Mchango wa Maulamaa wa Kishia Katika Uislamu (49)
Ni matumaini yangu kuwa, hamjambo wapenzi wasikilizaji popote pale mlipo.
Karibuni kujiunga nami tena katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Mchango wa Maulamaa wa Kishia Katika Uislamu ili kwa pamoja tuweze kufungua ukurasa mwingine katika kurasa za historia ya Maulamaa na wanazuoni wa Kishia pamoja na mchango wao katika Uislamu bila kusahau athari na vitabu vyao mashuhuri. Kipindi chetu kiliichotangulia kilimzungumzia Sayyid Ali Tabatabai, mashuhuri kwa lakabu ya Swahib Riyadh.
Tulibainisha kwamba, Sayyid Ali Tabatabai alianza kusoma masomo ya dini mwanzoni mwa ujana wake na katika kipindi cha muda mfupi tu alidhihirisha kipaji kikubwa alichokuwa nacho. Miongoni mwa vitabu vyake mashuhuri ni "Riyadh al-Masail Fi Bayan al-Ahkam Bidalail" (ریاض المسائل فی بیان الاحکام بالدلائل) ambacho kinajulikana zaidi kwa jina la Riyadh al-Masail. Sehemu ya 49 ya kipindi hiki juma hili itatupia jicho maisha ya Sayyid Muhammad Tabatabai mmoja wa Marjaa watajika. Kuweni nami hadi mwisho ya kipindi.
Sayyid Muhammad Tabatabai anayejulikana pia kama Ayatullah Mujahid alizaliwa 1180 Hijria katika mji wa Karbala, Iraq. Baba yake ni Sayyid Ali Tababai tuliyemzunguzia katika kipindi chetu kilichopita na ambaye ni mashuhuri kwa lakabu ya Swahib Riyadh, mmoja wa mafakihi na marajii wa Mashia wa daraja ya juu. Mama yake ni mjukuu wa Allama Wahid Bahbahani. Sayyid Muhammad alizaliwa katika kipindi ambacho mji wa Karbala ulikuwa umegeuka na kuwa kituo cha elimu na fikihi katika ulimwengu wa Kishia. Hiyo ilitokana na juhudi kubwa zilizofanywa na Allama Bahbahani. Katika mazingira hayo, Sayyid Muhammad alianza kusoma masomo ya awali na ya msingi kwa baba yake. Licha ya kuwa Sayyid Muhammad hakupata tawfiki ya kuhudhuria darsa na masomo yaliyokuwa yakitolewa na babu yake yaani Allama Bahbahani, lakini alifanikiwa kuhudhuria na kusoma kwa wanafunzi mahiri na hodari wa babu yake huyo.
Mbali na kusoma kwa baba yake, Sayyid Muhammad alihudhuria pia darsa za Allama Bahr al-Ulum mjini Najaf na mbali na masomo aliweza kunufaika na fadhila nyingi kama za uchajimungu, zuhdi na kuipa mgongo dunia, kama ambavyo alimuoa binti wa Allama Bahr al-Ulum. Aidha akiwa mjini Najaf msomi huyo aliweza kuhudhuria masomo ya fakihi na mwanazuoni mahiri na mwenye uwezo mkubwa kielimu yaani Sheikh Jafar Kashif al-Ghitaa.
Sheikh Jaafar Kashif al-Ghitaa alikuwa amebobea na kutabahari mno katika elimu za Fikihi na Usuli. Mbali na kuwa kiongozi wa kidini alikuwa akihesabiwa pia kuwa shujaa wa kitaifa aliyekuwa mstari wa mbele. Kudiriki zama ilikuwa moja ya sifa stahiki za Kashif al-Ghitaa. Sayyid Muhammad Tabatabai hakujifunza elimu ya fikihi tu kwa walimu wake, bali alijifunza pia mambo mengine mengi kama kuhisi kuwa na masuulia na majukumu mkabala na masuala mbalimbali ya kijamii pamoja na ushujaa na ujasiri katika mambo.
Kutokana na hima na idili kubwa aliyokuwa nayo Sayyid Muhammad Mujahid katika kujifunza elimu zikiwemo elimu za Usuli na fikihi, aliweza kwa haraka mno kukwea daraja za kielimu, kiasi kwamba, baba yake alimtaja kama ni msomi kuliko yeye na kwamba, ni msomi zaidi yake na hivyo akachukua uamuzi wa kutotoa tena fatuwa.
Baina ya Maulamaa wa Kishia ni ada na imezoeleka kwamba, kwa kuweko alimu msomi zaidi mahali fulani wasomi wengi haijuzu kwao kutoa fatuwa. Ni kutokana na sababu hiyo ndio maana Muhammad kwa heshima ya baba yake aliamua kuondoka Karbala na kuhajiri kuelekea Isfahan.
Alikaa Isfahan kwa muda wa miaka takribani 10. Katika zama hizo, mji wa Isafahan ulikuwa kituo na kitovu muhimu kwa ajili ya elimu za dini. Katika kipindi hicho, wanazuoni na Maulamaa wengi walikuwa wakihudhuria darsa na masomo yake na walikuwa wakimtambua kama mwalimu mahiri na hodari katika Vyuo vya Dini vya Karbala na Isfahan.
