Mar 27, 2023 07:07 UTC
  • Hakika ya Uwahabi 16

Marekani kamwe haukudhani kwamba Waislamu ambao hawakuwa na silaha yoyote wangeweza kusimama mbele ya jeshi ambalo lilikuwa limejizatiti kwa akila aina ya silaha za kisasa, kwa lengo la kutetea haki zao. Lakini ilipoona kuwa watu wa Afghanistan walikuwa wamesimama imara kwa ajili ya kutetea maslahi yao, Marekani iliamua kutumia vibaya fursa hiyo kulinda maslahi yake.... yaani wakati wa kusema uongo mkubwa ulikuwa umewadia.

Bismillahir Rahmanir Raheem.

Katika vipindi vilivyopita tuliona namna kuna uhuisiano mkubwa kifikra kati ya makundi ya kigaidi na kitakfiri na Uwahabi na tukaahidi kuwa katika vipindi vinavyokuja tutajaribu kuelewa zaidi uhusiano na mawasiliano yaliyopo kati ya pande hizo. Ili kulifahamu vizuri suala hilo inatupasa kwanza turejee nyuma kidogo katika historia. Karibuni.

******************

Baada ya kumalizika Vita vya Pili vya Dunia, Marekani na Shrikisho la Kisovieti la Urusi zilishindana kwa ajili ya kudhibiti maeneo kadhaa yenye nguvu za kistratijia katika Mashariki ya Kati. Miaka minne baada ya Marekani kushambulia kwa mabomu ya nyuklia mji wa Hiroshima nchini Japan, Urusi ilifanyia majaribio bomu lake la kwanza la nyuklia na hivyo Marekani ikajiepusha kukabiliana nayo moja kwa moja kijeshi. Hiyo haikuwa na maana kuwa huo ndio uliokuwa mwisho wa makabiliano kati ya nchi mbili hizo. Marekani ambayo katika Vita vya Pili vya Dunia iligharamika pakubwa katika kuendesha vita hivyo ilikabiliwa na matizo mengi ya kiuchumi na hivyo haikuwa katika hali nzuri ya kuanzisha vita vingine na hasimu wake huyo wa Urusi. Kwa msingi huo iliamua kudumisha uhasama wake na nchi hiyo kupitia makabiliano yasiyo ya moja kwa moja, makabiliano ambayo yaliendeshwa na wengine kwa niaba yake au kupitia fedha za wengine. Hivyo ndivyo vinavyoitwa 'vita vya niaba.'

Umoha wa Sovieti ambao ulikuwa unafanya juhudi kubwa za kudhibiti hali ya mambo katika Mashariki ya Kati ilifanya jitihada za kuwaweka watawala vibaraka katika nafasi za uongozi nchini Afghanistan ambao wangetii na kutekeleza amri zake. Jambo hilo kamwe halikukubaliwa na watu wa nchi hiyo ya Kiislamu. Umoja wa Sovieti ambao ulitambua vizuri kwamba Marekani haikuwa na ubavu wa kukabiliana nayo kijeshi katika kipindi hicho iliamua kutuma nchini Afghanistan askari wake wa Jeshi Jekundi kwa ajili ya kuiunga mkono serikali ya Kabul.

Takriban mwaka mmoja ulikuwa umepita kabla ya tukio hilo ambapo Mapinduzi ya Kiislamu yalikuwa yametokea nchini Iran kwa uongozi wa Imam Khomeini (MA) na hivyo kuibua matumaini na hamasa mpya katika Umma wa Kiislamu. Moyo wa kupambana na ubeberu na ukoloni ulihuishwa tena miongoni mwa Waislamu wa Afghanistan na hivyo kuwahamasisha kupambana dhidi ya mfumo wa kikomonisti wa Umoja wa Urusi. Burhan ad-Deen Rabbani na Ahmad Shah Masoud walijitokeza miongoni mwa watu wa Afghanistan na kuongoza mapinduzi na mapambano ya Waafghani dhidi ya wavamizi wa kigeni. Burhan ad-Deen ambaye baadaye alikuwa rais wa Afghanistan, katika mojawapo ya safari zake nchini Iran aliyataja Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran kuwa ndiyo yaliwahamasisha Waafghani kuanzisha mapinduzi dhidi ya mabeberu wa kigeni na kwamba shaari na nara zao zilikuwa zili zile zilizopigwa na wananchi wa Iran mwanzoni mwa mapinduzi yao, yaani za kupinga siasa za kambi zote mbili za Magharibi na Mashariki.

Shah Ahmad Masoud (kulia) na Burhan ad-Deen Masoud

*******************

Marekani kamwe haukudhani kwamba Waislamu ambao hawakuwa na silaha yoyote wangeweza kusimama mbele ya jeshi ambalo lilikuwa limejizatiti kwa akila aina ya silaha za kisasa, kwa lengo la kutetea haki zao. Lakini ilipoona kuwa watu wa Afghanistan walikuwa wamesimama imara kwa ajili ya kutetea maslahi yao, Marekani iliamua kutumia vibaya fursa hiyo kulinda maslahi yake.... yaani wakati wa kusema uongo mkubwa ulikuwa umewadia.

Yule yule rais wa Marekani ambaye wakati huo alikuwa akiwatuhumu Waislamu wa Iran kuwa ni maadui wa walimwengu wote na kuzitaka nchi 80 za Mashariki na Magharibi kukabiliana na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, kwa upande wa pili alikuwa akiwasifu Waislamu wa Afghanistan kuwa ni 'wapiganaji katika njia ya uhuru' na kuwaambia: "Hamko peke yenu. Marekani iko pembeni yenu na inashirikiana na nyinyi bega kwa bega kwa kutumia uwezo wake wote wa kimaada na kimaanawi. Kupigana kwa ajili ya kurudisha uhuru ni haki yenu."

Hizi ndizo zile zile siasa zinazoitwa, 'tenganisha ili upate kutawala.'

Kwa upande mmoja wanasiasa wa Marekani waliona kuwa kuendesha vita vya niaba ndilo lililokuwa chaguo bora zaidi la kukabiliana na Umoja wa Sovieti na katika upande wa pili walikuwa na wasi wasi mkubwa kuhusiana na kuenea kwa fikra za kimapinduzi za Imam Khomeini (MA) katika Mashariki ya Kati. Kwa msingi huo waliamua kutumia fursa iliyojitokeza huko Afghanistan kwa maslahi yao na wakati huo huo kukabiliana na Mapinduzi ya Iran, na hivyo kuweza kupiga ndege wawili kwa jiwe moja. Hivyo waliamua kuweka pembeni mila zao za kale za ukaoboy na badala ya kuchukua silaha, wakaamua kutumia vyombo vyao vya habari kwa ajili ya kufikia malengo yao katika nchi mbili hizi za Kiislamu. Habari za vita na Makomonisti nchini Afghanistan zikabadilika kuwa habari zilizopewa kipaumbele katika vyombo vya habari vya nchi za Magharibi. Vyombo hivyo vya habari viliakisi na kuchangamkia habari hizo ni kana kwamba ni Umoja wa Sovieti pekee ndio uliokuwa koloni katika zama hizo na kuwa Marekani na Uingereza hazikuwa na nafasi yoyote katika kupora ardhi za Waislamu. Baada ya kuwakandamiza Waislamu kwa makumi ya miaka, sasa walikuwa wamegeuka na kujidhihirisha kuwa watu wema waliotetea maslahi ya Waislamu.

*******************

Ni katika miaka hiyo hiyo ya mwanzoni mwa vita vya Afghanistan ndipo Abdullah Azzam, aliyekuwa na ndoto kubwa kichwani alisafiri kutoka Saudi Arabia na kuelekea Afghanistan. Azzam ambaye alizaliwa Palestina na kuhitimu shahada ya uzamivu (PhD) ya fiqhi ya Kiislamu katika Chuo cha al-Azhar nchini Misri, alijiunga na kundi la Ikhwanul Muslimeen, takriban wakati mmoja na kuanza kukaliwa kwa mabavu ardhi za Palestina, ambapo alishiriki katika vita vya siku sita vya Waarabu na Wazayuni wa Israel. Abdallah Azzam ambaye alishuhudia kwa macho yake mwenyewe udhaifu mkubwa wa serikali za Kiarabu katika vita hivyo alikwenda Afghanistan akiwa na matumaini makubwa ya kuunda jeshi lenye nguvu na baada ya kukombolewa nchi hiyo alitumie jeshi hilo kwa ajili ya kuikomboa Palestina kutoka mikononi mwa Wazayuni na washirika wao wa Magharibi wakiongozwa na Marekani na Uingereza.

Abdullah Azzam

Taratibu propaganda za vyombo vya habari na misaada mikubwa ya kifedha na hali (kimaanawi) ya Marekani, Saudi Arabia na nchi nyingine kadhaa iliwashawishi vijana wa Kiislamu kutoka pembe zote za dunia kuhamia Afghanistan. Moja ya misaada hiyo ya kimaanawi ni fatwa zilizotolewa na Abdullah Azzam kwa ajili ya kile kilichoitwa kuwa Jihadi, fatwa ambazo zilitiwa saini na kupitishwa na mamufti wakuu wa Kiwahabi wa Saudi Arabia, akiwemo Abdullah bin Baz. Kwa njia hiyo wapiganaji waliokuwa na fikra tofauti kabisa na zinazogongana kuhusu Uislamu walikuwa wamekusanyika sehemu moja huko Afghanistan. Sasa hapa palihitajika kuwa na mtu ambaye angeweza kuliunganisha pamoja kifikra na kimalengo jeshi hilo la watu kutoka mataifa tofauti, na wakati huo huo kuliainishia sera na njia ya maisha mapya, njia ambayo moja ya misingi yake muhimu ilikuwa fikra ya kuwakufurisha Waislamu wengine wasiofuata na kukubaliana na fikra hiyo.

*************

Ili kufikia lengo la kubadilisha fikra ya umoja na mshikamano kati ya Waislamu kuwa ya kuwatenganisha, hakukuwa na chaguo jingine zuri kwa Wamarekani kuliko Mawahabi wa Saudi Arabia.