Aug 10, 2022 21:57 UTC
  • Akhamisi tarehe 11 Agosti 2022

Leo ni Alkhamisi tarehe 13 Mfunguo Nne Muharram 1444 Hijria sawa na Agosti 11 mwaka 2022.

Tarehe 13 Muharram mwaka wa 61 Hijria yaani siku kama hii ya leo miaka 1383 iliyopita Abdullah bin Afif aliuawa shahidi na gavana wa Yazid bin Muawiya, Ubaidullah bin Ziad. Afif alikuwa mtu wa kwanza kuanzisha malalamiko na upinzani wa waziwazi dhidi ya jinai za Ubaidullah bin Ziad za kumuua shahidi mjukuu wa Mtume (saw), Imam Hussein (as). Baada ya Ubaidullah bin Ziyad kuwashambulia kwa maneno makali na kuwavunjia heshima mateka wa Karbala waliokuwa wamepelekwa katika majlisi yake, Abdullah bin Afif ambaye alikuwa miongoni mwa wachamungu wakubwa wa mji wa Kufa huko Iraq na wafuasi wa kweli wa Amirul Muuminin Ali bin Abi Twalib (as), alikerwa mno na mwenendo huo wa gavana wa Yazidi wa kuwavunjia heshima Watu wa Nyumba ya Mtume (saw) na kumjibu mtawala huyo kwa hasira. Ubaidullah ambaye hakutarajia kuona majibu kama hayo baada ya kuua watu wa Nyumba ya Mtume (saw) alitoa amri ya kukamatwa Afif na kupelekwa kwake. Hata hivyo watu wa kabila lake walizuia kitendo hicho. Askari wa utawala wa Bani Umayyah walivamia nyumba ya Abudullah bin Afifi usiku na kumtoa nje kisha wakamuua shahidi kwa kumkata kwa mapanga. 

Tarehe 11 Oktoba miaka 493 iliyopita Martin Luther alitangaza rasmi madhehebu ya Protestant. Uprotestanti ulianzishwa na Martin Luther kama harakati ya kidini katika karne ya 16 kwenye ulimwengu wa Kikristo kwa lengo la kufanya mageuzi ya kidini. Harakati hiyo ilianza dhidi ya kanisa Katoliki na udikteta wa viongozi wa madhehebu hiyo kuhusu suala la msamaha wa dhambi unaotolewa makasisi na Papa. Martin Luther aliyekuwa Mjerumani alianza harakati hiyo ya uasi ndani ya kanisa Katoliki baada ya kufasiri Injili kwa lugha ya Kijerumani tofauti kabisa na amri ya Papa kwa lengo la kuvunjilia mbali taasubu za kimadhehebu za Kikatoliki.

Martin Luther

Siku kama ya leo miaka 70 iliyopita Haile Selassie, aliyekuwa mfalme wa Ethiopia alitia saini azimio la Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lililokuwa na lengo la kuiunganisha Eritrea na Ethiopia. Ardhi ya Waislamu ya Eritrea ambayo hapo kabla ilikuwa ikikoloniwa na Italia, katika Vita vya Pili vya Dunia ilikaliwa kwa mabavu na Uingereza. Mwezi Disemba 1950 Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa liliidhinisha Eritrea kuongozwa kwa mfumo wa shirikisho sambamba na kuunganishwa na Ethiopia. Hata hivyo kutokana na kwamba wananchi wengi wa Eritrea hawakuridhishwa na hatua hiyo pamoja na kupuuzwa haki zao na utawala wa Ethiopia, walizidisha upinzani dhidi ya utawala wa Addis Ababa na hatimaye kuanzisha harakati ya kupigania uhuru wa nchi yao mnamo mwaka 1960. Mwaka 1993 mapambano ya wananchi wa Eritrea yalizaa matunda ambapo walishiriki katika kura ya maoni na kupiga kura ya kujitenga na Ethiopia.

Haile Selassie

Na siku kama ya leo miaka 62 iliyopita nchi ya Chad ilipata uhuru kutoka kwa mkoloni Mfaransa na siku hii hutambuliwa kama siku ya kitaifa nchini humo. Mwishoni mwa karne ya 19 na mwanzoni mwa karne ya 20 wakoloni wa Ufaransa waliishambulia Chad na katika kipindi cha miaka mitatu wakaidhiiti ardhi yote ya nchi hiyo. Mwaka 1958 Ufaransa iliipa Chad hiari ya kujiongoza na miaka miwili baadaye na katika siku kama ya leo nchi hiyo ikapata uhuru kamili na kuchagua mfumo wa uongozi wa jamhuri. Nchi ya Chad inapakana na nchi za Libya, Cameroon, Sudan, Afrika ya Kati, Nigeria na Niger.

Bendera ya Chad