Aug 04, 2022 07:03 UTC
  • Sibtain katika Qur'ani na Hadithi

Assalaam Alaykum wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inayokutangazieni kutoka mjini Tehran. Tuna furaha kujiunga nanyi katika kipindi kingine cha Sibtain katika Qur'ani na Hadithi ambacho tunatumai kitatunufaisha sote kwa pamoja, karibuni.

Wapenzi wasikilizaji, kama anavyosema al-Masoudi katika kitabu chake cha Ithbaat al-Wasiya, Mitume na Mawasii kamwe hawakusitisha wala kusimamisha shughuli zao katika jamii bali waliendelea kuishi kwenye jamii zao wakijibu maswali ya watu na kuwatatulia matatizo yao mbalimbali. Mitume na mawasii hao waliendelea kuhudumia jamii zao hadi mitume wengine walipoteuliwa na kuchukua nafasi zao baada ya watangulizi wao kuaga dunia. Hali iliendela kuwa hivyo hadi ulipotimia wakati wa Mtume wetu wa mwisho Muhammad (saw). Uislamu haikuwa dini ya kwanza na wala Mtume Muhammad hakuwa Mtume wa kwanza kutumwa kwa wanadamu. Mwenyezi Mungu alimtaka mtukufu huyo awabainishie wazi hilo waja wake kwa kumwambia awaambie kama tunavyosoma katika Aya ya 9 ya Surat al-Ahqaaf: "Mimi si kiroja miongoni mwa Mitume…." Yaani sema: Mimi sihitilafiani na Mitume wengine katika mienendo, kauli wala matendo……

Inasemekana kwamba maana ya kauli hiyo ni kwamba Mtume alitakiwa awaambie wafuasi na watu aliotumwa kuwaangoza kwamba yeye hakuwa mtume wa kwanza kutumwa kwa wanadamu hadi adai kitu ambacho hawakukidai wao.

Miongoni mwa taratibu na tamaduni zilizofuatwa na Mitume na Manabii ni kuusia viongozi wa kidini ambao wangechukua nafasi zao baada ya wao kuondoka duniani na hili ni jambo ambalo Mtume wetu Mtukufu Muhammad al-Mustafa (saw) alilifanya hadharani na mara kadhaa katika maisha yake ambapo alimchagua Ali bin Abi Talib (as) kuwa kiongozi wa Umma wa Kiislamu baada yake na tukio mashuhuri zaidi kuhusiana na suala hilo lilitimia huko Ghadir Khum.

*********

Nam, ndugu wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Katika tukio hilo, Mtume (saw) alianza kwa kumuarifisha Imam Ali kama kiongozi ambaye angechukua nafasi yake baada ya kuondoka yeye duniani na kisha baada ya hapo akawaarifisha na kutaja katika nyakati na matukio tofauti majina ya viongozi wengine ambao wangekuja baada yake tokea Imam Hassan hadi Imam wa mwisho ambaye ni al-Mahdi (af). Suala hilo limefafanuliwa na kuelelezewa kwa marefu na mapana na wanahistoria mashuhuri wa ulimwengu wa Kiislamu wakiwemo al-Kanji as-Shafi' katika kitabu cha Kifayat at-Talib, al-Qanduzi al-Hanafi katika Yanabiul Mawadda, al-Hamuwaini al-Juwayni as-Shafi' katika Faraid as-Simtain, al-Khawarazmi al-Hanafi katika Maqtal al-Hussein (as) na wengine wengi katika ulimwengu wa Ahlu Sunna.

Baadhi ya maulama wa Kishia ambao wameelezea suala hilo kwa kina ni pamoja na Sheikh as-Swadouq katika kitabu cha Ikmaal as-Deen wa Itmaam an-Ni'ma, al-Khazzar al-Qumi katika Kifayat al-Athar na wengine wengi. Sehemu ya Aya ya 7 ya Surat ar-Raad inaashiria ukweli huo kwa kusema: Hakika wewe ni Mwonyaji, na kila kaumu ina wa kuwaongoza. Na marejeo mengi ya historia yanasema kuwa baada ya kuteremka Aya hiyo takatifu, Mtume Mtukufu (saw) alisikika mara nyingi akisema kuwa aliyekusudiwa kwenye Aya hiyo ni Imam Ali (as). Alikuwa akisema: "Wewe ndiye kiongozi - Eeh Ali - kupitia kwako wataongoka wa kuongoka baada yangu." Pia amenukuliwa akisema: "Mimi ndiye mwonyaji." Kisha akauweka mkono wake kwenye bega la Ali (as) na kumwambia: "Wewe ndiye kiongozi ambaye kupitia kwako wataongoka waongokaji baada yangu..." Hivi ndivyo alivyoandika as-Suyuti katika kitabu chake cha ad-Durr am-Manthur, as-Shablanji as-Shafi' katika Nur al-Abswar, Fakhr ar-Razi katika Tafsir al-Kabir, Tabari katika Jamiul Bayaan, al-Muttaqi al-Hindi katika Kanzul Ummal na wengine wengi.

