Aug 04, 2022 06:58 UTC
  • Sibtain katika Qur'ani na Hadithi

Assalaam Alaykum wasikilizaji wapenzi wa Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inayokutangazieni kutoka mjini Tehran. Ni wasaa mwingine wa kujumuika nanyi katika kipindi kingine cha Sibtain katika Qur'ani na Hadithi ambacho tunatumai kitatunufaisha sote kwa pamoja, karibuni.

Kwa kawaida mataifa huishi na kupitia hatua tatu muhimu katika historia yao. Hatua ya kabla ya utume ni hatua ambapo taifa huwa linaishi katika hali ya upotovu na kuchanganyikiwa na kusubiria jambo fulani. Hatua ya kuishi kwenye hali ya uwepo wa mitume nayo ni hatua ya kupitia mitihani, kipindi cha mpito, mabadiliko na makabiliano ya ndani na nje na kisha ya mwisho ni hatua ya baada ya utume ambacho huwa ni kipindi cha uthabiti au mapinduzi. Hatua hii huwezesha ukweli kudhihirika wazi na kujitenga na unafiki, na hivyo kuliweka taifa katika hali mpya ya uhai. Wakati huo huo hali hii huenda ikalifanya taifa kugawanyika na kuwafanya watu kubuni makaundi tofauti ya kimadhehebu. Je, katika hali hii ni mbinu na njia gani inaweza kutumika ili kunusuru na kuliokoa taifa lisije likatambukia katika matatizo makubwa zaidi?

Ndugu wasikilizaji, Mwenyezi Mungu Mtukufu alitambua vyema kwamba Umma wa Kiislamu ungetumbukia kwenye mtihani mkubwa baada ya kuaga dunia Mtume (saw) na ndio maana akamtaka Mtume abalighi na kuwafikishia Waislamu ujumbe wa kuteuliwa khalifa na mtu ambaye angechukua nafasi yake baada ya yeye kurejea kwa Mola wake. Alimtaka Mtume (saw) atangaze hadharani habari hiyo muhimu na kutoa dhamana kwamba angemkinga na kila baya na maovu ya watu kama tunavyosoma katika 67 ya Surat al-Maida inayosema: Ewe Mtume! Fikisha uliyoteremshiwa kutoka kwa Mola wako Mlezi. Na ikiwa hukufanya hayo basi hukufikisha ujumbe wake. Na Mwenyezi Mungu atakulinda na watu. Hakika Mwenyezi Mungu hawaongoi watu makafiri. Ujumbe na habari hiyo ilikuwa muhimu kiasi kwamba kama Mtume hangeitangaza hadharani basi kazi yote aliyoifanya katika uhai wake wa utume na amabayo iliandamana na mashaka na mateso mengi haingekuwa na maana. Habari hiyo muhimu, wapenzi wasikilizaji, haikuwa nyingine ila ilikuwa ni ya kutangazwa hadharani uongozi na Uimamu wa Imam Ali, Amirul-Muuminina (as), katika kusadikisha yaliyopita, na kuwajibisha yatakayokuja. Alitangaza pia Uimamu wa watoto wake watoharifu (as) ambao walipasa kuchukua uongozi wa Umma wa Kiislamu baada yake. Miongoni mwa watukufu hao walikuwemo al-Hassanain (as) na kwa njia hiyo Mwenyezi Mungu akawa amekamilisha dini yake na kuwatimizia Waislamu, waumini bali watu wote neema yake.

Al-Kulayni ananukuu katika kitabu cha al-Kafi kauli ya Imam Baqir (as) kwamba: “Uislamu umejengwa juu ya mambo matano ambayo ni: Swalah, Zaka, Saumu, Hija na Wilaya.” Akaulizwa: Ni lipi lililo bora zaidi kati ya hayo? Akasema: Wilaya ni bora zaidi, kwa sababu ndio ufunguo wa mengine yaliyosalia, na ni walii ambaye huongoza kuelekea mambo hayo mengine."

Na Imam Ali bin Musa ar-Ridha (as), amenukuliwa akisema katika Hadithi ndefu, kwamba: “Hakika Uimamu ni hadhi ya Mitume na mirathi ya mawasii. Hakika Uimamu ni ukhalifa wa Mwenyezi Mungu na Mtume wake (saw), nafasi ya Amirul Muuminin (as) na urithi wa Hassan na Hussein, amani iwe juu yao. Hakika Uimamu ni hatamu za dini, mfumo wa Waislamu, marekebisho ya dunia na heshima ya waumini…."

Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw), alianza kwa kumtaja Ali, na akamalizia kwa Mahdi, akifafanua majina na vyeo vyao. Alisema Katika khutba tukufu ya al-Ghadir: “Enyi watu! Ninaacha nyuma yangu Uimamu na urithi ambao utaendelea hadi Siku ya Kiyama. Nimeshafikisha ujumbe nilioamrishwa kuufikisha, ikiwa ni hoja kwa kila aliyepo na asiyekuwepo, kwa kila aliyeshuhudia au asiyeshuhudia, awe amezaliwa au la. Basi aliyepo amjulishe asiyekuwepo na mzazi amjulishe mtoto hadi Siku ya Kiyamah. Wataufanya ukhalifa kuwa ni milki na unyakuzi, Mwenyezi Mungu awalaani wanyakuzi na wanyang'anyi."

Enyi watu! Mimi ndio njia ya Mwenyezi Mungu iliyonyooka aliyokuamrisheni kuifuata, kisha Ali baada yangu, kisha wanangu kutoka kizazi chake, maimamu wanaoongoza kwenye haki, na kwayo ni waadilifu…. Enyi watu! Mimi ni Nabii na Ali ni wasii wangu. Imam wa mwisho katika sisi ni al-Qaim al-Mahdi."

**********

Hivyo, ndugu wapenzi, hivi ndivyo Uimamu ulivyoanzia kwa Amirul-Muuminina Ali (as), kisha akawaendea wanawe, wakitanguliwa na Hassan na Hussein (as) kwa amri ya Mwenyezi Mungu ambaye anasema katika Aya ya 36 ya Surat al-Ahzab: Na haiwi kwa Muumini mwanamume wala Muumini mwanamke kuwa na khiari katika jambo, Mwenyezi Mungu na Mtume wake wanapokata shauri katika jambo lao. Na mwenye kumuasi Mwenyezi Mungu na Mtume wake basi hakika amepotea upotofu ulio wazi.

Na Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) amenukuliwa akisema:

"Hakika Mwenyezi Mungu Mtukufu amechagua katika siku Ijumaa, katika miezi Ramadhani, katika mikesha Usiku wa Amri (Lailatul Qadr/Usiku wa Utukufu/Usiku wa Cheo), kutoka kwa Ali al-Hassan na al-Hussein na akawateuwa kutoka kwa al-Hussein mawasii ambao huzuia Kitabu cha Mwenyezi Mungu kupotoshwa na wapotovu, na wizi (kughusubu) unaofanywa na watu wa batili na majahili….."

Na hapa, ndugu wasikilizaji, Imam ar-Ridha (as) anawajibu wale wanaodhani kwamba Uimamu ni miongoni mwa hiari na machaguo ya watu kwa kusema: "Je, wanajua thamani ya uimamu na nafasi yake katika umma, hadi wapewe hiari kuhusu jambo hili? Hakika Uimamu una thamani kubwa zaidi, shani tukufu zaidi nafasi ya juu zaidi, umbali wake (na watu wa kawaida) ni mkubwa zaidi na kina chake ni kikubwa zaidi kadiri kwamba watu hawawezi kukifikia kwa kutumia akili zao au kukidiriki kupitia maoni au kujichagulia wenyewe Imamu.

Mwenyezi Mungu alimpa Uimamu Nabii Ibrahimu Khalil (as) katika daraja na hatua ya tatu baada ya kuwa amempa cheo cha utume na urafiki. Hiyo ilikuwa alama na ishara ya ubora wa heshima aliyopewa Nabii Ibrahim na Mwenyezi Mungu na hivyo kunyanyua nafasi na cheo chake. Alimwambia: Hakika mimi nitakufanya uwe Imamu wa watu. Kisha Mwenyezi Mungu Mtukufu akamtukuza kwa kuufanya Uimamu kuwa miongoni mwa kizazi chake chenye watu wateule na wasafi. Hadi Mwenyezi Mungu alipourithisha Uimamu huo Mtume Mtukufu (saw) kwa kusema: Watu wanaomkaribia zaidi Ibrahim ni wale waliomfuata yeye na Nabii huyu na walioamini. Na Mwenyezi Mungu ndiye Mlinzi wa Waumini. Uimamu ukawa makhsusi kwa ajili yake, hadi Mtume (saw) alipoupata naye akamwachia Ali (as) kwa amri ya Mwenyezi Mungu Mtukufu na kwa msingi wa utaratibu alioufaradhisha. Hivyo ukawa miongoni mwa watoto wake wateule na wema ambao Mwenyezi Mungu aliwapa elimu na imani. Uimamu huo utaendelea kusalia katika kizazi cha Ali (as) hadi Siku ya Kiyama; kwa vile hakuna Mtume mwingine baada ya Muhammad (saw). Hivyo hawa wajinga na majahili wanataka kujichagulia imamu kwa msingi gani?!"