Njozi za Marekani Kujiona Dola Lenye Nguvu za Kipekee Zimefikia Ukingoni?
Profesa Jeffrey Sachs wa Chuo Kikuu cha Columbia amesema: "Vita vya Iran ndio wakati ambapo dhana ya Marekani kuwa dola lenye nguvu za kipekee ilikumbana na ukweli halisi."
Kwa mujibu wa profesa huyo wa Chuo Kikuu cha Columbia, hilo halikuwa pigo na kushindwa kwa utawala au rais fulani tu, bali ni kuporomoka kwa mradi mzima wa sera za nje za Marekani baada ya zama za Vita Baridi. Baada ya kusambaratika Umoja wa Kisovieti wa Urusi ya zamani mwaka 1991, Washington ililifananisha kimakosa ombwe la muda la kutokuwepo dola kuu kinzani na kubaki peke yake kwa sura ya kudumu kama dola pekee lenye nguvu, na hata ikajiita "taifa lenye udharura wa kuwepo", lakini dhana ya kuwepo dunia ya kambi moja pekee yenye nguvu ilikuwa tangu mwanzo wake ni njozi tupu.
Sachs anasisitiza kwamba, kumalizika enzi za Magharibi kuwa nguvu pekee yenye sauti ya juu hakujaanza katika kipindi cha Trump, lakini chimbuko lake linarejea mwaka 1945, kwa sababu ubeberu wa Ulaya na baadaye wa Marekani haujawahi katu kuwa wa kudumu, bali ni hali ya kipekee na iliyotokana na zama za kabla ya viwanda na ustawi wa kiviwanda uliosababishwa na uporaji wa rasilimali za nchi zilizokoloniwa.
Uchokozi wa kijeshi uliofanywa dhidi ya Iran umeweka wazi na hadharani ukweli kwamba, Marekani imefikia kikomo cha nguvu na uwezo wake; na si kwamba imeshindwa kutokana na kadhia ya operesheni ya kijeshi tu, bali ni kwa sababu ule ulimwengu ambao uliiandalia nchi hiyo mazingira ya kuwa dola kuu lenye sauti ya juu haupo tena.
Washington haiwezi tena kuyatwisha madola muhimu ya ukanda huu yale hasa inayoyataka. Iran imehimili na kuvivuka vikwazo, vita vya uwakala, na makabiliano ya moja kwa moja na Marekani; imeweza pia kudumisha mshikamano wake wa ndani, kuimarisha miungano yake ya kikanda, na kuianika mbele ya kadamnasi mipaka ya nguvu za kulazimisha za Marekani. Kwa sababu hiyo, Sachs anaitakidi kuwa, kushindwa kwa Washington hakukuwa kushindwa kijeshi tu, bali ni kushindwa kimkakati na kiidiolojia pia. Tabaka tawala la kisiasa nchini Marekani lingali linataka kuuaminisha ulimwengu kwamba, nchi yoyote inayoonyesha ungangari mbele ya mashinikizo ya Washington imekiuka utaratibu wa asili unaotawala dunia, na kwa hiyo Muqawama na upinzani wa Iran si uhalisia wa kijiopolitiki, bali ni aina ya uasi na ukaidi usioweza kuvumilika.
Profesa huyo wa chuo kikuu cha Columbia ameikosoa dhana iliyonayo Marekani kuhusu uwezo wake wa kuidhibiti mifumo ya kimataifa kwa sura ya kudumu akisema, mara kadhaa Washington imekadiria kwa kiwango cha kupindukia nguvu za nyenzo zake za mashinikizo. Russia imeshajivua kiheshima hali ya kutengwa kifedha, China imeweza kujijengea mifumo inayokwenda sambamba na ya Marekani, na Iran imejiweka kwenye hali inayoendana na mazingira yaliyopo. Dhana kwamba Marekani inaweza kuzigandisha au kuziyeyusha chumi za mataifa mengine wakati wowote ipendapo, ni ya zama za ulimwengu ambao hivi sasa haupo tena.
John Mearsheimer, mwananadharia na msomi mwingine mtajika wa Marekani, yeye analitilia mkazo suala hili kwa mtazamo mwingine. Mearsheimer anaamini kuwa, vita dhidi ya Iran havijadhoofisha nguvu za kijeshi tu za Marekani, lakini pia vimepunguza sana "uwezo wake wa makadirio ya nguvu." Kwa mujibu wa mwanafikra huyo, kutumbukia tena Marekani kwenye kinamasi cha Mashariki ya Kati ndio zawadi ambayo China iliihitajia kwa ajili ya kuimarisha nafasi yake barani Asia.
Profesa Jeffrey Sachs, yeye anasisitiza pia kwamba, hakuna rais yeyote wa Marekani, awe ni Mrepublican au Mdemocrat, anayeweza kuurudisha nyuma mkondo wa kuyoyoma nguvu za Magharibi au wa kuongezeka nguvu za kambi ya Asia. Kwa mtazamo wa Sachs, tatizo hasa si Trump mwenyewe binafsi, bali ni kutoweza Washington kujizoeza na kwenda sambamba na ulimwengu ambao Marekani haibaki tena kuwa dola pekee lenye nguvu kubwa. Na hapa Profesa Sachs anauliza suali la msingi, ambalo ni: Je, Washington inaweza kuukubali ulimwengu wa kambi kadhaa? Au itaendeleza vita visivyowezekana kushinda kwa ajili ya kurudi tena kwenye zama zisizorudika?
Jibu la suali hili, ndilo litakaloamua hatima ya mfumo ujao wa dunia.../