Jun 25, 2023 08:03 UTC
  • Hakika ya Uwahabi 19

Baada ya Marekani kudai katikati ya mwaka 2011 kwamba ilikuwa imemuua Bin Laden, Ayman al-Zawahiri, kiongozi nambari mbili wa al-Qaeda, alichukua uongozi wa kundi hilo. Tofauti na alivyokuwa Bin Laden, al-Zawahiri hakuwahi kuhimiza kundi lake lipigane dhidi ya Marekani. Mbinu yake ilikuwa ni kupambana na watawala wa nchi za eneo.

Bismillahir Rahmanir Rahiim. Kwa jina la Mwenyezi Mungu, Mjuzi wa siri zote, ambaye kwake yaliyopita na yajayo ni mamoja, na hakuna kinachofichika kwake. Hamjambo wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Hiki kitakuwa kipindi cha mwisho katika mfululizo wa vipindi hivi vya Hakika ya Uwahabi ambavyo tunatumai vimetufaidi sote kwa pamoja.

Baada ya Marekani kudai katikati ya mwaka 2011 kwamba ilikuwa imemuua Bin Laden, Ayman al-Zawahiri, kiongozi nambari mbili wa al-Qaeda, alichukua uongozi wa kundi hilo. Tofauti na alivyokuwa Bin Laden, al-Zawahiri hakuwahi kuhimiza kundi lake lipigane dhidi ya Marekani. Mbinu yake ilikuwa ni kupambana na watawala wa nchi za eneo. Watawala ambao, kwa maoni yake, walitawala na kwenda kinyume na mafundisho ya Uislamu na hivyo akawa anawatuhumu wote kuwa ni makafiri.

Miezi michache kabla ya Ayman al-Zawahiri kuchukua silaha kwa ajili ya kupigana dhidi ya watawala wa eneo, watu wa nchi za Kiarabu walikuwa wameanzisha malalamiko na maandamano makubwa ya amani dhidi ya serikali zao. Maandamano hayo ambayo baadaye yaliitwa "Msimu wa Machipuo wa Waarabu", yalianzia Afrika Kaskazini na kuendelea hadi Kusini Magharibi mwa Asia.

Wachambuzi wengi wa kisiasa waliamini kwamba kufuatia ushindi wa maandamano hayo ya umma, hakukuwepo tena na haja ya uwepo wa makundi ya wabeba silaha kama al-Qaeda. Lakini baada ya kupinduliwa serikali kadhaa katika mkondo huo wa maandamano na malalamiko ya umma, tofauti kati ya makundi ya ndani ziliibuka, jambo ambalo liliandaa mazingira ya kupata nguvu tena  al-Qaeda na makundi mengine ya kigaidi kama Daesh. Kutokuwepo amani na nidhamu, migogoro kati ya makundi mbalimbali, na kupigwa marufuku vyama na jumuiya za Kiislamu katika nchi za Kiislamu, ndicho kisingizio kilichokuwa kikitafutwa na makundi ya kigaidi ya al-Qaeda na Daesh.

Hata katika nchi kama Tunisia, ambako makundi mbalimbali yalifanikiwa kufikia makubaliano na umoja, magaidi wa al-Qaeda na Daesh, walifanya operesheni kadhaa za kigaidi ambapo katika moja ya operesheni hizo, waliua watalii zaidi ya hamsini wa Ulaya na kuhatarisha usalama pamoja na shughuli za uchumi za nchi hiyo. Vitendo hivyo vya ugaidi havikuwa na matokeo mengine isipokuwa kuibua malalamiko ya wananchi, migogoro na vita vya wenyewe kwa wenyewe.

Miaka michache iliyopita, Hillary Clinton, Waziri wa zamani wa Mambo ya Nje wa Marekani, katika mahojiano na kanali ya Fox News, alikiri waziwazi nafasi ya Marekani katika kuunda kundi la al-Qaeda lililoanzishwa na Osama bin Laden. Alisema: "Wakati Wasovieti walipoivamia Afghanistan, tuliamua kwenda Pakistan na kubuni jeshi la Mujahidina na kulipa makombora ya Stinger na silaha zingine.... Baada ya vita kumalizika, tuliwaachilia watu hao waliokuwa wamepata mafunzo ya hali ya juu ya kijeshi, waliojizatiti kwa silaha na wenye misimamo mikali kuenea nchini Afghanistan na Pakistan."

