Jumanne tarehe 4 Oktoba 2022
Leo ni Jumanne tarehe 7 Rabiul Awwal 1444 Hijria sawa na tarehe 4 Oktoba 2022.
Katika siku kama ya leo miaka 1102 iliyopita Ali bin Muhammad Tanukhi alimu, mwandishi na malenga mashuhuri wa karne ya nne Hijria aliaga dunia huko katika mji wa Basra, kusini mwa Iraq akiwa na umri wa miaka 64. Ali Tanukhi alizaliwa huko Antakia mashariki mwa Uturuki ya leo na akiwa kijana alielekea Baghdad na kuasisi makazi yake. Ali bin Muhammad Tanukhi alikuwa mahiri katika lugha na fasihi ya Kiarabu na kuwa miongoni mwa malenga mashuhuri wa zama hizo. Mbali na kutunga diwani yake ya mashairi ambayo imebaki kama kumbukumbu hadi hii leo, Tanukhi aliandika pia vitabu mbalimbali kimojawapo kikiwa ni kile alichokipa jina la al Arudh.

Siku kama ya leo miaka 192 iliyopita, Ubelgiji ilijitangazia uhuru. Mwanzoni mwa karne ya 18 Ubelgiji ilikuwa chini ya udhibiti wa Austria, huku ikidhibitiwa na Ufaransa mwishoni mwa karne hiyo hiyo. Hata hivyo baada ya Napoleon Bonaparte kushindwa na madola ya Ulaya, mwaka 1815 Ubelgiji na Uholanzi ziliunda muungano. Hata hivyo muungano huo haukudumu kwa muda mrefu kufuatia Wabelgiji wa Kikatoliki kuanzisha uasi dhidi ya Waholanzi wa Kiprotestanti na hivyo kuamua kujitangazia uhuru wao katika siku kama ya leo.
Katika siku kama ya leo miaka 94 iliyopita tabibu Alexander Fleming alivumbua dawa ya penicillin. Fleming ambaye alikuwa daktari maarufu nchini Uingereza, alizaliwa tarehe Sita Agosti mwaka 1881 katika familia ya wakulima mjini Lochfield farm, magharibi mwa Scotland. Fleming alivumbua dawa hiyo baada ya kuona kuwa askari wengi walikuwa wakipoteza maisha kutokana na kukumbwa na bakteria wa maambukizi kwenye majeraha, suala ambalo lilimtia wasi wasi mkubwa. Miaka 10 baada ya kumalizika vita, sawa na tarehe Nne Oktoba mwaka 1928 Miladia, Fleming alifanikiwa kuvumbua dawa ya penicillin, ambayo huua vijidudu vya maambukizi kwenye kidonda.
Siku kama ya leo miaka 65 iliyopita satalaiti ya kwanza ilirushwa angani na msomi wa Urusi ya zamani na kwa utaratibu huo zama za udhibiti wa anga zikawa zimeanza. Satalaiti hiyo iliyopewa jina la Sputniki 1 ilizunguka dunia mara 1400 kwa siku 92 na kwa mara ya kwanza ikafikisha ujumbe wa radio kutoka angani kuelekea ardhini.
Na siku kama ya leo miaka 44 iliyopita, Serikali ya Kuwait ilimnyima Imam Khomein ruhusa ya kuishi nchini humo na hivyo akulazimika kuelekea nchini Ufaransa. Hatua ya Imam kuelekea Paris, ilikuwa sababu ya kuharakisha mwenendo wa mafanikio ya Mapinduzi nchini Iran, kinyume kabisa na matarajio ya dikteta Saddamwa Iraq na Mohammad Reza Pahlavi, mfalme kibaraka wa wakati huo wa Iran ambao waliamini kwamba kwa kumbaidisha Imam Khomein (MA) wangekuwa wameua harakati zake za kimapinduzi. Akiwa mjini Paris, Imam aliishi katika kijiji kilichoitwa Neauphle-le-Château, kilometa 50 kutoka mji huo, ambapo aliendeleza harakati zake za kimapinduzi kupitia barua na kanda za sauti kwa wanamapinduzi nchini Iran.
