Ijumaa, tarehe 8 Julai 2022
Leo ni Ijumaa tarehe 8 Dhulhija 1443 Hijria sawa na Julai 8 mwaka 2022.
Leo tarehe 8 Dhulhija ni siku ya Tarwiya. Siku hii imepewa jina la siku ya Tarwiya kwa maana ya kijitosheleza kwa maji kwa sababu katika zama za Nabii Ibrahim (as) maji hayakuwa yakipatikana katika jangwa na Arafat na kwa msingi huo watu walikuwa wakipeleka maji eneo la Arafat kutoka Makka tarehe 8 Dhulhija wakijitayarisha kwa ajili ya mahitaji ya maji ya kesho yake yaani tarehe tisa.
Katika siku kama ya leo miaka 1383 iliyopita kulingana na kalenda ya Hijria, Imam Hussein bin Ali (AS), mjukuu wa Mtume Muhammad SAW aliondoka Makka na kuelekea Kufa nchini Iraq baada ya kukataa kumbai na kutoa kiapo cha utiifu kwa Yazid bin Muawiya. Miezi minne kabla ya hapo, Imam Hussein alikuwa amewasili mjini Makka akiwa pamoja na familia yake na alikitumia kipindi cha kuweko waumini waliotoka pembe mbalimbali za dunia kwa ajili ya kufanya ziara katika Nyumba hiyo ya Mwenyezi Mungu, kuwaamsha na kuwabainishia dhulma na ufisadi mkubwa uliokuwa ukifanywa wa utawala wa Yazid mwana wa Muawiya. Wakati huo huo kutokana na wito wa mara kwa mara wa watu wa Kufa na njama za utawala wa Yazidi za kutaka kumuuwa, Imam Hussein aliondoka Makka na kueleka Kufa.

Katika siku kama ya leo miaka 37 iliyopita alifariki dunia Ayatullah Muhammad Mahdi Rabbani Amlashi aalimu na mujahidi wa Kiirani. Ayatullah Amlashi alizaliwa mwaka 1313 Hijria Shamsiya katika familia ya kidini katika mji mtukufu wa Qum na kuanza masomo ya kidini katika mji huo. Mwanazuoni huyo alipambana vilivyo kwa miaka mingi katika njia ya kuutetea Uislamu na kulinda thamani zake. Kama walivyokuwa viongozi na wafuasi wengine wa Imam Khomeini Mwenyezi Mungu amrehemu mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Ayatullah Rabbani Amlashi katika uhai wake hakuacha kufanya juhudi za kupambana dhidi ya utawala wa Shah licha ya kufungwa na kubaidishwa.
Siku kama ya leo miaka 28 iliyopita, alifariki dunia Kim Il-sung aliyekuwa Kiongozi na Katibu Mkuu wa Chama cha Kikomonisti wa Korea Kaskazini. Kim Il-sung alizaliwa mwaka 1912. Akiwa na cheo cha ukapteni jeshini alirejea kaskazini mwa nchi hiyo mwaka 1945 akiandamana na jeshi. Alipanda ngazi ya uongozi haraka na akachaguliwa kuwa kiongozi wa chama cha wakomunisti wa nchi hiyo. Mwaka 1948 wakati nchi hiyo ilipoasisiwa na kuwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Watu wa Korea, Kim Il-sung alifikia cheo cha uwaziri mkuu. Katika vita vya Korea, Kim Il-sung aliteuliwa kuwa kamanda mkuu wa majeshi ya nchi hiyo na mwaka 1972 akawa rais wa taifa hilo.