China: Tofauti kati ya Iran na Marekani zinapaswa kutatuliwa kupitia mazungumzo
Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa China amesisitiza kuwa, tofauti kati ya Iran na Marekani zinapaswa kutatuliwa kupitia mazungumzo na upatanishi, na akaonya kwamba mvutano kati ya nchi hizo mbili unaweza kuathiri moja kwa moja amani na utulivu katika Asia Magharibi.
Wang Yi amesema hayo katika Mkutano wa Usalama wa Munich na kusisitiza kwamba, migogoro na mizozo yote inapaswa kutatuliwa kupitia upatanishi na kupatiwa ufumbuzi kwa njia ya mazungumzo.
Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa China ameonya kwamba Marekani inapaswa kuwa "tahadhari" katika kuamiliana kwake na Iran, akisema kwamba mvutano kati ya Tehran na Washington unaathiri moja kwa moja amani katika eneo la Asia Magharibi.
Afisa huyo mkuu wa kidiplomasia wa China amesisitiza kwamba "badala ya kuunda migogoro mipya, pande husika zinapaswa kuchukua hatua kwa tahadhari."
Msimamo wa Beijing unakuja wakati ambapo msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China, Mao Ning, alisema hapo awali akijibu vitisho vya Trump dhidi ya Iran kwamba: "Beijing inapinga kuingiliwa masuala ya ndani ya nchi nyingine na matumizi ya nguvu au vitisho katika mahusiano ya kimataifa."
Wang Yi ameongeza: "Tunaamini kwamba uhuru na usalama wa nchi zote lazima ulindwe kikamilifu kwa msaada wa sheria za kimataifa." Mwanadiplomasia huyo wa China alisisitiza kwamba tunatoa wito kwa pande zote kufanya juhudi zaidi ili kudumisha amani na utulivu katika Asia Magharibi.
Hayo yanajiri katika hali ambayo, duru ya pili ya mazungumzo ya Iran na Marekani imepangwa kufanyika Jumanne ijayo, Geneva Uswisi.