Jun 22, 2022 07:03 UTC
  • Sibtain katika Qur'ani na Hadithi 10

Assalaam Alaykum wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inayokutangazieni kutoka mjini Tehran na karibuni kusikilizaji sehemu ya 10 ya kipindi hiki cha Sibtain katika Qur'ani na Hadithi.

Ndugu wasikilizaji, bado tunajadili Aya ya Mawadda au Mapenzi ambayo inazungumzia wajibu na ulazima wa kuwapenda Ahlul Bait wa Mtume Mtukufu (saw) inayosema: Sema: Kwa haya sikuombeni malipo yoyote kwenu ila mapenzi katika ndugu.

Suala hili linaashiria umuhimu wa jambo hili ambalo pia limesisitizwa katika Hadithi nyingi za Mtume ikiwemo ile inayotutaka tulindeni heshima na upendo wake kwa kuwapenda Watu wa Nyumba yake (as). Udharura wa kuwapenda watukufu hao wa Nyumba ya Mtume pia umebainishwa na wanahistoria pamoja na washairi ambao wametunga mashairi na tungo nyingine nyingi za kuenzi na kuwatukuza watukufu hao (as). Tunakukaribiesheni tuendelee kujadili suala hili kupitia Aya tuliyotangulia kuitaja hapo juu pamoja na Hadithi nyingine katika uwanja huu.

*************

Baada ya utangulizi huo mfupi wapenzi wasikilizaji, sasa tunaendelea kujadili utambulisho wa watu hao wa Nyumba ya Mtume (saw) waliozungumziwa katika Aya hiyo. Ni nani watukufu hawa ambao Mwenyezi Mungu amemtaka Mtume wake Mtukufu (saw) awaarifishe kwa wanadamu na kutenga malipo makubwa kwa kila atakayewapenda na kuwanusuru na kuwaadhibu wale watakaowachukia na kuwatenga? Hebu tuchambue baadhi ya vitabu vya wanahistoria na wasomi wakubwa wa Kiislamu ili tupate kujua wanasema nini kuhusiana na utambulisho wa watukufu hao. Ni wazi kuwa uchunguzi na upekuzi wa jambo hili utatusaidia pakubwa kuweza kutekeleza vyema amri ya Mwenyezi Mungu na Mtume wake (saw) wanaotutaka tuwapende na kuwanusuru watukufu hao wa Nyumba ya Mtume (as).

Faqihi wa medhehebu ya Maliki az-Zamakhshari anasema katika Tafsiri yake mashuhuri ya al-Kashif katika kufasiri Aya hii ya Mawadda kwamba Aya hii ilipoteremka, Mtume (saw) aliulizwa ni nani hao ambao mapenzi kwao yamewajibishwa kwa Waislamu naye akajibu kwa kusema: 'Ni Ali, Fatwimah na wana wao wawili wa kiume', yaani al-Hassan na al-Hussein…..Hata kama neno 'mawadda' linatumika katika kamusi za lugha ya Kiarabu kwa maana ya mapenzi na mahaba lakini katika kamusi za kidini linaanisha mapenzi makubwa, uongozi, kusimamia mambo ya watu, kushikamana, kufuata, kuiga, kunusuru, kutetea na kumlinda mtu unayempenda…. Na bila shaka watu waliokusudiwa kupendwa zaidi katika Aya na Riwaya hii ni Ali, Bwana wa mawasii wa Mtume, Fatwimat az-Zahra, mbora wa wake wa ulimwengu na al- Hassan na al-Hussein Mabwana wa Vijna wa Peponi.'

Na hapa ndugu wasikilizaji, inasikitisha kusema kuwa msomi mashuhuri, yaani Fakhr ar-Razi licha ya dalili zote hizi zilizo wazi na ambazo yeye mwenyewe pia amezithibitisha, lakini hakukubali wala kukiri wilaya na uongozi wa Ahlu Bait wa Mtume (saw). Msomi huyu mpinzani ambaye ni mashuhuri kwa hila na kutilia shaka mambo yaliyo wazi kabisa na yanayokubaliwa na wote, kwa ajili ya kupotosha ukweli na hakika ameandika katika Tafsiri yake mashuhuri ya al-Kabir katika kufasiri Aya ya Mawadda kama ifuatavyo: Imethibiti kwamba wanne hawa (yaani watu wa karibu ya Mtume waliokusudiwa katika Aya ya Mawadda….ni: Ali, Fatwimah, al-Hassan na al-Hussein) ndio watu wa karibu ya Mtume, na hili likithibiti, basi wanapaswa kuonyeshwa heshima kubwa. Na dalili ya kutengewe heshima hiyo kubwa inatokana na mambo kadhaa: Ya kwanza ni kauli ya Mwenyezi Mungu inayosema: Ila mapenzi katika ndugu, na hilo linatokana na tuliyoyazungumzia huko nyuma kwamba 'Aali za Muhammad (as) ni wale wanaorejesha mambo yao kwa Mtume (saw)'. Hivyo wale ambao kiwango cha urejeshaji wa mambo yao kwa Mtume kilikuwa kikubwa na kikamilifu zaidi basi hao ndio waliokuwa Aali za Mtume. Na wala hakuna shaka kwamba Fatwima, Ali na Hassan na Hussein (as) ndio waliokuwa na uhusiano mkubwa zaidi na Mtume wa Mweyezi Mungu, na hili linathibitishwa na mapokezi mengi ya kuaminika, hivyo wao ndio wanaopaswa kuwa Aal. Jambo la pili ni jwamba hakuna shaka kuwa Mtume (saw) alimpenda sana Fatwima na akisema: 'Fatwimah ni sehemu ya mwili wangu, linaniudhi linalomuudhi yeye.'

