Hakika ya Uwahabi 3
Bismillahir Rahmanir Raheem. Tunamshukuru Mwenyezi Mungu Mtukufu ambaye aliwabainishia wanadamu njia sahihi na ya wazi kuelekea wongofu ambapo baadhi walifuata njia hiyo na wakafaulu na wengine wakakengeuka na kupotea.
Tuliona katika vipindi viwili vilivyopita namna Uingereza ilivyozipatanisha koo mbili za Aal Saud na Mawahabi huko katika Bara Arabu kwa lengo la kuharibu jina la Uislamu na Waislamu ambapo pia tulizungumzia kwa ufupi jinsi utawala wa Othmania ulivyoweza kuutokemeza mara mbili muungano huo wa shari dhidi ya Umma wa Kiislamu. Kuweni nasi hadi mwisho wa kipindi ili tupate kujifunza mengi zaidi kuhusu suala hilo.
Baada ya kutiwa saini mkataba wa urafiki baina ya kasri ya Aal Saudi wakishirikiana na Mawahabi na Uingereza mnamo mwaka 1866, Waislamu ambao walikuwa wamepata pigo kubwa na kudhuriwa na ukoloni wa Uingereza walikasirishwa sana na jambo hilo ambapo utawala wa Othmania ukisaidiwa na ukoo wa ar-Rashid ulifanikiwa kuuangamiza utawala ulioasisiwa na pande mbili za Wasaudi na Mawahabi. Mabaki yao yaani Abdu Rahman na mtoto wake barobaro yaani Abdul Aziz walifanikiwa kukimbilia Kuwait ambayo wakati huo ilikuwa chini ya ukoloni wa Uingereza.
Mwanzoni mwa karne ya 20, Ulaya ilikumbwa na msikusuko mingi sana. Historia ilikuwa inakaribia kusajili vita vikubwa ambavyo vingeikumba dunia nzima. Utawala wa Othmania na nchi za Kiislamu, ikiwemo Iran, hazikuwa na nia ya kuingia katika vita hivyo, lakini Uingereza na washirika wake walikusudia kuzishughulisha nchi zote hizo na vita hivyo. Kwa kutilia maanani kuwa utawala wa Kiislamu wa Othamnia na washirika wake huko Najd, yaani ukoo wa al-Rashid, walikuwa kikwazo kikubwa katika kufikiwa malengo ya ukoloni wa Uingereza katika eneo hilo, Uingereza iliamua kuvua samaki mkubwa kwenye msukosuko na tope la vita hivyo, na bila shaka ikafanikiwa kufikia lengo hilo wakati huo.
Vita vya Kwanza vya Dunia vilidumu kwa miaka minne na moja ya matokeo yake ilikuwa ni kusambaratishwa dola kuu la Othmania. Kwa kufutwa dola la Othmania, utawala wa Kiwahabi wa Saudia haukuwa na adui mwingine mkubwa katika eneo, hivyo Uingereza ikaamua kumuunga mkono haraka Abd al-Aziz wa Kiwahabi. Serikali mpya ya Kiwahabi, ambayo haikuwa tena na haja kubwa ya kupata msaada wa kifedha na silaha kutoka Uingereza, ikawa imeasisiwa na kuwa na uwezo wa kuiteka Riyadh nzima.
Baada ya kutekwa Riyadh, moja ya hatua za kwanza za serikali ya tatu ya Kiwahabi ya Saudia ilikuwa ni kuwatia hofu wananchi kwa kuwakata vichwa viongozi wa serikali iliyokuwa inaelekea kuanguka ya ar-Rashid. Hawakuishia hapo, bali ima walichomo moto au kuwaua kikatili karibu watu 1,200 wakazi wa Riyadh. Kwa vitendo hivyo vya kutisha, Mfalme Abdulaziz wa Kiwahabi alipata umaarufu mkubwa na kupendwa sana na mabwana zake wa Uingereza. Maafisa wengi wa Uingereza katika eneo la Ghuba ya Uajemi mara nyingi walikuwa wakikutana au kutangamana naye, kumpa pesa na silaha na pia kumshauri na kumpendekezea mambo aliyotakiwa kuyafanya katika utawala wake. Ni kutokana na msaada huo ndipo Abdul Aziz aliweza hatua kwa hatua kuteka sehemu kubwa ya Bara Arabu, ambayo leo inajulikana kama "Saudi Arabia".
Ili kuimarisha zaidi utawala wake, Mfalme Abdul Aziz aliwafukuza wajukuu wa Mtume wa Uislamu Muhammad (saw) kutoka ardhi hizo za Bara Arabu au kwa jina jingine Hijaz. Mwaka 1919 alituma jeshi lake katika eneo la Turabah huko huko Hijaz ambapo lilifanya mauaji makubwa ya umati usiku dhidi ya wakazi wanaume zaidi ya elfu sita (6000) katika eneo hilo.
Mwezi Agosti 1924 Mawahabi walishambulia eneo la Taif ambapo waliwakata vichwa wanaume na wavulana wadogo na wakati huo huo kuwabaka bila huruma wanawake na mabinti waliokuwa wakilia na kupiga makelele kwa kushuhudia jamaa zao wakiuawa kwa namna hiyo ya kutisha mbele ya macho yao. Wanawake wengi wa Taif walioshuhudia unyama huo waliamua kujitumbukiza kwenye visima vya maji ili kukwepa kubakwa na makatili hao wa Kiwahabi.
