Yemen yakishambulia kwa kombora la "Palestina 2" kituo cha anga cha Nevatim cha jeshi la utawala wa Kizayuni
(last modified Sun, 27 Apr 2025 02:35:24 GMT )
Apr 27, 2025 02:35 UTC
  • Yemen yakishambulia kwa kombora la

Msemaji wa vikosi vya ulinzi vya Yemen ametangaza kuwa vikosi hivyo imekishambulia kwa kombora kituo cha jeshi la anga la utawala wa Kizayuni cha Navatim katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu zilizopachikwa jina bandia la Israel.

Brigedia Jenerali Yahya Saree, ameeleza katika taarifa aliyotoa Jumamosi kwamba, katika kuendeleza msimamo wa kuwaunga mkono wananchi wanaodhulumiwa wa Palestina na kulaani mauaji ya kimbari yanayofanywa na utawala wa Kizayuni dhidi ya watu wa Ghaza, kikosi cha makombora cha majeshi ya Yemen kimekilenga kituo cha anga cha utawala huo ghasibu cha Navatim kilichoko kaskazini mwa jangwa la Negev kusini mwa ardhi zinazokaliwa kwa mabavu.
 
Saree amebainisha kuwa operesheni hiyo iliyofanywa kwa kutumia kombora la balestiki la "Palestina 2" ilitekelezwa kwa mafanikio kutokana na mitambo ya ulinzi wa anga ya utawala wa Kizayuni kushindwa kulitungua kombora hilo.
 
Msemaji wa vikosi vya ulinzi vya Yemen ameongeza kuwa, majeshi ya nchi hiyo yataendelea kukabiliana na uvamizi na uchokozi wa Marekani na yataendelea kupanua uwezo wake wa kijeshi kwa kuzingatia mabadiliko yanayojiri kwenye medani ya mapambano na kwa ajili ya kuwaunga mkono wananchi wanaodhulumiwa wa Palestina.
 
Aidha, Brigedia Jenerali Saree amesisitiza kuwa, operesheni za ulinzi na za uungaji mkono wa nchi hiyo zitaendelea hadi pale vita vya Ghaza vitakapokoma na mzingiro dhidi ya eneo hilo utakapoondolewa.
 
Hayo yanajiri katika hali ambayo jeshi la utawala wa Kizayuni lilitangaza Jumamosi asubuhi kwamba kuna kombora lililorushwa kutoka Yemen kuelekea katika maeneo yanayokaliwa kwa mabavu.
 
Chaneli ya 12 ya televisheni ya utawala wa Kizayuni iliripoti mnamo Aprili 14 kwamba zaidi ya makombora 16 ya balestiki yamerushwa kutoka Yemen kuelekea ngome za kijeshi za utawala huo tangu jeshi lake lilipoanzisha tena mashambulizi ya kinyama na mauaji ya kimbari huko Ghaza Machi 18.../