Mchango wa Maulamaa wa Kishia Katika Uislamu (51)
Assalaamu alaykum wapenzi wasikilizaji popote pale yanapokufikieni matangazo haya ya Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran
Karibuni kujiunga nami tena katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Mchango wa Maulamaa wa Kishia Katika Uislamu. Kipindi chetu kilichopita kilimzungumzia Sayyid Abdallah Shubbar mmoja wa Maulamaa mahiri wa Kishia aliyeishi katika karne ya 13 Hijria.
Tulisema kuwa, Sayyid Abdallahh Shubbar alizaliwa mwaka 1188 Hijria katika mji wa Najaf Iraq. Baba yake yaani Sayyid Muhammad Ridha alikuwa miongoni mwa wasomi, Maulamaa na wachamungu watajika mjini Najaf ambapo watu walimpa lakabu ya "Swahib al-Da'wat al-Mustajabah" kwa maana ya mtu ambaye dua yake ilikubaliwa. Kipindi chetu cha leo ambacho ni sehemu ya 51 ya mfululizo huu kitaangazia maisha ya msomi na alimu mwingine wa Kishia yaani Mulla Ahmad Naraqi mashuhuri zaidi kwa jina la Fadhil Naraqi. Kuweni nami hadi mwisho wa kipindi.
Mulla Ahmad alizaliwa mwaka 1185 Hijria huko Naraq moja ya viunga vya mji wa kihistoria wa Kashan nchini Iran. Baba yake ambaye ni Mulla Mahdi Naraqi alikuwa mashuhuri kwa lakabu ya Muhaqqiq Naraqi na alikuwa mwanahisabati mahiri na mwanafalsafa mweledi. Mulla Ahmad Naraqi alikuwa mahiri mno katika elimu za nujumu, fikihi, usuli, hadithi, Ilmur Rijal, fasihi na mashairi. Aidha alizingatia mno uhakiki na uvumbuzi wa wasomi wa Magharibi. Alianza kusoma kwa baba yake akiwa na umri mdogo na kunufaika mno na masomo ya mzazi wake huyo. Alipofikisha umri wa miaka 20, Ahmad Naraqi alihajiri pamoja na familia yake na kuelekea katika mji mtakatifu wa Najaf ambapo lengo la kugura huko lilikuwa ni kutafuta elimu. Akiwa mjini Najaf alihudhuria darsa na masomo ya Alllama Bahbahani. Baada ya kuaga dunia Allama Wahid Bahbahani, Ahmad Naraqi alifunga safari na kurejea katika eneo alilozaliwa.
Baada ya miaka minne kupita tangu kuaga dunia mwalimu wake, Ahmad Naraqi alimpoteza baba yake pia aliyefariki dunia mwaka 1209 Hijria na hivyo kukosa neema ya kuwa pamoja na baba. Kumpoteza baba yake ambaye alikuwa amemsogeza mwanawe hatua kwa hatua katika elimu ya akhlaq lilikuwa pigo kubwa mno kwa Ahmad Naraqi. Kwa mara nyingine tena alifunga safari na kuelekea Najaf na kuhudhuria masomo ya walimu watajika na mashuhuri katika zama hizo kama Allama Bahr al-Ulum na Allama Kashif al-Ghitaa, ambao tumezungumzia kwa mapana na marefu historia na maisha yao katika vipindi vyetu vilivyotangulia. Katika kipindi hicho Ahmad Naraqi alifanikiwa kufikia daraja za juu kielimu na kuwa na nadharia katika elimu kama fikihi, usuli, teolojia, akhlaq, mashairi, irfani, falsafa, mantiki, jiometri na kadhalika.
Baada ya kukamilisha masomo yake alirejea mahali alipozaliwa. Aliuchagua mji wa kihistoria wa Kashan kuwa makazi yake na kwa kuwa alikuwa na nafasi mwafaka ya kielimu na mafanikio mazuri baina ya wananchi, alifikia daraja ya Umarjaa na kama alivyokuwa baba yake, naye akachukua jukumu la uongozi wa kidini na kisiasa wa watu katika zama hizo.
Daima Mulla Ahmad Naraqi alikuwa akifikiria ustawi na maendeleo ya watu wastadhaafu na wanyonge na alijitokeza katika nyakati tofauti kwa ajili ya kuwatetea watu madhulumu. Ahmad Naraqi alikuwa na mapenzi maalumu baina ya watu. Licha ya kuwa watawala pia walikuwa wakimpa heshima maalumu, lakini katu hakunyamazia kimya dhulma ya vyombo vya utawala.
