Alkhamisi tarehe 7 Julai 2022
Leo ni Alkhamisi tarehe 7 Dhulhija 1443 Hijria sawa na Julai 7 mwaka 2022.
Siku kama ya leo, tarehe 7 Dhulhija miaka 1329 iliyopita, aliuawa shahidi Imam Muhammad Baqir AS, mjukuu mtukufu wa Mtume Muhammad (SAW) na mmoja wa Maimamu watoharifu katika kizazi chake. Imam Baqir AS alizaliwa katika mji mtakatifu wa Madina na kupata umashuhuri katika uwanja wa elimu, ambapo alikuwa akijibu maswali na masuala magumu ya zama, na kwa sababu hiyo alipewa lakabu ya "Baqir", yaani mchimbua elimu. Kipindi cha uimamu wa mtukufu huyo kiliambatana na kudhoofika kwa utawala wa Bani Umayyah, suala ambalo lilimpa fursa nzuri ya kulea Waislamu wa zama hizo kifikra na kielimu. Imam Baqir (as) alisifika kwa ukarimu, kuwasamehe waliomkosea, kuwasaidia masikini na kuwatembelea wagonjwa. Redio Tehran inatoa mkono wa pole kwa Waislamu wote kwa mnasaba huu mchungu wa kuuliwa shahidi Imam Baqir (AS).

Miaka 215 iliyopita mwafaka na siku kama hii ya leo, ulitiwa saini mkataba wa kihistoria wa Tilsit katika mji wenye jina hilo huko Russia kati ya Alexander wa Kwanza, mfalme wa Russia na Napoleon Bonaparte wa Ufaransa. Kwa mujibu wa mkataba huo Urusi na Ufaransa zilikubaliana kuwa, ikiwa nchi yoyote ingeishambulia nchi moja wapo kati ya hizo, zingesaidiana kumpiga adui. Mkataba huo wa urafiki, uliendelea hadi mwaka 1810.
Katika siku kama ya leo miaka 100 iliyopita, tarehe 16 Tir 1301 Hijiria Shamsia, alifariki dunia Ayatullah Zainul Abidin Marandi. Msomi huyo mkubwa alisoma elimu za awali katika mji aliozaliwa wa Marand, huko katika mkoa wa Azerbaijan Mashariki nchini Iran. Baada ya hapo alielekea mjini Najaf, Iraq na kupata kusoma kwa maulama wakubwa kama vile Ayatullah Sayyid Mohammed Hassan Husayni Nouri Shirazi na Habib Allah Rashti. Baada ya muda fulani Ayatullah Marandi alikuwa marjaa taqlidi katika maeneo ya Azerbaijan na hatimaye akafariki dunia siku kama ya leo akiwa na umri wa miaka 72 na kuzikwa katika makaburi ya Wadi-al Salaam mjini Najaf.

Siku kama ya leo miaka 85 iliyopita, alifariki dunia Ayatullah Mirza Abul-Huda Karbasi, msomi mkubwa wa fiqhi na masomo mengine ya kidini. Baada ya kuhitimu masomo ya awali ya dini ya Kiislamu alielekea mjini Najaf, Iraq kwa ajili ya kukamilisha masomo yake ya kidini yapata mwaka 1281 Hijiria Shamsia, ambapo aliweza kusoma masomo ya ngazi ya juu ya usulu fiqhi na fiqhi kwa maulama wakubwa wa mji huo kama vile Ayatullah Akhund Mohammad Kazem Khorasani na Mohammed Kazem Yazdi. Aidha Ayatullah Mirza Abul-Huda Karbasi ameandika vitabu kadhaa kama vile 'Kifaayatul-Usul' 'al-Badrut-Tamaam' 'Zallatul-Aqdaam' na 'al-Fawaaidur-Rijaaliyah.'
Katika siku kama ya leo miaka 44 iliyopita, visiwa vya Solomon vilivyoko kaskazini mashariki mwa Australia katika bahari ya Pacific vilipata uhuru. Visiwa hivyo viligunduliwa na watu kutoka Ulaya mwaka 1567. Mwaka 1885 Ujerumani ilidai umiliki wa visiwa vya kaskazini mwa Solomon na ndiyo maana ikachukua hatua ya kuvishambulia na kisha kuvikalia kwa mabavu. Muongo mmoja baadaye, Uingereza ilivishambulia visiwa hivyo na kuvidhibiti. Harakati ya kupigania uhuru ilianzishwa katika visiwa hivyo baada ya Vita Vikuu vya Pili vya Dunia na kuzaa matunda katika tarehe kama ya leo ambapo visiwa hivyo vilipata uhuru.

Na tarehe 7 Julai mwaka 2005 kulitokea mlipuko katika basi na milipuko mingine katika vituo vitatu vya treni ya chini ya ardhi katikati mwa mji mkuu wa Uingereza, London na kusababisha vifo vya watu 50 na wengine wapatao 700 kujeruhiwa. Mashambulio hayo yalifanywa sambamba na kikao cha Viongozi wa Nchi Tajiri Kiviwanda Duniani G8 huko nchini Scotland kaskazini kwa Uingereza. Mashambulio hayo ya mabomu yalitekelezwa ili kupinga ushirikiano wa London na Washington katika kuikalia kwa mabavu Afghanistran na Iraq na kuuawa kiholela wananchi wa nchi hizo. Serikali ya Uingereza ilidai kwamba, Waislamu walihusika na tukio hilo, na kwa muktadha huo mashinikizo dhidi ya Waislamu wa Uingereza yaliyoanza baada ya mashambulio ya Septemba 11, 2001 yakashadidi zaidi.