Sep 23, 2022 02:45 UTC
  • Ijumaa tarehe 23 Septemba 2022

Leo ni Ijumaa tarehe 26 Safar 1444 Hijria imayosadifiana na tarehe 23 Septemba 2022.

Miaka 347 iliyopita katika siku kama ya leo, Valentin Conrart mwandishi na mwanafasihi wa Kifaransa aliaga dunia akiwa na umri wa miaka 72. Alizaliwa mwaka 1603 katika familia iliyokuwa na mapenzi makubwa na fasihi ya lugha na kwa msingi huo ndio maana alipokuwa katika rika la ujana, Valentin Conrart akawa na mapenzi na taaluma ya fasihi ya lugha na taratibu akaanza kujihusisha na fani ya uandishi.

Valentin Conrart

Katika siku kama ya leo miaka 120 iliyopita sawa na tarehe Mosi Mehr 1281 Hijria Shamsia, alizaliwa Ayatullahil Udhmaa Sayyid Ruhullah al Musawi Khomeini, mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Baba yake Imam Khomeini ambaye alikuwa miongoni mwa wanazuoni wa Kiislamu, aliuawa shahidi Imam akiwa bado mtoto na hivyo akalelewa na mama na shangazi yake. Baada ya kukamilisha masomo ya msingi, Ruhullah Khomeini alijiunga na masomo ya juu kwa walimu mashuhuri hususan Ayatullah Abdul Karim Hairi na Muhammad Ali Shahabadi. Imam Khomeini alianzisha harakati kubwa ya kupambana na utawala wa kidhalimu wa Shah baada ya kufariki dunia Ayatullah Borujerdi. Upinzani na mapambano yake yalimfanya mtawala kibaraka, Shah ampeleke uhamishoni katika nchi za Uturuki, Iraq na Ufaransa. Imam aliendeleza mapambano yake dhidi ya Shah akiwa uhamishoni alikobakia kwa kipindi cha miaka 15 na baadaye alirejea nchini na kuuondoa madarakani utawala wa kifalme wa Shah na kuasisi Jamhuri ya Kiislamu ya Iran hapo mwaka 1979.

Imam Khomeini

Siku kama ya leo miaka 90 iliyopita sawa na Septemba 23 mwaka 1932, Saudi Arabia iliasisiwa, na Abdulaziz bin Saud akawa mfalme wa nchi hiyo. Bara Arabu au Hijaz ni mahali alipotokea Mtume wa Uislamu Muhammad S.A.W. Saudi Arabia ilijitoa chini ya udhibiti wa utawala wa Abassiya mwanzoni mwa karne ya tatu Hijria na hadi karne kadhaa badaye, nchi hiyo iliendelea kuwa na ukosefu wa amani. Jitihada za al Saud za kutaka kuiongoza Saudia zilianza katikati mwa karne ya 18 na kushika kasi zaidi mwanzoni mwa karne ya 20. 

Bendera ya Saudi Arabia

Siku kama ya leo miaka 83 iliyopita, aliaga dunia Sigmund Freud daktari wa magonjwa ya akili raia wa Austria. Sigmund alizaliwa mwaka 1856. Daktari huyo alifanya utafiti na kuchunguza matatizo mbalimbali ya kiakili yanayomkumba binadamu na kutoa maoni na nadharia mpya kuhusu chanzo cha magonjwa ya akili. Kwa sababu hiyo anahesabiwa kuwa mwasisi wa elimu ya uchunguzi wa kisaikolojia au Psychoanalysis.

Sigmund Freud