Mbunge wa Kongresi: Marekani iliwezesha mauaji ya halaiki Ukanda wa Gaza
Mbunge wa chama cha Democratic katika Kongresi ya Marekani amesema kuwa, msaada wa kijeshi wa Marekani kwa Israel "usio na masharti" uliwezesha mauaji ya halaiki huko Gaza," akibainisha kuwa maelfu ya wanawake na watoto waliuawa katika matukio ambayo "yangeweza kuepukwa kabisa."
Alexandria Ocasio-Cortez amesema hayo katika Mkutano wa Usalama wa Munich, kujibu swali kuhusu haja ya kutathmini upya msaada wa kijeshi kwa utawala wa kizayuuni wa Israel na kueleza bayana kwamba,"msaada usio na masharti, hata iweje, haufikiriki... Ninaamini umewezesha mauaji ya halaiki huko Gaza."
Mbunge huyo ametangaza nia ya kugombea urais kwa tiketi ya chama cha Democratic amesisitiza kwamba, Marekani inawajibika kutekeleza sheria zake, hasa "Sheria za Leahy" zinazokataza kutoa usaidizi wa kijeshi kwa vitengo vya kigeni vinavyohusika katika ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu, akibainisha kuwa, sheria hizi hazitumiki kwa ukali sawa kwa vitengo vya Israel ikilinganishwa na nchi zingine.
Ameonya kwamba usaidizi huu usio na masharti unadhoofisha uaminifu wa Marekani kimataifa na kuhimiza kutokujali ukiukwaji wa haki za binadamu.
Alexandria Ocasio-Cortez ameishutumu serikali ya Rais Donald Trump kwa kujaribu kuirudisha dunia katika enzi ya utawala wa kimabavu, akisema kwamba serikali hiyo inaiondoa Marekani kutoka katika nafasi yake ya kitamaduni katika uongozi wa dunia na kupunguza ushawishi wake barani Ulaya kwa maslahi ya Russia.
Alipoulizwa kama mgombea urais wa chama cha Democratic anapaswa kufikiria upya usaidizi wa kijeshi wa Marekani kwa Israel, Alexandria Ocasio-Cortez alibainisha: "Wazo la usaidizi kamili na usio na masharti, bila kujali vitendo vya mtu binafsi, halina mantiki, na usaidizi wa masharti unafaa zaidi."