Aug 07, 2022 02:23 UTC
  • Jumapili, Agosti 7, 2022

Leo ni Tarehe 9 Mfunguo Nne Muharram 1444 Hijria inayosadifiana na tarehe 7 Agosti mwaka 2022 Milaadia.

Leo kwa mujibu wa kalenda ya Hijria, ni siku ya Tasua yaani tarehe tisa Mfunguo Nne Muharram. Katika siku kama hii mwaka 61 Hijria wakati majeshi ya Yazid yalikuwa yamejiandaa kikamilifu kumshambulia Imam Hussein AS na masahaba zake katika ardhi ya Karbala, Imam alimtuma ndugu yake aliyesifika kwa ushujaa mkubwa yaani Abul Fadhl Abbas akawaombe maadui hao wampe fursa aupitishe usiku huo, kwa Swala na kunong'ona na Mola wake. Usiku huo Imam Hussein aliwakusanya wafuasi wake na baada ya kumhimidi Mwenyezi Mungu na kumsalia Mtume, aliwaambia: ''Kila anayetaka, aitumie fursa iliyobakia ya giza la usiku kwa ajili ya kuyanusuru maisha yake, kwani hakuna atakayebaki hai hapo kesho tutakapokabiliana na jeshi la Yazid.'' Hata hivyo masahaba na wafuasi waaminifu na waumini wa kweli wa mtukufu huyo walikuwa wameshakata shauri la kujitolea mhanga kwa ajili ya Mwenyezi Mungu hadi tone la mwisho la damu zao. Usiku huo wa kuamkia Ashuraa yaani tarehe 10 Muharram, uwanja wa Karbala ulikuwa medani ya ibada kwa mashujaa ambao licha ya kuwa wachache kwa idadi lakini walisimama imara kama mlima na hawakumuacha Imam na kiongozi wao hata dakika moja.

Siku kama ya leo miaka 62 iliyopita sawa na Agosti 7 1960 nchi ya Ivory Coast ilifanikiwa kujipatia uhuru kutoka kwa mkoloni Mfaransa. Wareno waliidhibiti nchi hiyo iliyoko magharibi mwa Afrika katika karne ya 16, lakini ulipofika mwaka 1891 Ufaransa iliidhibiti nchi hiyo, licha ya upinzani mkubwa wa wananchi wa Ivory Coast. Hatimaye ulipofika mwaka 1960, Ivory Coast ikiwa pamoja na nchi nyingine kadhaa za Kiafrika zilizokoloniwa na Mfaransa zilijipatia uhuru wao.

Bendera ya Ivory Coast

Siku kama ya leo miaka 40 iliyopita mwafaka na tarehe 7 Agosti 1982, yalitiwa saini makubalino ya kuondoka vikosi vya Harakati ya Ukombozi ya Palestina (PLO) mjini Beirut Lebanon kati ya Marekani, Lebanon na PLO. Makubaliano hayo yalitiwa saini kufuatia shambulio kubwa lililofanywa na jeshi la utawala wa Kizayuni wa Israel nchini Lebanon mwezi Juni 1982 kwa shabaha ya kuwafukuza wapiganaji wa PLO nchini Lebanon. Ijapokuwa kuondoka wanamgambo wa PLO nchini Lebanon kulitoa pigo kubwa kwa harakati hiyo, lakini miaka ya baadaye Wazayuni maghasibu walikabiliwa na kipigo kikali kutoka kwa wanamapambano wa harakati ya muqawama ya Lebanon, na kulazimika kuondoka kwa madhila katika ardhi ya nchi hiyo mwaka 2000.

Yasser Arafat

Siku kama ya leo miaka 14 iliyopita vikosi vya jeshi la Georgia vikisaidiwa na serikali ya Marekani vililishambulia eneo linalopigania kujitenga la Ossetia ya Kusini huko kaskazini mwa nchi hiyo. Mamia ya raia wasio na hatia wala ulinzi waliuawa na kujeruhiwa kwenye mashambulio hayo. Siku moja baadaye, wanajeshi wa Russia waliingilia kati na kuamua kuwaunga mkono wapiganaji wanaopigania kujitenga wa Ossetia ya Kusini na kulilazimisha jeshi la Georgia kurudi nyuma. Vikosi vya jeshi la Russia vilifanikiwa kuiteka bandari muhimu ya Patumi na kusonga mbele karibu na Tiblis mji mkuu wa nchi hiyo. Jeshi la Russia liliondoka huko Georgia Agosti 12 kwa upatanishi wa Rais wa Ufaransa, na Moscow ikayatambua rasmi kuwa huru maeneo mawili yaliyokuwa yakipigania kujitenga yaani Ossetia ya Kusini na Abkhazia.

 

Tags