Mbali na hayo, Aya hii wasikilizaji wapenzi ina maana nyingine ambapo inasema: Na kila kaumu ina wa kuwaongoza, kwa maana kuwa katika kila zama ni lazima kuwepo na Imam anayepasa kuwaongoza watu wake. Ni kutokana na ukweli huo ndipo Imam Baqir (as) akasema kama ilivyoandikwa katika kitabu cha Ikmal ad-Deen kwamba: "Kila Imamu huongoza kaumu yake katika zama zake." Kadhalika Imam (as) amenukuliwa akisema katika kitabu cha al-Kafi cha Kulaini kwamba: "Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) ndiye mwonyaji na kila zama ina mwongozaji anayetokana nasi ambaye huwaongoza katika yale aliyokujanayo Mtume (saw). Na viongozi hao baada yake (Mtume) ni Ali na kisha kufuatwa na Mawasii mmoja baada ya mwingine."

Abu Baswir anasema: "Nilimuuliza Imam Swadiq (as): Je, nini maana ya Aya inayosema: Hakika wewe ni Mwonyaji, na kila kaumu ina wa kuwaongoza? Akajibu: Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) ndiye mwonyoji na Ali (as) ni mwongozi (kiongozi). Eeh Abu Muhammad! Niambie, je, kungali kuna kiongozi katika zama hizi? Nikajibu: Niwe fidia kwako, ndio!  Daima kati yenu Ahlul Bayt, kuna kiongozi na nuru ambayo imekuwa ikiangaza hadi kukifikia wewe (Imam Swadiq (as)). Imam (as) akasema: Ewe Abu Muhammad! Mwenyezi Mungu akurehemu! Kama ingekuwa kwamba Aya ingekuwa inakufa na kila mtu aliyeteremshiwa aya hiyo basi Kitabu cha Mwenyezi Mungu (Qur'ani Tukufu) pia kingekuwa kimeshakufa (kingetoweka miongoni mwa watu). Lakini kinyume na hivyo, Kitabu hicho kingali kipo hai na kitaendelea kuwepo miongoni mwa waliopo hai hivi sasa kama kilivyokuwa miongoni mwa waliotangulia."

Hivyo ndugu wasikilizaji, Uimamu umeendelea kuthibiti na kuwepo hata baada ya kuaga dunia Imam Ali (as) kupitia kizazi chake kitukufu, yaani Imamain al-Hassan na al-Hussein na Maimamu wengine tisa watoharifu baada ya Hussein (as). Katika mahojiano yaliyonukuliwa na Sheikh Mufid katika kitabu chake cha al-Ikhtisaas inasemekana kuwa Mtume Mtukufu (saw) alimwambia Myahudi mmoja aliyekuwa akijadiliana naye: "Nakuapiza kwa Mwenyezi Mungu! Je, utanikubali iwapo nitakwambia (ulilouliza)? Myahudi akajibu: Ndio ewe Muhammad!

Mtume (saw) akasema: "Hakika cha kwanza kuandikwa kwenye Torati ni: Muhammad ni Mtume wa Mwenyezi Mungu, nayo yameandikwa kwa lugha ya Kiibrania." Kisha akasoma Aya (ya 157, Surat al-A'raaf) inayosema: Ambaye wanamkuta ameandikwa kwao katika Taurati na Injili… na nyingine ya 6 katika Surat as-Swaff inayosema: ….na mwenye kubashiria kuja Mtume atakayekuja baada yangu; jina lake ni Ahmad!

Kitu cha pili: Ni kwamba jina la Wasii wangu ni Ali bin Abi Talib. Cha tatu na cha nne: Wajukuu wangu ni Hassan na Hussein na cha tano ni kwamba mama yao ni Fatwimah ambaye ni Bibi wa wanawake wa ulimwenguni. Na katika Torati kuna jina la Wasii wangu Ilyaa na majina ya wajukuu zangu Shabbar na Shabir, nao ni nuru ya Fatwimah."

Siku moja Abu Huraira alimuuliza Mtume (saw) maana ya kauli ya Mwenyezi Mungu katika Aya ya 28 ya Surat az-Zukhruf inayosema: Na akalifanya hili liwe neno lenye kubaki katika vizazi vyake ili warejee, naye akamjibu kwa kusema: "Mwenyezi Mungu alijaalia Uimamu katika kizazi cha Hussein ambapo watatokana naye Maimamu wengine tisa, akiwemo Mahdi wa Umma huu."

Na kufikia hapa wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, ndio tunafikia mwisho wa kipindi chetu hiki cha Sibtain katika Qur'ani na Hadithi kwa juma hili. Basi hadi tutakapojaaliwa kukutana tena katika kipindi kingine juma lijalo panapo majaaliwa, tunakuageni nyote kwa kusema, Wassalaama Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh.