Aug 31, 2022 02:19 UTC
  • Jumatano, 31 Agosti, 2022

Leo ni Jumatano Mwezi 3 Mfunguo Tano Safar, 1444 Hijria, sawa na tarehe 31 Agosti, 2022 Miladia

Miaka 1387 iliyopita katika siku kama ya leo, yaani Mwezi 3 Safar mwaka 57 Hijria Qamaria, kwa mujibu wa baadhi ya mapokezi ya historia, alizaliwa katika mji wa Madina, Imam Muhammad Baqir (AS), mjukuu kipenzi wa Bwana Mtume SAW na Imamu wa Tano wa Waislamu wa madhehebu ya Shia. 

Ukamilifu wa kimaanawi na kielimu ambayo ni hidaya ya Mwenyezi Mungu waliyotunukiwa Ahlubayti wa Mtume SAW, ulidhihirika kwa uwazi katika shakhsia ya Imam Muhammad Baqir (AS) pia. Katika kipindi cha miaka 19 ya Uimamu wa mtukufu huyo, ambacho kilisadifiana na miaka ya mwishoni ya utawala wa Bani Umayyah, yalipatikana mazingira mwafaka katika jamii kwa yeye kuweza kuimarisha misingi ya kifikra na kiutamaduni ya Waislamu. Fani nyingi za elimu zilistawishwa na kuenea katika jamii ya Waislamu kupitia chuo cha fikra cha mtukufu huyo pamoja na mwanawe, yaani Imam Jaafar Sadiq (AS); na hata wanafunzi wake walikuja kuwa wavumbuzi wa fani mbalimbali mpya za elimu.

Lakini sambamba na hayo, Imam Baqir hakughafilika pia na kupambana na dhulma na uonevu wa utawala wa kijabari wa Bani Umayyah na ndiyo maana katika mwaka 114 Hijria Qamaria aliuliwa shahidi na mtawala wa zama hizo. Tunachukua fursa hii pia kukupeni mkono wa heri na baraka kwa mnasaba wa kuadhimisha kuzaliwa kwa mjukuu huyo kipenzi wa Mtume SAW.

Miaka 201 iliyopita katika siku kama hii, yaani tarehe 31 Agosti 1821, alizaliwa mwanafizikia na tabibu  mashuhuri Hermann Ludwig Ferdinand von Helmholtz katika mji wa Potsdam nchini Ujerumani. Msomi huyo alihitimu masomo yake katika fani ya utabibu na mnamo mwaka 1849 alifikia daraja ya uprofesa wa fiziolojia na fizikia katika vyuo vikuu vya Berlin na Heidelberg. Japokuwa Helmholtz alitambulika zaidi kama mwanafizikia, mwanabiolojia na tabibu, lakini alikuwa mtaalamu wa hisabati na falsafa pia. Mwanafizikia huyo alitoa mchango mkubwa sana katika fani za electrodynamics na chemical thermodynamics. Katika uga wa falsafa, Herman Ludwig Ferdinand Von Helmholtz ndiye mwasisi wa falsafa ya sayansi, ambayo ni tawi la falsafa linalohusika na misingi, njia na matumizi ya sayansi. Msomi huyo alifariki dunia mwaka 1894 akiwa na umri wa miaka 73. 

Hermann Ludwig Ferdinand von Helmholtz

Siku kama ya leo miaka 75 iliyopita yaani mwezi Tatu Safar mwaka 1369 Hijria Qamaria aliaga dunia alimu na mwalimu mkubwa wa akhlaqi Mirza Muhammad Ali Shah Abadi. Mirza Muhammad Ali Shah Abadi alisoma elimu za msingi kwa baba yake, ambaye yeye mwenyewe alikuwa mmoja wa mafakihi na wanafunzi wa Sahib Jawahir. Baadaye aliendeleza masomo yake ya dini kwa kaka yake Sheikh Ahmad Beid Abadi na kwa Mirza Muhammad Hashim Khonsari. Ili kukwea daraja za juu zaidi za elimu, alimu huyo mkubwa wa akhlaqi alielekea Daarul-Ilm ya Najaful-Ashraf, kisha baadaye akaelekea Samarra ambako alikuwa akihudhuria darsa za Ayatullah Mirza Muhammad Taqi Shirazi. Baada ya hapo akarejea Iran, ambapo kwanza makazi yake yalikuwa Tehran na kisha baada ya miaka michache akaelekea Qum. Imam Khomeini (MA) alikuwa mmoja wa wanafunzi wakubwa wa Ayatullah Shah Abadi. Mwalimu huyo mkubwa wa Irfani na Akhlaqi ameacha athari nyingi kikiwemo kitabu cha Manaazilu-Saalikin, Risala ya Akili na Ujinga na Nyongeza ya Kifaayatul-Usul. Alipomzungumzia mwalimu wake huyo, Imam Khomeini alisema: "Katika maisha yangu sikuwahi kuona roho nyofu kama ya Ayatullah Shah Abadi"

Mirza Muhammad Ali Shah Abadi 

Miaka 65 iliyopita, yaani tarehe 31 Agosti 1957 nchi ya Malaysia iliyoko mashariki ya bara la Asia ilipata uhuru wake kutoka kwa Uingereza. Watu wa Malaysia walianza kidogo kidogo kuingia katika Uislamu katika karne ya 13 Miladia. Ushawishi wa Wazungu kutoka Ulaya katika nchi hiyo ulianza mwanzoni mwa karne ya 16 alipowasili nchini humo baharia wa Kireno Afonso de Albuquerque. Mnamo karne ya 17 Uholanzi iliikalia na kuitawala Malaysia; na ulipofika mwaka 1824 na kufuatia mkataba wa makubaliano yaliyofikiwa baina ya Uingereza na Uholanzi, Malaysia ikatawaliwa na Uingereza na Indonesia ikakabidhiwa Uholanzi. Uingereza iliendelea kuitawala Malaysia hadi ilipopata uhuru wake katika siku kama ya leo.

Bendera ya Malaysia

 

Miaka 44 iliyopita katika siku kama hii ya leo, yaani tarehe 31 Agosti 1978, Imamu Musa Sadr alitoweka katika mazingira ya kutatanisha alipokuwa safarini nchini Libya. Imamu Musa Sadr alizaliwa tarehe 4 Juni mwaka 1928 katika mji wa Qum nchini Iran. Baada ya kumaliza masomo, mwaka 1959 alielekea Lebanon. Wakati huo, Waislamu wa nchi hiyo walikuwa na hali mbaya sana kijamii, kisiasa na kiuchumi. Kutokana na hali hiyo, Imamu Musa Sadr alichukua hatua kadhaa za msingi ili kuboresha hali zao na ndipo alipobuni taasisi ya kushughulikia masuala ya Waislamu wa Kishia iitwayo "Baraza Kuu la Mashia wa Lebanon". Taasisi hiyo ilipitishwa katika bunge la nchi hiyo na yeye akachaguliwa kuwa mkuu wake. Imamu Musa Sadr alikuwa pia akiunga mkono kikamilifu mapambano ya Wapalestina dhidi ya utawala haramu wa Kizayuni wa Israel; na kwa ajili hiyo akaanzisha "Harakatul-Mahrumin" ambayo ililenga kutetea haki za Waislamu wa Lebanon pia. Tangu Imamu Musa Sadr alipotoweka, zimefanyika jitihada nyingi na kubwa za kupata taarifa kuhusu hatima yake, lakini hadi sasa hazijazaa matunda.

Imamu Musa Sadr

 

Tags