Hillary Clinton alisimulia kumbukumbu zake katika kitabu kinachoitwa "Hard Choices" yaani Maamuzi Magumu, na kukichapisha mwaka 2014. Anataja katika kitabu hicho ukweli kwamba Marekani ilikuwa na nafasi muhimu katika kuanzisha tawi la al-Qaeda nchini Iraq, yaani Daesh, na wakati huo huo kuliimarisha zaidi nchini humo.

Baada ya kung'olewa madarakani utawala wa Baath nchini Iraq mwaka 2003, Abu Musab al-Zarqawi aliingia Iraq na baadhi ya wafuasi wake wenye nia moja. Miaka miwili kabla, alikuwa ameanzisha kundi la al-Tawheed wa al-Jihad nchini Afghanistan. Mwaka 2004, alitambuliwa na Bin Laden kama kiongozi wa tawi la al-Qaeda nchini Iraq. Baada ya kuungana na makundi mengine ya Kisalafi katika nchi hiyo, Zarqawi aliliita kundi lake "al-Qaeda katika Ardhi ya al-Rafidin." Mwanzoni, alitekeleza baadhi ya operesheni dhidi ya vikosi vya Marekani nchini humo, lakini muda si mrefu akaelekeza bunduki yake dhidi ya Mashia na kuwalenga watu wasio na hatia. Kwa kuchochea tofauti za kimadhehebu, alitekeleza kile Wamarekani walikuwa wanataka. Tofauti kama hizo daima zimekuwa kisingizio kizuri cha kuhalalisha uwepo wa wanajeshi wa Marekani katika nchi za Kiislamu.

Zarqawi alianzisha Baraza la Mujahidina kwa shabaha ya kufikia taratibu na mpangilio alioutaka kati ya makundi ya kisalafi lakini baada ya muda mfupi kulizuka hitilabu baina yake na Bin Laden ambapo aliuzuliwa kutoka kwenye nafasi hiyo. Kufuatia hitilafu hizo Zarqawi aliuawa na majeshi ya Marekani na kisha jina la Baraza la Mujahidina likabadilishwa kuwa Dola la Kiislamu la Iraq. Dola hilo lilifanya mambo sawa kabisa na kama walivyofanya mababu zake wa Kiwahabi, yaani lilifasiri Uislamu kama lilivyotaka na kuzituhumu imani za madhehebu mengine ya Kiislamu kuwa za kikafiri. Matokeo ya fikra potofu za kundi hilo yalikuwa ni kuuawa kinyama raia wa kawaida na hasa watoto na wanawake wa Iraq. Hawakutishika wala kuogapa kufanya jinai yoyote ile dhidi ya Waislamu. Walikuwa wakiwakata watu vichwa kikatili na kisha kuwachoma moto bila kujali lolote. Waliwaua wanaume, kuwafanya wanawake kuwa watumwa wa ngono na kuwalazimisha watoto wadogo kujilipua kwa mabomu katika operesheni za kigaidi.

Mwaka 2010 machufuko yaliibuka huko Syria ambapo nchi za Magharibi ziliyatumia kuwasha moto wa fitina miongoni mwa Wasyria, machafuko ambayo yalibadilika haraka na kuwa mapigano makubwa ya wenyewe kwa wenyewe. Katika hali hiyo tawi la al-Qaida nchini Iraq liliona machafuko hayo yakiwa fursa nzuri ya kueneza ushawishi na ugaidi wake katika eneo. Magaidi wa kundi hilo walielekea Syria ambapo waliyashawishi makundi mengine ya kigaidi nchini humo kama Jabhatu an-Nasra kujiunga nao na baada ya kuteka miji kadhaa muhimu ya nchi hiyo, wakabadilisha jina la kundi lao kutoka Dola la Kiislamu la Iraq kuwa Dola la Kiislamu la Iraq na Sham. Jina hilo pia lilibadilishwa baadaye na kuwa Daesh. Kundi hilo lilizichukulia nchi zote za Kiislamu na hata baadhi ya nchi za Ulaya kuwa katika mipaka ya utawala wao, ambapo lilimteua Abu Bakr al-Baghdadi kuwa khalifa wake.

