Jun 22, 2022 06:51 UTC
  • Sibtain katika Qur'ani na Hadithi

Assalaama Aleikum wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inayokutangazieni kutoka mjini Tehran.

Karibuni kusikiliza kipindi hiki ambacho ni sehemu ya pili ya kipindi cha wiki iliyopita ambapo tulianza kujadili Aya ya Mubahala. Tokea mwanzo wa kipindi hiki cha Sibtain, ambao ni Imam Hassan na Imam Hussein (as), tayari tumejadili fadhila, sifa na cheo cha juu cha kimaanawi cha Ahlul Bait wa Mtume (saw) katika Aya ya Majina, Aya ya Maneno, Aya ya Waumini, Aya ya Tat'hir na Aya ya Mubahala. Maimamu wawili hawa wametajwa katika Aya hizi tukufu na kuashiriwa nafasi yao maalumu na adhimu, hata kabla ya kuzaliwa humu duniani. Nafasi hiyo iliashiriwa na kusisitizwa pia katika sehemu nyingi baada ya kuzaliwa duniani na katika kipindi cha umri wao mdogo, kama tunavyoshuhudia kuhusiana na tukio la Mubahala. Kuhusiana na tukio hili muhimu la kihistoria, wapokezi wa Riwaya, wafasiri wa Qur'ani Tukufu  na wanahistoria wanaafikiana kwamba Aya ya Mwenyezi Mungu inayosema: Watakaokuhoji katika haya baada ya kukufikia elimu hii waambie: Njooni tuwaite watoto wetu na watoto wenu, na wanawake zetu na wanawake zenu, na sisi wenyewe na nyinyi wenyewe, kisha tuombe kwa unyenyekevu tutake laana ya Mwenyezi Mungu iwashukie waongo, iliteremka kuwahusu Imam wawili hawa pamoja na wazazi wao wawili, Ali na Fatwimah, mbora wa wanawake wa dunia wakiwa na Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw). Na hapa huenda swali hili likulizwa kwamba je, ni nani aliyesema hayo na kuyathibitisha? Jibu la swali hili kwa muhtasari ni kwamba, kuna wafasiri wengi wa Qur'ani, wapokezi wa Riwaya na wanahistoria ambao wamezungumzia kwa urefu jambo hili katika vitabu vyao vya kuaminika na hasa vya wanazuoni wa Kisuni kabla ya kuzungumzia wanazuoni wa Kishia. Miongoni mwa wanazuoni hao ni Ahmad bin Hambal katika kitabu chake cha Musnad, Muslim katika Sahihi yake, Tirmidhi katika Sunan yake, Tabari katika Tafsiri yake, Nishaburi Hakim as-Shafii' katika Mustadrak wake, Abu Naim al-Hafidh katika Dalail an-Nubuwwa yake, al-Hasakani al-Janafi katika Shawahid at-Tanzil, Hafidh bin Asakir ad-Dimeshqi as-Shafii' katika Taarikh Madinat ad-Dimeshq, Ibn al-Jauzi, Fakhr ar-Razi, Sibt bin al-Jauzi, Qurtubi, Muhib ad-Deen at-Tabari as-Shafii' na wengine wengi ambao muda wa kipindi hiki hauturuhusu kuwataja wote pamoja na vitabu walivyoandika vinavyothibitisha maana na makusudio ya Aya hii takatifu.

***************

Ndugu wasikilizaji, huenda watu wakauliza kwamba je, ni watoto wapi hao waliokusudiwa katika maneno ya Mwenyezi Mungu anaposema: Waambie: Njooni tuwaite watoto wetu?  Ibn Jauzi Jamad ad-Deen bin Ali ambaye ni wa madhehebu ya Hanafi anasema katika kitabu chake cha Zad al-Masir fi Ilm at-Tafsir kwamba Aya hii ya Waambie: Njooni tuwaite watoto wetu na watoto wenu, ilipoteremka Mtume (saw) aliwaita Ali, Fatwimah, Hassan na Hussein na kusema: 'Allahuma! Hawa ndio Ahli zangu. Naye as-Shaukani anasema latika kitabu chake cha Nail al-Autwar: Muslimi, Tirmidhi, Ibn al-Mundhar, al-Hakim na Baihaqi wamenukuu hadithi kutoka kwa Sa'd bin Abi Waqqas kwamba alisema: Kuhusu Aya hii Waambie: Njooni tuwaite watoto wetu na watoto wenu, Mtume wa Mwenyezi Mungu aliwaita Ali, Fatwimah, Hassan na Hussein na kusema: 'Allahuma! Hawa ndio Ahli zangu.' Naye Jabbir al-Ansari amenukuliwa katika kitabu hicho hicho akibainisha suala hili kwa kusema: 'Watoto wetu' ni Hassan na Hussein na 'Wanawake zetu' ni Fatwimah na 'Sisi' ni Mtume wa Mwenyezi Mungu na Ali.' Na hili ndilo jambo ambalo limesisitizwa na Tabarsi katika kitabu chake cha Maj'maul Bayaan fi Tafsir al-Qur'an ambapo anasema: 'Wafasiri wote wa Qur'ani wameafikiana kwa pamoja kwamba makusudio ya 'Watoto zetu' ni Hassan na Hussein.' Abu Bakr ar-Razi naye anasema: 'Na jambo hili linathibitisha kwamba Hassan na Hussein ni watoto wa Mtume wa Mwenyezi Mungu na kuwa mtoto wa binti kwa hakika ni mtoto wa baba ya binti huyo.'

