Jumamosi, Agosti 13, 2022
Leo ni Jumamosi mwezi 15 Mfunguo Nne Muharram mwaka 1444 Hijria sawa na Agosti 13 mwaka 2022 Milaadia.
Siku kama ya leo miaka 1091 iliyopita, yaani tarehe 15 Muharram mwaka 353 Hijiria, alifariki dunia Ibn Sakan mwanazuoni na mpokezi mashuhuri wa hadithi wa karne ya nne Hijiria. Ibn Sakan alizaliwa mwaka 294 Hijiria huko mjini Baghdad, Iraq ambapo alisafiri katika nchi mbalimbali kwa ajili ya kutafuta elimu. Ibn Sakan alikusanya hadithi nyingi katika miji ya nchi kama Uzbekistan, Tajikistan, Kazakhstan Kyrgyzstan (Transoxiana), Khorasan, Iraq, Sham na Misri na mwishowe akaweka makazi yake nchini Misri. Mpokezi huyo wa hadithi ameacha athari nyingi na mojawapo ni kitabu cha historia kinachohusu maswahaba wa Mtume SAW, kinachoitwa Al Huruf fi Al -Swahaba.
Katika siku kama ya leo, miaka 855 iliyopita, sawa na tarehe 15 Muharram mwaka 589, alizaliwa Ali bin Mussa bin Ja'far maarufu kwa jina la Ibn Twaus, faqihi, mpokezi wa hadithi na mwanazuoni mashuhuri wa Kiislamu katika eneo la Hillah nchini Iraq. Ibn Twaus alipitisha kipindi cha utotoni katika mji huo na baadaye alihamia mjini Baghdad ambako aliishi kwa kipindi cha karibu miaka 15. Ibn Twaus alipata umashuhuri mkubwa katika elimu na ucha-Mungu na ameandika vitabu vingi ambavyo ni marejeo ya taaluma za Kiislamu. Kitabu mashuhuri zaidi cha msomi huyo ni "al Luhuuf" ambacho ndani yake alizungumzia kwa namna bora zaidi matukio ya Siku ya Ashura na harakati ya Imam Hussein bin Ali bin Abi Twalib (as) katika medani ya vita vya Karbala. Kitabu kingine mashuhuri cha mwanazuoni huyo ni "Al Iqbal". Ibni Twaus alifariki dunia mwaka 664 Hijria, akiwa na umri wa miaka 75.
Siku kama ya leo miaka 159 iliyopita aliaga dunia Frederick Eugene Delacroix, mchoraji maarufu wa Ufaransa. Eugene Delacroix alirithi kipaji cha sanaa ya uchoraji kutoka kwa mama yake. Baada ya kupoteza wazazi wake wawili akiwa kijana mdogo na kujikuta akiishi maisha magumu sana ya umasikini, aliamua kufanya juhudi kubwa katika kujiendeleza na fani yake uchoraji. Baadaye alianza kufanya maonyesho ya sanaa hiyo katika ukumbi wa jiji la Paris. Katika kipindi hicho baadhi ya watu walikuwa wakimfanyia maskhara na kumkebehi, hata hivyo hakuvunjika moyo na hatimaye kazi zake zilikuwa na taathira. Alipata umashuhuri katika kipindi kifupi na kazi zake zikapokewa sana katika jamii.
Siku kama ya leo miaka 123 iliyopita, yaani tarehe 13 Agosti mwaka 1899 iliyopita, alizaliwa Alfred Hitchcock mtengeneza filamu mashuhuri wa Kiingereza. Alionesha kazi yake ya kwanza mwaka 1920 na baadaye akaanza kujihusisha na uongozaji filamu. Filamu zake za kuogopesha na za kusisimua zilikuwa mashuhuri mno katika zama hizo. Filamu hizo zilimfanya awe mashuhuri kwa jina la the Master of Suspense. Miongoni mwa filamu zake ni The Man Who Knew Too Much na Young and Innocent. Alfred Hitchcock aliaga dunia tarehe 28 Aprili 1980.
Siku kama ya leo miaka 112 iliyopita, aliaga dunia Florence Nightingale, mwanzilishi wa uuguzi wa kisasa huko nchini Italia, akiwa na umri wa miaka 90. Nightingale alizaliwa tarehe 12 Mei 1820 nchini Italia. Aliishi kipindi kirefu cha ujana wake nchini Uingereza. Akiwa kijana alifanya juhudi kubwa katika kuwasaidia watu, suala ambalo alilipa umuhimu mkubwa kuliko kitu kingine chochote na hatimaye alisabilia maisha yake kwa amjili ya kuuguza wagonjwa. Bi, Florence Nightingale alikuwa muuguzi na mwanahesabati mashuhuri wa Uingereza. Alipewa lakabu ya ''Mwanamke Mwenye Taa Mkononi' kutokana na uvumilivu wake mkubwa na kujinyima usingizi kwa ajili ya kuwahudumia wagonjwa nyakati za usiku. Alifanya juhudi kubwa pia kwa ajili ya kuboresha huduma za afya katika hospitali nyingi nchini Uingereza. Kazi hiyo aliyoifanya kwa miaka mingi bila kuchoka ilimdhoofisha sana kimwili kwa kadiri kwamba alikuwa kipofu mwishoni mwa umri wake na hatimaye aliaga dunia tarehe 13 Agosti 1910 Milaadia.
Siku kama ya leo miaka 62 iliyopita, Jamhuri ya Afrika ya Kati ilijikomboa na kupata uhuru kutoka kwa mkoloni Mfaransa. Ilikuwa katikati ya karne ya 19 wakati nchi hiyo iliyokuwa ikijulikana hapo kabla kwa jina la Ubangi-Shari, ilipounganishwa na makoloni ya Ufaransa barani Afrika. Hata hivyo mwaka 1958, Jamhuri ya Afrika ya Kati ilijipatia mamlaka ya ndani na miaka miwili baadaye yaani mwaka 1960, ikajikomboa na kupata uhuru kamili.