Ni suluhu au ushindani wa kiuchumi? Kongo, Rwanda na maslahi ya kimkakati ya Marekani
Mawaziri wa mambo ya nje wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Rwanda wametia saini makubaliano ya kimsingi ya amani, kwa upatanishi wa Marekani.
Katika makubaliano hayo, mawaziri wa mambo ya nje wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Rwanda wamekubaliana kuwa wataacha kutoa misaada ya kijeshi kwa makundi ya wabeba silaha; aidha watafanya juhudi za kuanzisha utaratibu wa kuratibu usalama ili kukabiliana na makundi yanayobeba silaha na mashirika yanayofanya uhalifu.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Rwanda Olivier Nduhungirehe amesema, makubaliano hayo yanafungua njia ya kufikiwa makubaliano ya uhakika ya amani. Makubaliano hayo yalisainiwa katika kikao kilichohudhuriwa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Marco Rubio, ambaye naye pia alitia saini hati hiyo kama shahidi. Baada ya kusainiwa mkataba wa makubalinao hayo, Rubio aliandika kwenye mtandao wa X: "tangazo la makubaliano ya msingi lililotiwa saini na mawaziri wa mambo ya nje wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Rwanda linafungua njia ya kupatikana amani, utulivu na ustawi katika eneo hilo." Waziri wa mambo ya nje wa Marekani vilevile amekiri kuwa, tangazo hilo litasaidia kulinda maslahi ya kimkakati ya Marekani katika sekta ya rasilimali za madini muhimu kwa ajili ya ukuaji wa sekta yake ya teknolojia, pamoja na kuleta amani na utulivu katika eneo hilo.

Japokuwa kwa kutia saini makubaliano hayo, Kongo na Rwanda zimepiga hatua kubwa kwa ajili ya kuhitimisha mapigano na kurejesha amani na utulivu, lakini ukweli ni kwamba vita hivyo na upatanishi wa Marekani vimefungua njia ya uwepo mkubwa zaidi wa Washington katika eneo hilo, kiasi kwamba waziri wa mambo ya nje wa Marekani ametamka kinagaubaga kuwa makubaliano hayo ni wenzo wa kulinda maslahi ya kimkakati ya Marekani katika kuyatia mkononi madini muhimu ya mashariki mwa Kongo.
Mvutano kati ya Kongo DR na Rwanda una historia ndefu. Chimbuko la mzozo huo linarejea mwanzoni mwa miaka ya 1990, ambapo baada ya kutokea mauaji ya kimbari nchini Rwanda, mamilioni ya wakimbizi wa Kihutu (wengi wao wakiwa ni wale waliotuhumiwa kuhusika katika mauaji ya kimbari) walikimbilia mashariki mwa Kongo DR. Uhamiaji huo mkubwa, sambamba na kukosekana utulivu wa kisiasa wa ndani, uliandaa mazingira ya kutokea vita na migogoro, hususan mashariki mwa Kongo; vita ambavyo Kongo DR inazituhumu Rwanda na Uganda kuwa zinajihusisha navyo; na kwa upande wake, Rwanda inaituhumu Kongo kuwa imewapa hifadhi wanamgambo wa Kihutu (wapinzani wa serikali ya Rwanda). Shutuma hizi za pande zote mbili zimeshadidisha mivutano ya mpakani na kuwafanya mamilioni ya raia walazimike kuyahama makazi yao na kuwa wakimbizi. Hata hivyo, mivutano hiyo imeongezeka zaidi katika miezi ya hivi karibuni, huku nchi nyingi za eneo hilo zikionya juu ya hatari ya kutokea vita vikuu vya kikanda.
Lakini mbali na hayo, sababu za kiuchumi na kiusalama nazo pia zina mchango mkubwa katika mizozo hiyo.
Kongo ni nchi yenye utajiri mkubwa wa rasilimali muhimu za madini hususan katika eneo la mashariki mwa nchi hiyo ambako kuna akiba kubwa ya madini adimu kama vile kobalti, koltani, bati, na dhahabu. Kupigania udhibiti wa rasilimali hizo siku zote imekuwa ndio sababu ya kuzuka vita katika eneo hilo. Pamoja na hayo, katika miongo ya hivi karibuni, sambamba na kupatikana maendeleo ya teknolojia, mataifa makubwa nayo pia yamekuwa yakifanya kila njia kuzitia mkononi rasilimali hizo. Jambo hili limevibadilisha vita vya Kongo DR kutoka kwenye hali ya mzozo wa kikabila na kuwa mzozo wa kijiopolitiki wa kupigania utajiri wa maliasili. Kwa hakika, utajiri wa Kongo sasa umekuwa uwanja wa ushindani kati ya madola yenye nguvu duniani. Migodi ya kobalti na koltani ni nyenzo muhimu sana kwa sekta ya teknolojia ya kisasa, hususan ya utengenezaji wa betri za magari ya umeme, simu za mkononi, na zana za kijeshi; na nusu ya migodi ya kobalti duniani iko mashariki mwa Kongo DR.

Ukweli ni kuwa, vita vya Kongo DR na Rwanda hivi sasa vinatumiwa na viongozi wa Marekani kama fursa kwa Washington ya kujiingiza na kupiga kambi ndani ya nchi hiyo ili kuzifikia moja kwa moja maliasili zake; na wakati huohuo, kuingia kwenye ushindani na China wa kuzihodhi rasilimali hizo. Kwa hakika, makubaliano ya msingi yaliyosainiwa kati ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Rwanda yanaiwezesha Marekani, ikiwa kama muangalizi na mdhamini wa amani, kuwa na nafasi kubwa zaidi katika usimamizi na udhibiti wa maliasili za Kongo. Sambamba na hayo, kwa kupungua machafuko na mapigano ya mpakani na kudhibitiwa makundi yanayobeba silaha, yanaandaliwa mazingira kwa ajili ya uwekezaji wa nchi za Magharibi katika uchimbaji na usafirishaji wa madini ya DRC nje ya nchi; uwekezaji ambao kwa kiwango kikubwa utakuwa chini ya usimamizi wa makampuni ya Marekani na washirika wake wa Magharibi.
Kusema kweli, mkataba wa amani uliosainiwa na Kongo DR na Rwanda ni ushahidi mwingine unaothibitisha ukweli kwamba mataifa ya Afrika yanalipa gharama kubwa ya kurejesha amani na utulivu, huku madola makubwa yenye nguvu yakiwa ndiyo yanayonufaika na hatua hiyo. Kuhusiana na suala hili, siku zijazo zitakuja kuonyesha kama makubaliano hayo yataleta amani ya kudumu au hiyo itakuwa awamu ya mpito tu ya mchezo mkubwa wa kushindania udhibiti wa maliasili za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo…/