Iran yatibua mpango wa Trump kuhusu Kombe la Dunia
https://parstoday.ir/sw/news/world-i138188-iran_yatibua_mpango_wa_trump_kuhusu_kombe_la_dunia
Iran imevuruga mipango ya Rais wa Marekani, Donald Trump, si tu katika nyanja za uchumi, siasa na masuala ya kijeshi kufuatia mvutano kati ya pande hizo mbili, bali pia katika mradi unaohusiana na Kombe la Dunia FIFA 2026.
(last modified 2026-05-05T12:05:33+00:00 )
May 05, 2026 11:51 UTC
  • Trump na Gianni Infantino
    Trump na Gianni Infantino

Iran imevuruga mipango ya Rais wa Marekani, Donald Trump, si tu katika nyanja za uchumi, siasa na masuala ya kijeshi kufuatia mvutano kati ya pande hizo mbili, bali pia katika mradi unaohusiana na Kombe la Dunia FIFA 2026.

Kwa mujibu wa taarifa iliyochapishwa Jumanne na jarida la The Athletic, mpango wa Trump wa kufanikisha mapato ya takriban dola bilioni 30 kupitia Kombe la Dunia umekumbwa na changamoto, baada ya wamiliki wa hoteli katika miji 11 itakayokuwa wenyeji wa mashindano hayo kuripoti kushuka maombi kwa asilimia 60 chini ya matarajio.

Ripoti zinasema kuwa karibu asilimia 70 ya mapato yanayotarajiwa na Marekani kutokana na Kombe la Dunia yanatokana na sekta ya utalii, hasa kupitia mashabiki wanaosafiri kuhudhuria mechi na kutumia huduma za hoteli. Takwimu zilizotolewa na wamiliki wa hoteli zinaonyesha kuwa sehemu kubwa ya malengo hayo haijafikiwa.

Ripoti zinaeleza kuwa hapo awali Trump alifanya mikutano kadhaa ya kutangaza mashindano hayo pamoja na Rais wa FIFA, Gianni Infantino, akilenga kuonyesha kuwa kungekuwako mwitikio mkubwa wa kimataifa.

Hata hivyo, kadiri muda wa kuanza mashindano ya Kombe la Dunia unavyokaribia, takwimu zinaonyesha kuwa mwitikio wa mashabiki ni mdogo kuliko ilivyotarajiwa.

Gazeti la Mirror la Uingereza limeripoti kuwa miongoni mwa sababu zinazochangia kupungua idadi ya wasafiri kwenda Marekani kuhudhuria mashindano ya Kombe la Dunia ni sera za kuchochea vita za Trump, ambazo zimevuruga hali ya Mashariki ya Kati na maeneo mengine duniani.

Aidha, gazeti hilo limetaja sababu nyingine zinazochangia hoteli kubaki na vyumba tupu kuwa ni kupanda bei za tiketi za mechi hadi mara sita zaidi ikilinganishwa na Kombe la Dunia la Qatar, ongezeko la ada za maegesho ya magari hadi mara nne, pamoja na sera kali za utumiaji mabavu za polisi zinazotekelezwa dhidi ya wahamiaji na baadhi ya wasafiri.