Baada ya kuaga dunia baba yake, Sayyid Muhammad Tabatabai aliondoka Isfahan na kurejea Karbala na kuchukua jukumu la Marjaa na kiongozi wa Mashia.
Baada ya hujuma ya kinyama ya kundi potovu la Mawahabi dhidi ya mji wa Karbala na kuuawa kwa umati maelfu kadhaa ya watu pamoja na Maulamaa wa mji huo, Sayyid Muhammad alihajiri na kuelekea katika mji wa Kadhimein na kujishughulisha na kufundisha jirani na Haram za Maimamu wawili Imam Hadi na Askary (as) sambamba na kuongoza jamii ya Mashia.
Zama za Umarjaa wa Ayatullah Sayyid Muhammad Tabatabai zilisadifiana na kipindi cha kuanza duru ya pili ya vita vya Iran na Russia na Maulamaa chini ya uongozi wake walikuwa na nafasi na mchango mkubwa na athirifu. Ni kutokana na sababu hiyo ndio maana akaondokea kuwa mashuhuri pia kwa lakabu ya Ayatullah Mujahid.
Sehemu ya utawala wa kifalme wa Fat'h-Ali Shah Qajar ambayo ilisadifiana na maisha ya Ayatullah Mujahid ni moja ya nyakati nyeti na zilizokuwa na mgogoro zaidi katika historia ya Iran na ulimwenguu kwa ujumla.
Katika zama hizo kulikuwa kumeanza ushindani mkali baina ya madola yenye nguvu duniani kwa ajili ya kuwa na udhibiti wa maeneo ya Asia na Afrika na hivyo kuyakoloni. Iran kutokana na nafasi yake muhimu ya kijiografia ilikuwa na umuhimu maalumu kwa wakoloni.
Katika zama hizo, Kamanda wa jeshi la Iran alikuwa Abbas Mirza. Tofauti na mfalme, Kamanda Abbas Mirza alikuwa na hamu ya kusimama kidete mbele ya uvamizi wa Russia na ili aweze kumkinaisha Fat'h-Ali Shah Qajar naye asimame kidete, aliomba msaada kutoka kwa Marajii wa wakati huo akiwemo Ayatullah Tabatabai.
Katika kipindi hicho, baadhi ya Maulamaa wa Iraq na Iran akiwemo Sayyid Muhammad Tabatabai walitoa jibu mwafaka kwa ombi hilo ambapo waliandika risala za kijihadi na kuwashajiisha watu wajitokeze kwa ajili ya kupigana vita na vikosi vya Russia. Jambo hilo lilileta uhai mpya kwa nguvu za kijeshi za Iran. Katika zama hizo, matumaini ya watu walikuwa wameyaelekeza kwa Marajii wa Kidini na Vyuo Vikuu vya Kidini (Hawza). Ndio maana katika mazingira kama haya, Ayatullah Mujahid na Maulamaa wengine walikuwa na habari kuhusiana na matukio yanayojiri na wote walikuwa wakikubaliana juu ya kutoa fatuwa dhidi ya Russia. Ayatullah Mujahid alimtumia barua Fat'h-Ali Shah mtawala wa wakati huo wa Iran na kumtaka azuie dhulma na hujuma ya jeshi la Russia.
Baada ya kutoa fatuwa ya jihadi, Ayatullah Mujahid akiwa pamoja na baaadhi ya Maulamaa na wanafunzi wa masomo ya dini (matalaba) alihajiri na kuja Iran na akiwa Tehran alitoa mwaliko kwa Maulamaa. Kufuatia mwaliko huo, Maulamaa wakakusanyika katika mji wa Tehran na kuafikiana kuhusiana na vita dhidi ya Russia.
Uwepo wa viongozi wa kidini kwa uongozi wa Ayatullah Mujahidi ulipelekea kujitokeza harakati ya wananchi nchini Iran na hivyo kupatikana nguvu kubwa kutoka katika kila kona ya Iran.
Kipindi fulani Sayyid Muhammad Mujahid aliishi katika mji wa Tabriz na kutokana na masaibu na mashaka aliyoyapata kufuatia vita alipata maradhi makali na akalazimika kuondoka katika mji huo. Mwanazuoni huyo aliaga dunia tarehe 13 Jamad al-Thani 1242 katika mji wa Qazvin kutokana na maradhi yaliyokuwa yakimsumbua. Mwili wa alimu na msomi huyo mtajika ukasafirishwa na kwenda kuzikwa katika mji wa Karbala.
Wapenzi wasikilizaji muda wa kipindi chetu kwa leo umefikia tamati, msisite kujiunga nami tena juma lijalo katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Mchango wa Maulamaa wa Kishia Katika Uislamu. Hadi tutakapokutana tena siku na saa kama ya leo, ninakuageni nikikutakieni kila la kheri.
Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh