Jumatano tarehe 3 Agosti mwaka 2022
Leo ni Jumatatu tarehe 5 Mfunguo Nne Muharram 1444 Hijria sawa na tarehe 3 Agosti mwaka 2022.
Siku kama ya leo mika 1383 iliyopita, Ubaidullah bin Ziyad baada ya kutuma kikosi cha askari wengine 1000 kuelekea Karbala kwa ajili ya kupigana vita na mjukuu wa Mtume (saw) Imam Hussein (as), alimpa jukumu Bwana mmoja aliyejulikana kwa jina la Zahr ibn Qais aliyekuwa na wapanda farasi 500 wasimame katika daraja la Sadah katika mji wa Kufa na awazuie watu wanaotaka kutoka katika mji huo na kwenda kuungana na Imam Hussein (as). Mtu aliyejuliana kwa jina la Ammar bin Abi Salaamah aliyekuwa ameazimia kwenda kuungana na Imam Hussein alipambana na Zahr na jeshi lake na kufanikiwa kutoka nje ya Kufa. Baada yake hakuna mtu aliyethubutu kumfuata. Ammar alifanikiwa kufika Karbala na kuungana na Imam Hussein (as) na akiwa huko alifanikiwa kupata daraja kubwa ya kuuliwa shahidi akiwa pamoja na mjukuu wa Mtume. Ammar bin Abi Salaamah alikuwa mmoja kati ya masahaba wa Mtume Muhammad (saw) na watu wa karibu kwa Imam Amirul-Muuminin Ali bin Abi Twalib (as) na alishiriki katika vita vingi akiwa pamoja na matukufu huyo.

Katika siku kama ya leo miaka 530 iliyopita baharia wa Kiitalia Christopher Columbus alianza safari kubwa zaidi ya kiuvumbuzi. Christopher Columbus alipewa jukumu la kuvumbua njia mpya inayoelekea India katika makubaliano yaliyofikiwa kati yake na mfalme na malkia wa Uhispania. Christopher Columbus aliondoka katika bandari ya Paulus huko Uhispania akiwa na meli tatu na mabaharia 120 na hatimaye walifika katika nchi kavu baada ya kuwa baharini kwa siku 33. Baharia huyo wa Kiitalia na wenzake walidhani kuwa wamefika India. Hata hivyo walikuwa wamefika katika kisiwa kilichojulikana kwa jina la Salvador katika bara la Amerika.
Miaka 108 iliyopita katika siku kama hii ya leo Mfereji wa Panama ulifunguliwa baada ya meli ya kwanza kupita katika mfereji huo. Mfereji wa Panama ulianza kujengwa na wahandisi wa Kifaransa na baadaye ujenzi huo ukakamilishwa na Wamarekani. Mfereji wa Panana ulio na urefu wa kilomita 68 unaunganisha bahari mbili za Atlantic na Pacific.
Siku kama ya leo miaka 62 iliyopita, mwafaka na tarehe 3 Agosti 1960, nchi ya Kiafrika ya Niger ilipata uhuru kamili na kuwa mwanachama wa Umoja wa Mataifa. Niger ilikuwa chini ya himaya ya Ufaransa tangu karne ya 18 na mwaka 1922 ikawa koloni rasmi la Wafaransa baada ya nchi hiyo kujenga vituo vyake vya kijeshi nchini humo. Hata hivyo taratibu wananchi wa Niger walianzisha uasi dhidi ya wakoloni wa Kifaransa na hatimaye nchi hiyo ilifanikiwa kupatia uhuru katika siku kama hii ya leo. Niger iko magharibi mwa Afrika na inapakana na Libya, Chad, Mali na Benin.

Miaka 44 iliyopita katika siku kama ya leo, katika hatua yake nyingine ya kigaidi utawala wa Kizayuni wa Israel uliwauwa Izzuddin Qalq mjumbe wa Harakati ya Ukombozi wa Palestina (PLO) na naibu wake huko Paris, Ufaransa. Shirika la ujasusi la utawala wa Kizayuni wa Israel MOSSAD katika miongo miwili ya 70 na 80 liliwauwa kigaidi viongozi wengi wa PLO ili kuidhoofisha harakati hiyo na kuilazimisha kuanzisha mazungumzo eti ya mapatano kati ya Wapalestina na Israel.