Mchango wa Maulamaa wa Kishia Katika Uislamu (47)
Assalaamu alaykum wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili ya Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran popote pale mlipo.
Nina furaha kukukaribisheni tena katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Mchango wa Maulamaa wa Kishia Katika Uislamu ili kwa pamoja tuweze kufungua ukurasa mwingine katika kurasa za historia ya Maulamaa na wanazuoni wa Kishia pamoja na mchango wao katika Uislamu bila kusahau athari na vitabu vyao mashuhuri. Kipindi chetu kiliicxhotangulia kilimzungumzia Sheikh Jafar Kashif al-Ghitaa. Tulisema kuwa, Kashif al-Ghitaa alizaliwa mwaka 1154 Hijria katika mji mtakatifu wa Najaf. Nasaba yake inarejea na kufika kwa Malik al-Ashtar swahaba na kamanda shujaa na mwenye nguvu wa jeshi la Imam Ali bin Abi Twalib (as). Sheikh Jafar Kashif al-Ghitaa ameandika na kualifu vitabu vingi katika nyuga mbalimbali za kidini kama Fikihi na Usul. Kipindi chetu cha leo ambacho ni sehemu ya 47 kitamzungumzia Mirza Abul-Qassim Gilani mashuhuri kwa jina la Mirza Qumi.
Katika maktaba ya kulea watu katika Uislamu, Maulamaa wa dini wana daraja ya juu ambapo baada ya Mitume na Maimamu (as) hakuna mtu anayefikia daraja yao. Tunapotupia jicho Qur’ani na hadithi mbalimbali tunaona ni kwa namna gani daraja ya wanazuoni na Maulamaa ilivyokuwa ya juu ambapo tunaona katika baadhi ya hadithi wanaelezwa kuwa ni warithi wa Mitume. Hata hivyo sifa hii inawahusu wale wanazuoni na Maulamaa ambao wameifanya elimu yao kwa ajili ya kumhudumia Mwenyezi Mungu na kuwaongoza wanadamu kuelekea katika saada ya milele.
Katika zama zake, Mirza Qumi alikuwa mmoja wa wanazuoni wasomi zaidi katika ulimwengu wa Kishia ambapo nadharia zake za kidini na mtindo wake wa kielimu kwa miaka mingi viliendelea kutawala katika vyuo vikuu vya kidini katika miji ya Isfahan, Najaf, Mash’had na Tehran. Mirza Abul-Qassim Gilani mashuhuri kwa lakabu ya Mirza Qumi ndiye mwandishi wa kitabu mashuhuri cha Qawanin al-Usul ambapo kwa miaka na miaka kilikuwa miongoni mwa mitaala ya masomo katika vyuo vya kidini vya Waislamu wa madhehebu ya Shia.
Mirza Abul Qassim alizaliwa mwaka 1151 Hijria katika moja ya vijiji vya mkoa wa Lorestan Iran. Hata hivyo aliondokea kuwa mashuhuri kwa lakabu ya Mirza Qumi kutokana na kuwa alifanikiwa kupata daraja ya Ijtihadi akiwa katika mji wa Qum na mji huo ulikuwa chimbuko la harakati zake za kielimu na kijamii. Baba yake ni Akhund Mulla Muhammad Hassan ambaye asili yake ni mji wa Gilan Iran. Mzazi wake huyo akiwa katika rika la ujana aliondoka Gilan na kuelekea Isfahan kwa ajili ya kwenda kutafuta elimu na baada ya kumaliza masomo yake aliuchagua mji wa Lorestan kuwa makazi yake.
Mirza Abul-Qassim alisoma masomo ya msingi kwa baba yake na baadaye alielekea Khansar na kusoma kwa Sayyid Hussein Khansari aliyekuwa mmoja wa Maulamaa mahiri na watajika katika zama hizo katika taaluma ya Fikihi na Usul na kufanikiwa kufikia daraja za juu katika uga huo.
Mwaka 1174 Mirza Abul-Qassim alielekea katika mji wa Karbala kwa ajili ya kujiendeleza zaidi kielimu na kulichagua eneo la jirani na Haram ya Imam Hussein (as) mjini humo kuwa makazi yake. Katika kipindi hicho, Mirza Abul-Qasim alihudhuria darsa na masomo ya Ayatullah Wahid Bahbahani mwanafakihi mtajika na aliyekuwa mwalimu mahiri katika zama hizo katika vyuo vya kidini vya Karbala na Najaf. Baadaye alirejea Iran na kuuchagua mji wa Qum kuwa makazi yake.
