hivyo…….. Wallahi, Enyi Wakristo! Mnajua kwamba Muhammad ni Mtume aliyetumwa kwa haki na amekujieni na ujumbe wa haki kama ilivyotabiriwa na mmoja wenu (yaani Isa bin Maryam)….. Ole wenu! Msikubali Mubahala! Msifanye Mubahala, mkaja kuangamia na kutobakia duniani hata Mkristo mmoja, hadi siku ya Kiama!'

Ni wazi kuwa watu hao wote wangeangamia kwa sababu Mwenyezi Mungu alikuwa amemuamuru Mtume wake awabahili Wakristo hao kwa kutumia watu bora na watukufu zaidi kati ya viumbe wake, ambao ni Muhammad kipenzi chake, Ali ambaye ni Wasii wa Mtume (saw), Fatwimah, mbora wa wanawake wa ulimwengu, na wajukuu wa Mtume wake (saw) ambao ni mabwana wa vijana wa Peponi, al-Hassan na al- Hussein (baraka na rehema za Mwenyezi Mungu ziwe juu yao wote), Wassalaam Alaikum Warahmatullahi Wabarakatuh.