Ukoo wa Wasaudi na Mawahabi, ambao uliona kwamba ulikuwa salama na kutokabiliwa na tishio lolote kutokana na kusambaratishwa utawala wa Othmania ulifanya jinai nyingi za kutisha huko Makka na Madina, miji miwili mitakatifu ya Kiislamu, bandari ya Jeddah na miji mingine mingi ya Hijaz. Waliyavunjia heshima makaburi ya zamani zaidi na kuharibu mengine mengi yenye thamani kubwa za kiutamaduni mjini Makka, misikiti na maeneo mengi ya kihistoria ambayo kwa karne nyingi yaliakisi historia tukufu ya Uislamu katika mji huo mtakatifu na mkongwe. Waliharibu mabaki yoyote ya dhahiri na ya kihistoria ya Mtume Muhammad (saw) kwa kisingizio kwamba yasije yakaabudiwa. Hata walishambulia na kuharibu sehemu kubwa ya haram na kaburi la Mtume Muhammad (saw) kwa silaha za Waingereza. Waliharibu na kuangamiza mabaki ya ustaarabu mkongwe wa Uislamu kwa kisingizio cha kupambana na ushirikina na kujaribu pia kutokomeza ustaarabu mpya wa Waislamu kwa kisingizio kuwa ulikuwa ishara ya Shetani. Walipoingia kwenye bandari ya Jeddah, walianza kuharibu mara moja laini za simu, vituo vya redio na suhula nyinginezo za maisha ya kisasa. Askari wa Kiwahabi walimpiga viboko mtu yeyote aliyeonekana kuwa na vitu kama vile miwani, nguo za Kimagharibi, dhahabu, manukato au hariri.
Baada ya kuasisiwa utawala wa Aal Saud na Mawahabi ambao walikuwa na wangali vibaraka wakubwa wa Uingereza huko Hijaz, Mfalme Abdul Aziz aliamua kuhodhi madaraka ambapo aliharibu magezi yote huru, vyama vya siasa, katiba na vyombo vya dola vilivyokuwa vikitawala katika ardhi ya Hijaz na hatimaye kuamua kubadilisha jina la ardhi hiyo na kuipa jina la ukoo wake yaani Saudi Arabia.
Baada ya kudhibiti ardhi ya Hijaz, ukoo wa Aal Saud alieneza ukatili wake dhidi ya koo nyingine za ardhi hiyo ambapo uliua, kukandamiza, kujeruhi na kukata viungo vya mwili vya koo hizo na hatimaye kupelekea wengi wa watu wa koo hizo kukimbilia usalama wao katika nchi nyingine za dunia na kutorudi tena katika ardhi yao ya asili huko Bara Arabu.
Mfalme Abdul Aziz wa Kiwahabi kutokana na matamanio yake ya kimwili na yasiyo na mpaka alioa wanawake wengi wapatao mia tatu (300) ambapo wengine alikuwa akilala nao usiku mmoja tu na kisha kuwapiga teke. Inasemekana alizaa wavulana 125 lakini hakuna yeyote anayeweza kukisia idadi ya mabinti aliowazaa. Alikuwa na mamia ya watumwa na kwa msingi huo alikuwa akishajiisha utumwa kinyume kabisa na mafundisho ya Uislamu. Mwenendo huo wa utumwa uliendelea katika ukoo wa Aal Saud hadi uliposimamishwa mwaka 1962 kwa kuhofia kufedheheka kimataifa.
Watoto wa Mfalme Abdul Aziz (Saud, Faisal, Khalid na Fahd) walitawala Hijaz kwa zama baada ya kuaga dunia baba yao, ambapo waliendeleza sera ile ile ya kuwategemea Wamagharibi na hasa Waingereza katika kudumisha utawala wao katika ardhi hiyo takatifu.
************
Kutokana na kuwa Marekani iliibuka mshindi wa mwisho katika Vita vya Pili vya Dunia na hivyo kuchukua nafasi ya Uingereza katika udhibiti wa ulimwengu, Saudi Arabia pia ilichukuliwa kuwa mshirika mkubwa zaidi wa Marekani katika Mashariki ya Kati. Kwa hakika nchi hiyo ambayo ina miji mitakatifu zaidi katika ulimwengu wa Kiislamu ilibadilika kuwa koloni jipya la Marekani, nchi ya Magharibi ambayo inahesabiwa kuwa adui mkubwa nambari moja wa Uislam na Waislamu. Katika miongo ya hivi karibuni, utajiri mkubwa wa mafuta wa Saudi Arabia umewapelekea Mawahabi kupuuza wakosoaji wao wengi na kufanya juhudi za kuboresha sura yao mbovu katika ulimwengu wa Kiislamu. Wanajitambulisha kuwa ni “vuguvugu la wanamageuzi” linalotaka kusafisha jina la Uislamu, na hata kuupa “Uwahabi” jina jipya la “Harakati ya Usalafi” (Sunna halisi) ili kufikia lengo hilo. Kwa mtazamo wao mwanzilishi wa Uwahabi, Muhammad bin Abd al-Wahhab, alikuwa mwanazuoni mkubwa wa Kiisllamu ambaye peke yake aliweza kuokoa na kuunusuru Uislamu kutokana na "ushirikina" na imani zisizo na msingi. Ni miaka mingi sasa ambapo Uwahabi uliotajirishwa kwa dola za mafuta, umekuwa ukienezwa kwa mbinu tofauti miongoni mwa Waislamu na nchi za Kiislamu. Mawahabi wanajaribu kuondoa mkosi wa kuwa kwao wachache katika ulimwengu wa Kiislamu na kueneza fikra zao potofu katika nchi za Kiislamu kwa kuanzisha taasisi mbalimbali za hisani na ufadhili au vituo vya kielimu katika nchi hizo.
**************