Boko Haram yauwa wanajeshi 23 katika eneo la Ziwa Chad
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i138206-boko_haram_yauwa_wanajeshi_23_katika_eneo_la_ziwa_chad
Takriban wanajeshi 23 wa Chad wameuawa na 26 kujeruhiwa katika shambulio la wanamgambo wa Boko Haram kwenye kituo cha kijeshi katika eneo la Ziwa Chad.
(last modified 2026-05-06T10:51:59+00:00 )
May 06, 2026 10:49 UTC
  • Boko Haram washambulia kambi ya jeshi ya Chad
    Boko Haram washambulia kambi ya jeshi ya Chad

Takriban wanajeshi 23 wa Chad wameuawa na 26 kujeruhiwa katika shambulio la wanamgambo wa Boko Haram kwenye kituo cha kijeshi katika eneo la Ziwa Chad.

Jeshi la Chad limesema katika taarifa yake kuwa kundi la wanamgambo wa Boko Haram wenye makao yao nchini Nigeria  ambalo kwa muda mrefu limekuwa tishio kuzunguka eneo la Ziwa Chad, linalokutanisha Cameroon, Chad, Niger na Nigeria Jumatatu lilifanya mashambulizi katika kisiwa cha Barka Tolorom huko Chad.

Jeshi la Chad aidha limeeleza kuwa wanamgambo wengi wa Boo Haram wameuawa katika hujuma hiyo.

Katika ujumbe wake alioutuma katika akaunti ya Facebook, Rais Mahamat Idriss Deby Itno amesema kuwa kwa mara nyingine tena kundi la kigaidi la Boko Haram limefanya shambulio la woga katika kambi yetu ya kijeshi huko Barka Tolorom.

Rais wa Chad ametoa pole kufuatia kuawa wanajeshi 23 wa Chad na kusema jeshi la nchi hiyo litaendeleza mapambano kwa ari mpya hadi tishio Boko Haram litakapokomeshwa kikamilifu.