Marekani yatuhumiwa kulazimisha makubaliano ya afya na mikataba ya madini nchini Zambia
-
Mulambo Haimbe
Zambia imeishutumu Marekani kwa jaribio la kuhusisha makubaliano ya ufadhili wa sekta ya afya na mikataba ya uchimbaji madini yake ya kimkakati. Hayo yamebainika baada ya balozi wa Marekani anayemaliza muda wake kuikosoa serikali ya Zambia kwa madai ya ufisadi, udhaifu wa utawala, na ukosefu wa ushirikiano na programu za misaada ya Marekani.
Katika hotuba yake ya kuaga tarehe 30 Aprili, Balozi wa Marekani anayemaliza muda wake nchini Zambia, Michael Gonzales, alisema Washington ilikuwa imeipatia Zambia ofa ya zaidi ya dola bilioni 2 za ziada kwa ajili ya afya na msaada wa kiuchumi tangu Oktoba. Hata hivyo, alidai kuwa serikali ya nchi hiyo ya Afrika imekataa kushirikiana katika suala hilo.
Siku ya Jumatatu, Waziri wa Mambo ya Nje wa Zambia, Mulambo Haimbe, alilaani kauli za balozi huyo na kuzitaja kuwa “kinyume cha misingi ya kidiplomasia” na zisizoendana na uhusiano baina ya mataifa yenye mamlaka kamili.
Amesema kuwa ingawa Lusaka inatambua haja ya kuongeza juhudi za kupambana na ufisadi katika sekta ya afya na nyanja nyingine, ilikuwa ni “hila na upotoshaji” kwa Gonzales kudokeza kuwa serikali “inafanya kazi kinyume na maslahi ya wananchi wa Zambia.”
Haimbe alisema katika taarifa kwamba: “Inapaswa kufahamika kwamba kuhusu hati ya makubaliano ya afya iliyopendekezwa, ambayo Marekani iliahidi kutoa msaada wa hadi dola bilioni 2 katika kipindi cha miaka mitano ijayo, Marekani na Zambia bado hazijafikiana juu ya baadhi ya masharti yaliyopendekezwa katika rasimu ya makubaliano hayo.”
Waziri huyo alisema mazungumzo kuhusu makubaliano ya afya yalisimama kutokana na masharti ambayo Zambia inaona kuwa “hayakubaliki,” yakiwemo vifungu vya kubadilishana taarifa ambavyo vinaweza kukiuka haki ya faragha ya raia.
Aidha, amesema Zambia pia ilipinga makubaliano yaliyopendekezwa kuhusu madini muhimu ya kimkakati, akitaja kile alichoeleza kuwa ni msimamo wa Washington wa kutaka kampuni za Marekani zipewe upendeleo maalumu.
Haimbe amesema. “Jambo jingine linaloitia wasiwasi serikali ya Zambia ni kuunganishwa kwa makubaliano na mifumo hii inayopendekezwa, kiasi kwamba kukamilika kwa makubaliano ya madini muhimu kunafanywa kuwa sharti la kufikiwa kwa makubaliano ya afya.”
Zambia ni miongoni mwa wazalishaji wakubwa wa shaba barani Afrika, na imezidi kuvutia mashirika ya kimataifa kutokana na madini yanayotumika katika magari ya umeme, teknolojia za nishati safi, na viwanda vya kisasa.
Haimbe amesema Lusaka inaendelea kuwa tayari kwa mazungumzo na washirika wa kimkakati, ikiwa ni pamoja na Marekani, lakini kwa msingi wa manufaa ya pande zote na kuheshimiana.
Mvutano huo unajiri wakati ambapo kuna ongezeko la tahadhari na upinzani barani Afrika dhidi ya mtindo mpya wa ushirikiano wa afya wa utawala wa Trump. Ghana ilikataa makubaliano ya afya yaliyopendekezwa na Marekani kutokana na wasiwasi kuhusu upatikanaji wa taarifa na mamlaka ya kitaifa, huku Zimbabwe nayo ikikataa ofa ya dola milioni 367 ambayo maafisa wake walisema ilitaka taarifa nyeti za afya, zikiwemo sampuli za virusi na data za ufuatiliaji wa magonjwa. Nchini Kenya, Mahakama Kuu pia imesitisha utekelezaji wa makubaliano yanayofanana na hayo kusubiri uamuzi wa shauri la kisheria kuhusu ulinzi wa taarifa za watu ambazo Marekani inazitaka kama sharti la kutoa msaada.