Daesh iliteka na kudhibiti kisima kikubwa zaidi cha mafuta cha Syria, kisima cha gesi, kupora zana na vifaa vya mitambo ya uzalishaji umeme na kuwaua kinyama wafanyakazi wa mitambo hiyo. Hata makaburi na majengo ya kale ya kihistoria pia hayakusalimika kutokana na jinai za Daesh, ambapo walilipua kwa mabomu na bila kujali kaburi la Nabii Yunus (as) nchini Iraq. Kaburi hilo linarejea nyuma katika historia hadi karne ya nane kabla ya kalenda ya Miladia inayotumika hivi sasa. Magaidi wa Daesh vilevile walishambulia jamii ya Mayazidi huko Iraq na kutekeleza unyama wa kupindukia wa kuwaua kikatili wanaume mia tano na kuwachukua wanawake wao kama watumwa wa ngono. Zaidi ya watoto 70 waliuawa kutokana na kiu na njaa waliyopata kufuatia shambulio hilo na zaidi ya familia 30,000 zikalazimika kuishi kama wakimbizi.

Baada ya mauaji hayo ya kinyama dhidi ya watu wa Iraq na Syria, vyombo vya habari vya nchi za Ulaya vilionyesha filamu za mauaji yaliyofanywa na Daesh dhidi ya raia waliodaiwa kuwa wa Ulaya ambapo jambo hilo lilichochea uadui na propaganda za vyombo hivyo dhidi ya Uislamu na Waislamu. Kufuatia propaganda hizo, rais wa wakati huo wa Marekani aliliomba rasmi bunge la nchi hiyo, Congress, kumpa idhini ya kutuma askari katika nchi za Iraq na Syria.

Sio watu wa nchi mbili hizo za Kiarabu pekee bali watu wote wa dunia bila kujali rangi, uraia, dini na madhehebu zao, walionja kwa njia moja au nyingine machungu ya kundi hilo la kigaidi. Watu wa Nigeria, Misri, Tunisia, Yemen na hata wa Ufaransa wanajua Daesh inamaanisha nini katika mtazamo wa ukatili na unyama. Jinai za kundi hilo la kigaidi zilikuwa nyingi na za kutisha kadiri kwamba Kamisheni Huru ya Kimataifa ya Kuchunguza Jinai za Daesh huko Syria ilisisitiza katika ripoti yake ya tarehe 14 Novemba 2014 kwamba kundi hilo lilikuwa limetekeleza jinai dhidi ya binadamu.

Mwanadiplomasia mmoja aliyestaafu wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani kwa jina la Michael Springmann alifichua kwamba operesheni za siri za nchi hiyo katika nchi za Mashariki ya Kati zilipelekea kubuniwa kwa makundi ya kigaidi barani Asia. Kwa mujibu wa mwanadiplomasia huyo, operesheni hizo za siri zingali zinaendelea tangu wakati wa vita baridi. Mbali na hayo, mkuu wa zamani wa shirika la habari za kiulinzi katika wizara ya Ulinzi ya Marekani, Pentagon, alifichua katika mahojiano na televisheni ya al-Jazeera kwamba kuimarika kwa kundi la kigaidi la Daesh kulitokana na uungaji mkono wa moja kwa moja wa Marekani kwa kundi hilo nchini Iraq.

Mwaka 2013 Edward Snowden, mwanakandarasi wa zamani wa Shirika la Usalama wa Taifa la Marekani alifichua baadhi ya habari muhimu dhidi ya vyombo vya usalama vya Marekani. Alisema kuhusiana na uhusiano wa siri wa nchi hiyo na kundi la kigaidi la Daesh kwamba: Vyombo vya usalama vya Marekani, Uingereza na utawala wa Kizayuni wa Israel vilikuwa na nafasi muhimu katika kubuni kundi la Daesh, ambapo kundi hilo liliundwa kupitia mfumo uliopewa jina la "Mzinga wa Nyuki." Edward Snowden anaamini kwa msingi wa nyaraka zilizofichuliwa kwamba kundi la Daesh lilibuniwa kwa ajili ya kuusaidia utawala haramu wa Israel. Anasema lengo la operesheni za 'Mzinga wa Nyuki' ni kubuni makundi ambayo yanatumia nara za Kiislamu kwa ajili ya kuwavutia wafuasi wenye misimamo ya kupindukia mipaka, wanaowakufurisha Waislamu na walioganda kifikra kutoka kila pembe ya dunia kwa madhumuni ya kuelekeza silaha zao dhidi ya nchi zinazopinga uwepo wa utawala haramu wa Kizayuni.