Jumamosi, 15 Oktoba, 2022
Leo ni Jumamosi tarehe 18 Mfunguo Sita Rabiul Awwal 1444 Hijria sawa na tarehe 15 Oktoba 2022 Miladia.
Siku kama ya leo miaka 1443 iliyopita kulingana na kalenda ya Hijria, ilianza kazi ya ujenzi wa Msikiti wa Mtume mjini Madina ambao ni msikiti wa pili kwa utukufu duniani baada ya Masjidul Haram. Mtume (SAW) alitoa amri ya kujengwa msikiti wa Madina baada tu ya kuhamia mjini humo na yeye mwenyewe alishiriki katika ujenzi wake. Kando kando ya msikiti huo kulijengwa vyumba vya Mtume na baadhi ya maswahaba zake. Mtume hakuutumia msikiti kwa ajili ya ibada tu, bali alitumia pia sehemu hiyo kwa ajili ya masuala kama kutoa hukumu baina ya watu, vikao vya mashauriano, mafunzo ya kivita na utatuzi wa masuala mbalimbali ya Waislamu. ***
Siku kama ya leo miaka 480 iliyopita alizaliwa Abul-Fat'h Jalal al-Din Muhammad Akbar, mfalme aliyekuwa na nguvu kubwa wa silsila ya Teimurian nchini India. Mfalme huyo alikuwa maarufu kwa jina la Akbar Shah na alichukua madaraka akiwa na umri wa miaka 13 baada ya kufariki dunia baba yake, yaani Homayun. Kwa kipindi cha miaka mitano aliongoza nchi akiwa na cheo cha naibu mtawala chini ya usimamizi wa Bairam Khan. Baada ya kushika madaraka kikamilifu alianza kupanua wigo wa utawala wake katika maeneo ya Bengal, Kashmir, Sindh, Punjab, Ahmednagar na Kandahar. Mfalme Abul-Fat'h Jalal al-Din Muhammad Akbar alikomboa kisiwa cha Dakan huko kusini mwa India kutoka mikononi mwa Wareno. Akbar Shah alifariki dunia mwaka 1605. ***
Siku kama ya leo miaka 178 iliyopita alizaliwa mwanafalsafa wa Kijerumani Friedrich Wilhelm Nietzsche. Baada ya kuhitimu masomo, Nietzsche alianza kufunza katika Chuo Kikuu cha Basel. Mwanafalsafa huyo alikuwa akipinga dini na misingi ya kimaadili na katika falsafa na mitazamo yake alikuwa akiamini nadharia ya "Superman", kwa maana ya mtu mwenye uwezo kupita kiasi. Nietzsche alikuwa akiamini kwamba, mtu mwenye uwezo kupita kiasi au Superman ni matokeo ya irada na matashi ya mwanadamu na huwa juu ya mema na mabaya yote. Mwanafalsafa huyo ameandika vitabu kadhaa ikiwa ni pamoja na Beyond Good and Evil, The Birth of Tragedy na Thus Spoke Zarathustra. Katika kipindi cha mwishoni mwa uhai wake Friedrich Wilhelm Nietzsche alipoteza mlingano wa kifikra na alifariki dunia mwaka 1900. ***
Na leo tarehe 15 Oktoba ni Siku ya Vipofu Duniani. Suala la usalama wa vipofu na haki zao za kijamii daima lilikuwa likipewa umuhimu maalumu katika jumuiya za kimataifa na kwa msingi huo mwaka 1950 Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa (UNESCO) na Baraza la Kimataifa la Vipofu zilikutana na kupasisha sheria ya Fimbo Nyeupe na kuitangaza tarehe 15 Oktoba kuwa ni Siku ya Fimbo Nyeupe au Siku ya Kimataifa ya Usalama wa Vipovu. Miongoni mwa vipengee vya sheria hiyo ni pamoja na haki ya vipofu kutumia suhula zote za hali bora ya kimaisha katika jamii, kuwahamasisha watu wa jamii hiyo kushiriki katika masuala ya serikali na kupewa ajira serikalini, kulinda haki za vipofu wakati wa kuvuka barabara na kadhalika. ***