Imekuja katika vitabu vya historia kwamba, watawala waliokuwa wakipelekwa Kashan baada ya kuteuliwa na mtawala wa wakati huo wa Iran Fat’h-Ali Shah Qajar walikuwa wakiamiliana kidhulma na kimabavu na watu. Ni kutokana na sababu hiyo, ndio maana Ahmad Naraqi alikuwa akijitokeza na kusimama kidete dhidi yao na hata mara kadhaa alimtimua na kumfukuza kutoka katika mji wa Kashan mtawala aliyekuwa ametumwa na Mfalme Fat’h Ali Shah.
Kusimama kidete huku kwa Ahmad Naraqi mbele ya dhulma na kuwatimua watawala waliokuwa wameteuliwa na Mfalme kwenda kutawala katika mji wa Kashan, kulimkasirisha sana Fat’h Ali Shah. Kwa muktadha huo, alimu huyo aliitwa na mfalme katika mji mkuu Tehran ambapo mfalme alimhutubu kwa lugha kali na yenye ghadhabu akimtuhumu kwamba, anakwamisha masuala ya utawala na uongozi.
Ahmad Naraqi ambaye alishuhudia kung’ang’ania mfalme msimamo wake wa kidhulma alikunja mikono ya nguo yake na kunyoosha mikono mbinguni na kumwambia Mwenyezi Mungu: Ewe Mwenyezi Mungu, mtawala huyo dhalimu umemuweka atawale watu, na mimi nimefanya juhudi za kuondoa dhulma hii, lakini dhalimu huyu amenikasirikia.

Kwa hakika Mulla Ahmad alitaka kumuombea laana mfalme huyo. Mfalme ambaye alikuwa akifahamu vyema nguvu ya imani, na imani thabiti ya mwanazuoni huyu mkubwa wa Kishia, aliingiwa na hofu na woga! Aliamka kutoka katika kiti chake cha ufalme na kuelekea upande wa Ahmad Naraqi. Akiwa na hali ya woga na kuchanganyikiwa aliishika mikono ya Mulla Ahmad na akamsihi na kumtafadhalisha asimuombee laana kwa Allah. Baada ya hapo kukafanyika mashariano na baada ya Mulla Ahmad kuafiki akatumwa katika mji wa Kashan mtawala mstahiki.
Wapenzi wasikilizaji kupitia tukio hilo la kihistoria tunaweza kufahamu jinsi Mulla Ahmad alivyokuwa na ushawishi na nguvu miongoni mwa watu na kwamba, Fat’h Ali Shah licha ya kiburi na jeuri yote aliyokuwa nayo alikuwa akikiri wazi daraja ya kimaanawi ya Mulla Ahmad na alikuwa akimuamini na ndio maana alimuomba na kumtafadhalisha kwamba asimuombee laana.
Moja ya uga ambao Fadhil Naraqi amefanya uhakiki na utafiti ni masuala yanayohusiana na mafunzo na malezi. Msomi huyu ana nadharia na mitazamo muhimu na mizuri katika uwanja huu ambapo wahakiki waliokuja baadaye yake walimsifu na kumthamini mno kutokana na nadharia hizi. Kwa mtazamo wa alimu huyu, mafunzo na malezi yana umuhimu maalumu katika maisha ya watu na msingi wake muhimu zaidi ni kuitukuza nafsi. Kama tutataka kubainisha kwa maneno mepesi maana ya izza na utukufu wa nafsi tunapaswa kusema kuwa, ni mtu kujiheshimu na kujithamini yeye mwenyewe. Kama mtu atakuwa na mtazamo huu ndani ya nafsi yake ataratibu na kuvifanya vitendo vyake viendane na utambuzi huu na hivyo hatokuwa tayari kufanya mambo machafu na yasiyofaa.
Ahmad Naraqi ambaye ni mmoja wa walimu wa Sheikh Murtadha Ansari msomi mwingine mahiri wa Kishia, kama walivyokuwa wanazuoni wengine, naye hakuwa nyuma pia katika uandishi wa vitabu. Ameandika vitabu takribani 30 katika uga wa mashairi, fikihi, usul fikih, akhlaq na hisabati. Hata hivyo kitabu chake mashuhuri zaidi ni Miiraj al-Saadah ambacho kinazungumzia masuala ya akhlaq. Walengwa wa kitabu hiki ni watu wa kawaida pia na siyo Maulamaa na wahakiki tu.
Wapenzi wasikilizaji muda wa kipindi chetu kwa leo umefikia tamati, tukutane tena katika kipindi kijacho ambacho tutaendelea kumzungumzia alimu na msomi huyu.
Hadi tutakapokutana tena wakati huo, ninakuageni nikikutakieni kila la kheri maishani. Wassalaam alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.