Mirza Abul-Qassim alikuwa mtu mwenye hima na juhudi kubwa katika kutafuta elimu na alitambulika kama mtu mwenye azma na irada thabiti katika uwanja huo. Alikuwa na ratiba ya kila lahadha ya maisha yake na hakuwa tayari kughafilika na na kuacha kufanya juhudi katika kujifunza na kutafuta elimu.
Alimu na msomi huyu alianza kuandika vitabu akiwa katika rika la ujana. Ana vitabu vyenye thamani kubwa katika akthari ya elimu za Kiislamu kama Fikihi na Usul, teolojia na kadhalika. Hata hivyo kitabu chake mashuhuri ni Qawanin al-Usul.
Mirza Abul-Qassim aliishi katika zama za wafalme wa Qajar nchini Iran Agha Muhammad Khan na Fat-h Ali Shah. Moja ya sifa na tabia mashuhuri ya Mirza Abul-Qassim ni kuzingatia sana suala la kutoa nasaha, kutoa miongozo na kuamrisha mema na kukataza mabaya. Mwanazuoni huyo ana barua mbili mashuhuri alizowaandikia watawala wa wakati huo wa Iran ambazo zimejaa nasaha ndani yake.
Barua ya kwanza aliiandika akiwa na umri wa miaka 50 na alimuandikia Agha Muhammad Khan Qajar na ya pili aliiandika akiwa na umri wa miaka 80 na aliamuandikia mfalme wa wakati huo wa Iran Fat'h Ali Shah Qajar. Barua mbili hizo zimeondokea kuwa mashuhuri kwa jina la Barua ya Muongozo ya Mirza Qumi na zimechapishwa kwa jina hilo hilo.
Kama tulivyoashiria, barua yake ya kwanza kama zinavyoonyesha nyaraka za historia aliiandika akimhutubu Agha Muhammad Khan Qajar mfalme wa kwanza na muasisi wa ukoo wa Qajar. Muhammad Khan Qajar alikuwa mtawala mwenye roho ngumu na licha ya kuwa na mapenzi na shauku kubwa na masuala ya kidini, lakini hakuwa na malezi sahihi ya kidini kutokana na upotofu wa kiitikadi na alikuwa akijiona kwamba, anaweza kufanya baadhi ya mambo ya kidhalimu.
Mwanzoni mwa barua yake, Mirza Abul-Qassim au Mirza Qumi akiwa na lengo la kuandaa mazingira ya kumuathiri mfalme kama huyo aliandika: Barua hii siyo ya nasaha kutoka kwa mjuzi kwenda kwa mtu mjinga, na wala siyo ya kumuongoza mtu anayetangatanga baada ya kupotea, bali ni ya mdahalo na mashauriano ya watu wawili wasomi na wenye ujuzi. Kwa kutumia maneno na lugha hii, alimu huyu akawa ameondoa kabisa hali ya mfalme huyo kusimama kidete na kutokubali kusikiliza nasaha.
Baada ya kuandika utangulizi huo, Mirza Qumi anabainisha kwa ushujaa mkubwa nukta muhimu sana lengo likiwa ni kuondoa upotofu wa kifikra wa mfalme, upotofu ambao ulikuweko katika fikra za mtawala huyo na kumruhusu kufanya dhulma na uonevu.
Barua ya pili ya Mirza Qumi aliiandika akimhutubu Fat'h Ali Shah Qajar. Katika zama hizo Masufi walikuwa wakifanya juhudi kubwa kwa ajili ya kupenya ndani ya utawala na walikuwa wakitaka kumfanya mfalme awe miongoni mwao. Mmoja wa malenga na washairi mashuhuri wa Kisufi alimuandikia ujumbe Mfalme Fat'h Ali Shah ili amvute katika pote la Usufi. Fat'h Ali Shah aliamua kumuandikia barua Mirza Qumi na kwa kuwa alikuwa akimtambua kama msomi na mwanazuoni mahiri na mchaji Mungu. Katika ujumbe huo alimtaka ambainishie lililo sahihi na lisilo sahihi katika ujumbe huo wa Masufi. Licha ya kuwa, katika zama hizo, Mirza Qumi alikuwa mzee na dhaifu kimwili, lakini kutokana na umuhimu ya jambo hilo, alijibu kwa umakini mkubwa takwa la mfalme katika fremu ya barua ambayo ndio ile barua ya pili inayojulikana kama Barua ya Muongozo.
Hatimaye Mirza Qumi aliaga dunia mwaka 1231 Hijria akiwa na umri wa miaka 80. Mazishi ya msomi huyo yalihudhuriwa na umati mkubwa wa watu na kuzikwa katika mji wa Qum jirani na haram ya Bibi Fatma Maasuma (as).
Mpenzii msikilizaji, muda wa kipindi chetu kwa leo umefikia tamati usisite kujiunga nami wiki ijayo.
Wassalaam Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh