Jun 25, 2023 07:59 UTC
  • Hakika ya Uwahabi 18

Miaka 13 ilikuwa imepita tangua kushindwa majeshi ya Umoja wa Sovieti nchini Afghanistan na kutokea mashambulio yaliyofanyika dhidi ya majengopacha mawili ya kibiashara mjini New York. Katika kipindi hicho Afghanistan ilikuwa imekumbwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe, vita ambavyo Usama bin Laden na washika wake walikuwa na nafasi muhimu katika kuvidumisha.

Mmoja wa washirika wa Bin Laden lilikuwa kundi la Taliban lililoongozwa na Muhammad Mullah Omar. Mullah Omar alizaliwa na kulelewa katika kijiji kimoja cha Afghanista ambapo alisoma masomo ya msingi ya Uislamu na kisha kuyafundisha katika kijiji hicho hicho akiwa na umri wa miaka 19. Hapo ndipo alianza kufahamika kwa jina la Mullah Omar. Alipoteza moja ya macho yake katika vita na jeshi la Umoja na Sovieti na baadaye kujiunga na madrasa ya Dar al-Ulum Haqqani alipokuwa amesafiri nchini Pakistan kwa ajili ya kutafuta silaha.

Madrasa ya Dar al-Ulum Haqqani nchini Pakistan

Madrasa ya Haqqani ni mojawapo ya madrasa mashuhuri za madhehebu ya Deobandi nchini Pakistan. Madhehebu ya Deobandi inajiona kuwa mmoja wa wafuasi wa Abu Hanifah na katika baadhi ya itikadi inajinasibisha kwa Ibn Taymiyya, kiongozi wa kifikra wa Mawahabi. Madhehebu hiyo inaitwa "Deobandiyya" kwa sababu ilianzishwa na kukua katika mji unaoitwa Deoband ulioko kaskazini mwa India, karibu na mahali alipozaliwa msomi na mwanazuoni mashuhuri anayeitwa Shah Waliyullah Dehlavi, ambaye wafuasi wa madhehebu ya Deobandi wanamwona kuwa kiongozi wao mkuu. Dehlavi alibuni mfumo maalumu wa elimu kwa ajili ya wanafunzi wake, ambao ulienea karibu katika pande zote za India. Fikra yake ilikuwa ya kuleta umoja baina ya Waislamu, tofauti kabisa na alivyokuwa Ibn Abd al-Wahhab ambaye anajichukulia yeye na wafuasia wake kuwa Waislamu wa pekee na wengine wote kuwa makafiri. Ni fikra hiyo ndiyo iliweza kuwawaunganisha Waislamu wa India na kuwawezesha kuishi pamoja kama ndugu katika mji wa Deoband hadi karne moja baadaye, ambapo Waingereza walivamia na kukalia kwa mabavu nchi hiyo.

Dar al-Ulum katika mji wa Deoband nchini India

Shule ya Deoband iliweka suala la maadili ya Kiislamu, upendo na mahaba, thamani za kidini na itikadi za Kiislamu katika muhimili wa shughuli zake za kiutamaduni kama njia bora ya kukabiliana na kujilinda dhidi ya hujuma ya kiutamaduni ya Waingereza. Kwa njia hiyo, wafuasi na wahitimu wa shule hiyo waliweza kukabiliana vilivyo na hujma pamoja na mashinikizo ya Wamagharibi na hivyo kufanikiwa kulinda na kuleta umoja katika jamii ya Waislamu. Ni Waislamu hao hao ndio baadaye walikuwa na mchango mkubwa katika harakati za kupigania uhuru wa India.

Kwa miaka mingi shule za Deoband zilikuwa shule bora zaidi za Kiislamu katika India kubwa lakini baada ya kujitenga Pakistan na nchi hiyo, baadhi ya wafuasi wa kundi hilo walianzisha nchini Pakistan shule zao wenyewe na kujiweka mbali na fikra halisi za Dehlavi. Moja ya shule hizo mpya zilizoanzishwa Pakistan ni shule ya Haqqani ambayo baadaye ilimvutia Mullah Omar wa Afghanistan.

Muhammad Mullah Omar

Itikadi za madhehebu ya Deoband zinatofautiana pakubwa na Mawahabi wa Saudi Arabia ambapo wafuasi wa madhehebi hiyo hawajichukulii kuwa Masalafi wala Mawahabi. Hii ni pamoja na kuwa miaka mingi ya matukio ya kisiasa katika eneo yamekuwa yakiwakutanisha na kuwakurubisha pamoja wafuasi wa pande mbili hizo. Katika miaka ambayo Afghanistan ilikuwa ikipigana vita na Umoja wa Sovieti na baadaye vita vya wenyewe kwa wenyewe, kulikuwepo na ushirikiano mkubwa baina ya shule za Deoband nchini Pakistan na utawala wa Saudi Arabia ambapo Mawahabi walifanikiwa kwa kiwango fulani kupenyeza fikra zao za kuwakufurisha Waislamu katika shule hizo.

Kuongezeka fikra hizo katika shjule za Deoband kuliibua makundi yenye misimamo mikali na ya kupindukia mipaka katika shule hizo kadiri kwamba kulichochea mivutano dhidi ya Mashia, ambapo makundi hayo yaliwakufurisha na kuwajibisha kumwagwa damu yao. Moja ya makundi hayo lilijulikana kwa jina la Sepah Swahaba, ambalo kwa miaka mingi lilihusika na vitendo vingi vya kutisha vya ugaidi nchini Pakistan na Afghanistan na hasa dhidi ya Mashia wa nchi hizo.

Walimu au mashekhe waovu wanaohitimu masomo katika shule hizo za Deoband, huchukulia fikra zao kuwa ndio dini na za Waislamu wengine kuwa bida' na uzushi. Muhammad Mulllah Omar ni mmoja wa mashekhe hao bandia waliohitimu masomo yao katika shule ya Haqqani wakiwa na fikra hizo za mgando na za kigaidi, ambaye baada ya kuhitima masomo huko Pakistan alirejea Afghanistan kwa ajili ya kueneza huko fikra hizo hatari dhidi ya Uislamu. Baada ya kuwasili huko alibeba silaha kwa ajili ya kueneza kile alikiita utekelezaji wa sheria za Kiislamu. Mwanzoni Mullah Omar hakuwa na wafuasi wengi bali walikuwa watu thelathini tu ambao hawakuwa na silaha nyingi. Pamoja na hayo kundi hilo liliungwa mkono kwa hali na mali na vyombo vya ujasusi na usalama vya Pakistan ambapo baadaye liliibuka kuwa kundi lenye nguvu kubwa za kijeshi na kujipa jila la Taliban.

Katika vipindi tofauti, serikali ya Pakistan iliyashawishi makundi ya Sepah Swahaba na mengine yaliyokuwa yamehitimu kutoka katika shule za Deoband kwenda kusaidiana na kundi la Taliban nchini Afghanistan ambapo makundi hayo yalitekeleza mauaji na jinai za kutisha dhidi ya watu wa nchi hiyo. Kwa mfano, katika hujuma ya kigaidi waliyotekeleza katika mji wa Mazar Shariff, walifanya mauaji ya kutisha na kinyama dhidi ya wakazi wa mji huo kadiri kwamba mauaji hayo yalitajwa kuwa ya kimbari. Baadhi ya watu wanaosimulia tulio hilo la kutisha wanasema kwamba miili ya wahanga wa mauaji hayo ilirundikana kwa siku kadhaa katika mitaa na njia za mji huo, na makatili wa Taliban hawakuruhusu miili hiyo iondolewe na hivyo kubakia katika sehemu hizo kwa siku sita.

Katika muda huo wote shujaa wa pekee ambaye alipambana na kusimama imara dhidi ya hujuma hiyo ya Taliban na washirika wao wa kigeni alikuwa Ahmad Shah Masoud. Ni yule yule mwanamapambano shujaa ambaye alifanya bonde la Panj Shir na maeneo mengine ya kaskazini mwa Afghanistan kuwa sehemu isiyofikiwa na jeshi la Umoja wa Sovieti. Mara hii pia aliyadhibiti vizuri maeneo hayo na kuchukuliwa kuwa kimbilio la pekee la kuwalinda watu wa Afghanistan.

Ahmad Shah Masoud

Mwaka 1996 ambapo kundi la Taliban lilikaribia kudhibiti sehemu kubwa ya Afghanistan, Usama bin Laden kiongozi wa kundi la kigaidi la al-Qaida alirejea Afghanistan na kushirikiana kwa karibu na Mullah Omar na wafuasi wake. Kama tulivyoashiria awali Usama bin Laden ni yule yule mtu ambaye alikuwa akiwapa vijana wa Kiarabu silaha za Wamarekani kwa ajili ya kupigana dhidi ya jeshi la Umoja wa Sovieti. Mwanzoni alikuwa kiunganishi wa serikali za Saudi Arabia na Marekani na makundi ya wabeba silaha nchini Afghanistan lakini taratibu akabadilika kuwa kamanda wa makundi yenye silaha ya vijana wa Kiarabu na baadaye kubuni kundi la al-Qaida.

Baada ya kushindwa jeshi la Umoja wa Sovieti, Usama bin Laden alijiona kuwa shujaa na kamanda wa kipekee lakini Marekani na Saudi Arabia hazikumchukulia mtu kama huyo aliye na uchu wa madaraka kuwa kwa maslahi yao. Walimuweka chini ya udhibiti na uchunguzi mkali wa kiusalama jambo lililompelekea Usama bin Laden aamue kuhama Saudia. Alikuwa na marafiki wengi kati ya viongozi wa Taliban hivyo akaamua kurejea Afghanistan ambapo Taliban ilikuwa imechukua udhibiti wa sehemu kubwa ya nchi hiyo na kuendeleza huko shughuli zake za ugaidi. Mullah Omar na Taliban walimkaribisha kama shujaa na licha ya kuwa alikuwa chini ya mashinikizo makubwa ya kimataifa lakini hawakuacha kumuunga mkono na kuendelea kumpa hifadhi aliyohitaji.

Obama na Osama

Mwaka 2001 Milaadia, siku mbili kabla ya kushambuliwa majengopacha ya kibiashara mjini New York. Kundi la Taliban kwa msaada wa taasisi za ujasusi za Pakistan lilikuwa limefanikiwa kuua kigaidi na kumuondoa njiani mwanapambano wa pekee aliyekuwa akilizuia kudhibiti Afghanistan nzima. Lilitekeleza shambulio la kigaidi lililomuua Ahmad Shah Masoud na hivyo kuvunja kwa kiasi kikubwa mapambano na ngome ya kaskazini mwa Afghanistan. Siku mbili baadaye, majengopacha ya New York yalilipuliwa kupitia shambulio la kigaidi ambapo Wamarekani walilihusisha kundi la al-Qaida na shambulio hilo na hicho kikawa kisingizio kizuri cha kuvamiwa na kushambuliwa kijeshi Afghanistan na majeshi ya Marekani. Afghanistan katika kipindi hicho ilikuwa inaomboleza kifo cha shujaa wake Ahmad Shah Masoud.

Marekani ambayo ilivamia Afghanistan kwa kisingizio cha kupambana na Taliban na al-Qaida, ilifanya mauaji na jinai za kutisha dhidi ya raia wa kawaida wa nchi hiyo bila kufanikiwa kuwatia mbaroni au haikutaka kukamata na kuwaadhibu Mullah Omar na Bin Laden. Mullah Omar baadaye alikimbilia Pakistan. Baada ya kupita miaka mingi tokea matukio hayo yafanyike, hakuna mtu aliye na habari za kuaminika kuhusiana na hatima ya Bin Laden. Licha ya Marekani kudai kuwa ilimuua, lakini hakuna yeyote aliyeona mwili wala kaburi lake.

Uvamizi wa Marekani Afghanistan

Mnamo 2001, wakati miaka kumi na tatu ilikuwa imepita tangu kushindwa Umoja wa Sovieti huko Afghanistan, mpinzani pekee wa umoja huo yaani Marekani, alivamia na kuingia Afghanistan. Marekani inauchukulia ushindi huo kuwa ulitokana na nafasi aliyokuwanayo Usama bin Laden. Bila shaka, mchango wa fikra za kitakfiri za makundi yenye misimamo mikali nchini Afghanistan nao haupaswi kupuuzwa. Fikra ambazo zilienea kwa msaada wa Uwahabi wa Saudia na bado zina nafasi kubwa katika kuvuruga amani na usalama wa Mashariki ya Kati.