Ijumaa, Agosti 12, 2022
Leo ni Ijumaa mwezi 14 Mfunguo Nne Muharram mwaka 1444 Hijria sawa na Agosti 12 mwaka 2022 Hijria.
Siku kama ya leo miaka 181 iliyopita, alifariki dunia mjini Isfahan, moja ya miji maarufu ya Iran, Sayyid Sadruddin Musawi Amili, msomi na mtaalamu wa hadithi wa Kiislamu. Sayyid Sadrud-Din Musawi Amili alizaliwa katika moja ya viunga vya mji wa Jabal Amel, nchini Lebanon. Akiwa kijana mdogo alisafiri nchini Iraq ambapo baada ya kuhitimu masomo yake ya awali katika hawza ya elimu ya mjini Najaf, alianza kufanya utafiti katika elimu kadhaa kama vile fiqhi, usulu fiqhi na hadithi na kufikia daraja la juu katika uwanja huo. Sayyid Sadrud-Din Musawi Amili ameandika vitabu mbalimbali katika uga wa elimu ya sheria, nahawu na mifano ya aya za Qur’ani Tukufu.
Siku kama ya leo miaka 120 iliyopita, alifariki dunia Sayyid Abul Qasim Lahore. Abul Qasim bin Hussein bin Naqi Ridhawi Taqawi Lahore aliyekuwa faqihi na mfasiri wa Qur'an Tukufu alizaliwa huko Kashmir. Sayyid Abul Qasim Lahore alikuwa miongoni mwa maulama wakubwa nchini India na ameandika vitabu vingi katika taaluma mbalimbali. Msomi huyo alizikwa Lahore. Miongoni mwa vitabu vyake ni pamoja na 'Burhanu Shaqqul-Qamar wa Raddun-Nayril-Akbar' 'na al Swiraatul-Mustaqim.'
Tarehe 12 Agosti mwaka 1949 hati ya makubaliano ya kimataifa ya kuwalinda majeruhi na mateka wa kivita ilipasishwa kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa huko Geneva, Uswisi. Hati hiyo ilibuniwa kufuatia miamala isiyo ya kibinadamu na jinai zilizokuwa zikifanywa dhidi ya majeruhi na mateka wa kivita wakati wa Vita vya Pili vya Dunia. Kwa mujibu wa makubaliano hayo, nchi zenye mateka zilitakiwa kuwasilisha orodha ya majina ya mateka kwa Shirika la Msalaba Mwekundu Duniani. Hata hivyo licha kuweko makubaliano hayo, lakini madola mengi duniani yamekuwa yakipuuza na kutojali haki za mateka na majeruhi wa kivita.
Siku kama hii ya leo miaka 46 iliyopita sawa na tarehe 12 Agosti 1976, kambi ya wakimbizi wa Palestina ya Tel al Zaatar iliyoko karibu na Beirut mji mkuu wa Lebanon, ilitekwa baada ya kuzingirwa kwa muda mrefu na wanamgambo wa Kimaroni wa nchi hiyo na wakazi wake wakauawa kwa umati. Kambi hiyo ilikuwa ikiwahifadhi maelfu ya wakimbizi wa Palestina na ilianza kuzingirwa mwanzoni mwa mwaka 1976 kwa uungaji mkono na uingiliaji wa utawala wa Kizayuni wa Israel. Utawala wa Kizayuni ulifanya hivyo kwa lengo la kushadidisha vita vya ndani huko Lebanon.
Na miaka 23 iliyopita, Umoja wa Mataifa uliitangaza Agosti 12 kila mwaka, kuwa ‘Siku ya Vijana Duniani’ ili kueleza umuhimu wa vijana katika dunia ya sasa. Tabaka hili lenye utanashati la jamii ndiyo sababu ya maendeleo ya kila nchi kwa msingi huo vijana katika kila nchi wanapaswa kupewa umuhimu mkubwa. Kutokana na umuhimu wao vijana wanapaswa kulindwa na kusaidiwa na serikali hususan katika masuala ya ajira, makazi na kujenga familia. Katika upande mwingine kizazi cha leo cha vijana kinakabiliwa na changamoto nyingi za kimwili na kiroho ikiwa ni pamoja na ongezeko la matumizi ya dawa za kulevya, magonjwa ya kuambukiza kama Ukimwi na virusi vya HIV, intaneti na michezo ya computa ambayo inawatumbukzia vijana wengi katika ufuska na utovu wa maadili. Kutangazwa Siku ya Vijana Duniani kunaweza kusaidia juhudi za kuwakumbusha vijana umuhimu wao na kuzuia changamoto mbalimbali zinazolikabili tabaka hilo muhimu.