Nam, ndugu wapenzi, wawili hawa al-Hassan na al-Hussein (as) ni watoto wa Mtume Mtukufu (saw) ambao walitokana na Ali na Fatwimah (as), kwa mujibu wa Qur'ani Tukufu na Sunna za Mtume (saw). Na uana (uzawa) huu unaotokana na Bwana wa Viumbe wote, Muhammad al-Mustafa (saw) ni utukufu, cheo cha hali ya juu na utakaso wa Qur'ani Tukufu kwa Hassan na Hussein (as). Ibn Hajar al-Makki as-Shafii' anasema katika kitabu chake cha as-Swaiqul Muhriqa kwamba: 'Hakika watoto wa Fatwimah na kizazi chake wanaitwa watoto wa Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) na wananasibishwa kwake Mtume kwa njia sahihi ya kinasaba iliyo na faida kubwa ya humu duniani na ya huko Akhera…….' Anaendelea kusema: 'Ali aliwalalamikia watu walioandaa kikao cha Shuraa (yaani kuhusiana na kughusubiwa ukhalifa wake) kwa kuwaambia: 'Ninakukumbusheni maneno ya Mwenyezi Mungu: Je, yuko miongoni mwenu mtu aliyefanywa kuwa sawa na nafsi ya Mtume, na watoto wake kuwa sawa na watoto wa Mtume, na wake zake kuwa sawa na wake za Mtume isipokuwa mimi? Wakasema, Allahumma, hapana!

**************

Na hatimaye, ndugu Waislamu, tunapenda kuzungumzia hapa baadhi ya makusudio ya Aya ya Mubahala ili tupate kunufaika kielimu na baadhi ya makusudio hayo. Baadhi ya makusudio na maana ya Aya hiyo ni kwamba inabainisha ukweli wa ujumbe wa Mtume Mtukufu (saw) na utume wake mtukufu na wa mwisho. Al-Alusi anasema katika Tafsiri yake ya Ruh al-Maani:  'Na kisa hiki cha Mubahala ni dalili ya wazi zaidi inayothibitisha utume wa Muhammad (saw) na utukufu na fadhila za kizazi chake, jambo ambalo halitiliwi shaka na muumini.'

Na hata kabla ya Alusi, wapenzi wasikilizaji, jambo hili lilikuwa tayari limesisitizwa na kuthibitishwa na az-Zamakhshari katika tafsiri yake mashuhuri ya al-Kasshaf ambapo amefafanua maana ya Aya ya Mubahala na Riwaya sahihi zilizopokelewa kuhusiana nayo kwa kusema: 'Na kwenye Aya hii kuna dalili nzito na ya wazi inayothibitisha fadhila na utukufu wa Ahlu Kisaa (as).'

Suala hili, wapenzi wasikilizaji, linazungumzia kwa ujumla watu maalumu wa Nyumba ya Mtume Mtukufu (saw) wakiwemo al-Hassan na al-Hussein (as). Je, watukufu wawili hawa wana nafasi gani maalumu katika Aya hii ya Mubahala? Jambo tunalojifunza kutokana na maana iliyo wazi ya Aya hii ni kwamba watukufu wawili hawa walipewa nafasi maalumu na ya kipekee na kufadhjilishwa na Mwenyezi Mungu juu ya watu wengine wote licha ya umri wao mdogo. Mwenyezi Mungu Mtukufu aliwachagua na kumuamuru Mtume wake (saw) afanye Mubahala na Wakristo wa Najran kupitia kwao katika kipindi hicho nyeti, hatari na muhimu sana katika historia ya Uislamu. Dalili nyingine ni kuwa watukufu wawili hawa wamethibitishwa wazi kuwa ni watoharifu, wema, maasumu bali katika elimu ya Mwenyezi Mungu Mtukufu, ni Maimamu, mabwana wateule, mawasii wakamilifu na wanaoongozwa kwa kila njia na Mwenyezi Mungu. Kuna dalili nyingi mno na za wazi kabisa zinazothibitisha suala hili. Tutatosheka hapa kwa kutaja maneno ya wanazuoni wawili wa kwanza akiwa ni Ibn Abu Ilaan ambaye ni mmoja wa wanazuoni wa maimamu wa Mu'tazila ambaye anasema katika ufafanuzi wake wa Aya ya Mubahala: 'Na jambo hili linathibitisha kwamba Hassan na Hussein walikuwa wamefikia umri wa taklifu yaani umri wa kubaleghe, kwa sababu Mubahala hauwahusishi ila watu waliobaleghe.' Kauli ya pili ni ya mwanazuoni mwingine ambaye anasema: 'Kwa hakika Hassan na Hussein wakiwa na wazazi wao wawili (as) ndio tu waliofaa kuhusishwa kwenye Mubahala katika kivuli cha Mtume Mtukufu (saw) na sio watu wengine. Hii ni kutokana na ukweli kwamba wao ndio viumbe bora zaidi mbele ya Mwenyezi Mungu na watukufu zaidi kwake.

Na kufikia hapa wapenzi wasikilizaji ndio tunafikia mwisho wa kipindi hiki cha Sibtain katika Qur'ani na Hadithi, ambacho mmekuwa mkikitegea siku kupitia Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu inayowatangazia kutoka mjini, Tehran. Basi hadi tutakapokutana tena juma lijalo katika kipindi kingine kama hiki, panapo majaaliwa, tunakuageni nyote kwa kusema, Wassalaam Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh.