Oct 13, 2022 02:31 UTC
  • Alkhamisi tarehe 13 Oktoba 2022

Leo ni Alkhamisi tarehe 16 Rabiul Awwal 1444 Hijria sawa na tarehe 13 Oktoba 2022.

Siku kama ya leo miaka 1443 iliyopita kwa mujibu wa baadhi ya mapokezi ya historia, Swala ya kwanza ya Ijumaa iliswaliwa na Mtume Muhammad (saw) baada ya mtukufu huyo kuhama mji wa Makka. Baada ya kuwasili katika eneo la Bani Salim bin Auf kwa jina la Quba karibu na Madina wakati wa adhuhuri, Mtume (saw) alitoa hotuba na kusimamisha Swala ya Ijumaa mahala hapo. Wanahistoria wanasema hiyo ilikuwa Swala ya kwanza ya Ijumaa katika Uislamu. Hatua hiyo pia inaonesha umuhimu wa ibada hiyo ya kiroho na kisiasa ambayo Bwana Mtume aliamua kuitekeleza mara tu baada ya kuwasili karibu na mji wa Madina. Baadaye Waislamu walijenga msikiti katika eneo hilo palipofanyika Swala ya Ijumaa ya kwanza katika Uislamu.

Siku kama ya leo miaka 140 iliyopita alifariki dunia mwandishi na mwanafalsafa wa Kifaransa, Joseph Arthur de Gobineau mwanaharakati wa Ufaransa ambaye anajulikana zaidi kwa kusaidia kuhalalisha ubaguzi wa rangi kwa kutumia nadharia ya kisayansi. Gobineau alizaliwa mwaka 1816 huko Paris na baada ya kumaliza masomo yake alijishughulisha na uandishi wa habari. Gobineau aliwahi kuwa katibu na balozi wa Ufaransa nchini Iran na kupata kujifunza lugha za Kifarsi na Kiarabu. Mwandishi huyo wa Kifaransa aliamini kuwa watu weupe hasa wale wenye asili ya Aryan ndio watu bora zaidi na meandika vitabu kadhaa kuhusiana na kutokuwepo usawa kati ya wanadamu. Nadharia ya kuwa kizazi cha Aryan ndicho kizazi bora zaidi kuliko vizazi vingine vya wanadamu ni moja ya sababu zilizompelekea Adolf Hitler kuanzisha Vita vya Pili vya Dunia na kuua kwa umati watu wasiokuwa wa asili ya Aryan.

Siku kama hii ya leo miaka 58 iliyopita bunge la kimaonyesho la Iran lilipasisha sheria iliyowapa washauri wa kijeshi wa Marekani nchini kinga ya kutofikishwa mahakamani iwapo wangepatikana na hatia ya aina yoyote (Capitulation Accord) . Kwa mujibu wa sheria hiyo, wahalifu wa Kimarekani wangehukumiwa nchini kwao kama watatenda jinai nchini Iran, na mahakama za Iran hazikuwa na haki ya kushughulikia kesi zao. 

Sheria hiyo ilitambuliwa kuwa dharau kwa taifa la Iran na iliyokiuka wazi kujitawala kwa nchi. Kwa msingi huo hayati Imam Ruhullah Khomeini (MA) siku kadhaa baada ya kupasishwa sheria hiyo bungeni alitoa hotuba ya kihistoria akieleza taathira zake na kumshambulia vikali Mfalme Shah na Marekani. Baada ya hotuba hiyo Imam Khomeini alikamatwa na kupelekwa uhamishoni.

 

Tags