Qalibaf: Hali katika Mlango Bahari wa Hormuz imekuwa “isiyovumilika” kwa Marekani
-
Mohammad Baqer Qalibaf
Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu yaani Bunge la Iran, Mohammad Baqer Qalibaf, ameonya kwamba hali inayoendelea katika Mlango Bahari wa Hormuz imekuwa “isiyovumilika” kwa Marekani, huku akisisitiza kuwa Tehran “bado haijaanza hata hatua zake halisi.”
Katika chapisho aliloweka kwenye X siku ya Jumanne, Qalibaf alisema kuwa “mlingano mpya” unaundwa katika njia hiyo muhimu ya kimkakati.
Ameongeza kuwa: “Usalama wa meli na usafirishaji wa nishati umehatarishwa na Marekani na washirika wake kupitia kuvunja makubaliano ya kusitisha mashambulizi na kuweka mzingiro,” Qalibaf amebaini kuwa. “Bila shaka, nia zao ovu zitapungua.”
Aidha amesisitiza kuwa Iran inafahamu kwa undani shinikizo linaloongezeka kwa Marekani.
Ameongeza kuwa: “Tunajua vyema kwamba kuendelea kwa hali ya sasa ni jambo lisiloweza kuvumilika kwa Marekani, ilhali sisi wenyewe bado hatujaanza hata hatua zetu,”.
Matamshi haya yanakuja wakati ambapo Washington imeongeza chokochoko zake katika Ghuba ya Uajemi na Mlango‑Bahari wa Hormuz—eneo ambalo uwepo wa kijeshi wa Marekani umeendelea kuwa chanzo cha misukosuko ya kikanda na hatari kwa njia za kimataifa za nishati.