Jul 19, 2022 21:54 UTC
  • Jumatano tarehe 20 Julai 2022

Leo ni Jumatano tarehe 20 Dhulhija 1443 Hijria sawa na Julai 20 mwaka 2022.

Siku kama ya leo miaka 1315 iliyopita alizaliwa Imam Mussa al-Kadhim (as) ambaye ni mmoja kati ya wajukuu watukufu wa Bwana wetu Muhammad (saw). Alilewa na baba yake Imam Ja'far Swadiq (as) na kupata elimu na maarifa ya Kiislamu kutoka kwa mtukufu huyo kwa kipindi cha miaka 20. Baada ya kuuawa shahidi baba yake, Imam Kadhim (as) alishika hatamu za Uimamu na uongozi wa Umma wa Kiislamu kwa kipindi cha miaka 35 na kukabiliana na mashaka mengi. Imam Kadhim (as) alipitisha kipindi kikubwa cha umri wake katika kuwazindua na kuwaelimisha Waislamu maarifa asili ya dini. Suala hili liliwatia hofu kubwa watawala wa Bani Abbas ambao walimkamata na kumfunga jela ili kumuweka mbali na Waislamu waliokuwa na kiu ya maarifa halisi ya dini yao. Imam Kadhim (as) alisifika kwa ukarimu mkubwa, uvumilivu na usamehevu. Tunatoa mkono wa baraka kwa Waislamu wote kwa mnasaba wa kuadhimisha siku hii muhimu ya kuzaliwa mtukufu huyo.

Miaka 212 iliyopita katika siku kama ya leo, uhuru wa Colombia ulitangazwa rasmi. Colombia iligunduliwa mwishoni mwa karne ya 15 na Wahispania na kuanza kukoloniwa. Kuanzia mwishoni mwa karne ya 18, harakati za kupigania uhuru za wananchi wa nchi hiyo ziliongezeka na hatimaye harakati hizo kuzaa matunda katika siku kama ya leo. Hatua ya Napoleon Bonaparte ya kuikalia kwa mabavu Uhispania, ilizipatia fursa nzuri nchi makoloni ya Uhispania ikiwemo Colombia kuzidisha mapambano ya ukombozi. 

Bendera ya Colombia

Katika siku kama ya leo miaka 156 iliyopita, Georg Friedrich Bernhard Riemann, mwanahisabati wa Kijerumani aliaga dunia baada ya kuugua maradhi ya kifua kikuu. Georg Friedrich alizaliwa mwaka 1826 katika mji wa Hanover nchini Ujerumani na baada ya kumaliza masomo yake ya awali aliendelea na masomo ya hisabati. Alipofikisha umri wa miaka 28 Bernard Riemann alikuwa tayari ni mhadhiri wa Chuo Kikuu katika uwanja huo wa hisabati. 

Georg Friedrich Bernhard Riemann

Miaka 85 iliyopita katika siku kama ya leo, alifariki dunia Guglielmo Marconi mvumbuzi wa radio wa Kiitalia akiwa na umri wa miaka 63. Guglielmo alizaliwa mwaka 1874 huku akiwa mtoto wa mfanyabiashara mmoja wa Kiitalia. Marconi alipenda sana kujifunza masuala ya ufundi na sanaa tangu akiwa kijana  mdogo ambapo alianza utafiti wa mawimbi ya sauti. Marconi hatimaye alifanikiwa kuvumbua radio baada ya utafiti wake huo na baadaye akaikamilisha bila ya kutumia waya.

Guglielmo Marconi

Siku kama ya leo miaka 53 iliyopita, kwa mara ya kwanza mwanadamu alifika mwezini. Katika siku hiyo wanaanga wa Kimarekani Neil Armstrong na Edwin Aldrin walitumia chombo cha kusafiria katika anga za mbali kwa jina la Apolo- 11 na kufika mwezini na baadaye wakarejea duniani huku wakiwa na sampuli za mawe na udongo walizokuja nazo katika safari hiyo. Kwa utaratibu huo juhudi kubwa za mwanadamu zilizokuwa zikifanywa kwa muda mrefu kwa lengo la kufikia mwezini zikawa zimezaa matunda.

Neil Armstrong na Edwin Aldrin

Na miaka 48 iliyopita katika siku kama ya leo, wanajeshi wa Uturuki walivamia na kukalia kwa mabavu sehemu ya ardhi ya Cyprus, mashariki mwa kisiwa hicho. Tangu kale Waturuki na Wagiriki wa Cyprus walikuwa wakizozana juu ya namna gani pande mbili hizo zigawane mamlaka ya nchi hiyo.

Bendera ya Cyprus