Na imethibiti kutokana na Riwaya nyingi za kuaminika zilizopokelewa kutoka kwa Mtume (saw) kwamba alikuwa akimpenda Ali, Hassan na Hussein (as)……. Na iwapo hilo litathibiti – na maneno haya mpenzi msikilizaji bado ni ya Fakhr ar-Razi – basi umma mzima nao utawajibika kuwapenda kutokana na kauli ya Mwenyezi Mungu katika Aya ya 158 ya Surat al-Ahzab inayosema: Basi mwaminini Mwenyezi Mungu na Mtume wake asiyejua kusoma wala kuandika, ambaye anamwamini Mwenyezi Mungu na maneno yake. Na mfuateni yeye ili mpate kuongoka.'

*************

Ndugu wasikilizaji, kuna Aya mbili hizi ambazo humfanya msomaji kusimama kidogo kutafakari kidogo. Aya hizo zinafanana mwanzoni na kutofautiana kimaneno mwishoni. Ya kwanza ni Aya ya 18 ya Surat an-Nahl inayosema: Na mkizihisabu neema za Mwenyezi Mungu, hamuwezi kuzidhibiti. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa maghfira, Mwenye kurehemu. Na ya pili ni Aya ya 34 ya Surat Ibrahim ambayo inasema: Na mkihisabu neema za Mwenyezi Mungu hamuwezi kuzidhibiti. Hakika mwanaadamu ni dhalimu mkubwa, mwingi wa kukufuru.

Nam, ndugu wasikilizaji, ni wazi kuwa neema za Mwenyezi Mungu ni nyingi mno kiasi kwamba mwanadamu hana hata uwezo wa kuzihesabau kama zinavyobainisha wazi Aya hizi takatifu, na neema kubwa kati ya hizo bila shaka ni neema ya imani juu ya upweke wa Mwenyezi Mungu, utume wa Mtume wake Mtukufu (saw) na Maimamu ambao ni makhalifa wake na ambao ndio watakaowaongoza wanadamu kwenye heri na saada hadi Siku ya Kiama. Kuhusiana na suala hilo, Mwenyezi Mungu ameahidi kwamba atawaghufiria wanadamu dhambi zao zote iwapo wataamua kutubu dhambi na kumfuata Mtume Muhammad (saw) na Aali zake watoharifu (as) pamoja na kudumu katika kuwapenda, kuwafuata na kuwanusuru katika kila hali. Huo ndio ukubwa wa rehema, neema na maghufira ya Mwenyezi Mungu Mtukufu kwa waja wake humu duniani. Ni wazi kuwa iwapo wanadamu watekwenda kinyume na neema hiyo na kuamua kumuasi Muumba wao kwa kuishi nje ya mipaka ya imani na kupuuza miongozo ya Mtume (saw) pamoja na mapenzi kwa Ahlu Bait wake (as), basi watakuwa wamejidhulumu wao wenyewe na kukufuru neema za Mwenyezi Mungu. Bila shaka watakuwa wamepuuza na kutozingatia malipo aliyotaka apewe Mtume (saw) kama alama ya kumshukuru kutokana na juhudi na wema mkubwa aliowafanyia katika kuwafikishia ujumbe muhimu na adhimu wa mbinguni.

Hafidh al-Askalani al-Hanafi ameashirika katika kitabu chake cha Shawahid at-Tanzil Hadithi iliyopokelewa kutoka kwa Ibn Abbas akisema: 'Maansar walishauriana baina yao kuwa wakusanye mali ambapo Mtume (saw) angeweza kuitumia (katika shughuli zake za ulinganiaji). Walimwambia Mtume (saw): Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu! Tunapenda kukusanyia katika mali zetu kitu kidogo ambacho kitakusaidia (katika shughuli zako za ulinganiaji). Hapo Mwenyezi Mungu akateremsha Aya inayosema: Sema: Kwa haya sikuombeni malipo yoyote kwenu ila mapenzi katika ndugu.'

Na Hadithi sahihi zaidi ni ile iliyonukuliwa na al-Huwaizi katika Tafsiri ya Nur at-Thaqalain katika kufafanua Aya ya Mawadda. Ananukuu Hadithi iliyopokelewa kutoka kwa Imam Swadiq akisema kwamba Mtume aliporejea Madina akitoka kwenye Hija yake ya mwisho mjini Makka, Maansar walifika mbele yake na kushukuru neema kubwa aliyowapa Menyezi Mungu kwa kuwatumia Mtume (saw) ambaye aliwaonyesha njia nyoofu ya saada na kuwadhalilisha maadui wao kupitia kwake. Baada ya kutoa shukrani zao kwake, walipendekeza wampe nusu ya mali zao ili apate kuitumia katika kulisha, kukirimu na kuwashughulikia wageni wengi waliokuwa wakifika kwake kutoka katika mji mtakatifu wa Makka. Kabla ya kuwajibu Mtume alisubiri kidogo ili apate jibu kutoka kwa Mwenyezi Mungu kuhusiana na suala hilo. Muda si mrefu, Malaika Jibril (as) aliteremka na kumletea Aya ifuatayo: Sema: Kwa haya sikuombeni malipo yoyote kwenu ila mapenzi katika ndugu, na hapo akawa amekataa kuchukua mali hiyo ya Maansar.

Na kwa hayo wapensi wasikilizaji ndio tunafikia mwisho wa kipindi hiki cha Sibtain katika Qur'ani na Hadithi ambacho kimekujieni kupitia Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inayokutangazieni kutoka mjini Tehran. Basi hadi tutakapokutana tena juma lijalo panapo maaliwa, tunakuageni nyote kwa kusema, Wassalaam Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh.