Watoto 1,000 wauawa Palestina katika kipindi cha wiki moja
Watoto wasiopungua 1,000 wa Kipalestina wameuawa shahidi katika kipindi cha juma moja kufuatia wimbi jipya la hujuma na unyaama wa utawala ghasibu wa Israel dhidi ya Wapalestina.
Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi wa Kipalestina (UNRWA) likitoa mfano wa ukosefu wa msaada wa chakula huko Gaza limeripoti kuuawa shahidi watoto elfu moja wa Kipalestina ndani ya wiki moja ya kuanza kwa awamu mpya ya hujuma za utawala ghasibu wa Israel dhidi ya eneo hilo.
Shirika la UNRWA UNRWA limetangaza: Tunashuhudia ongezeko lisilo na mfano wake la vifo vya raia na majeruhi katika Ukanda wa Gaza. Tangu Machi 2, hakuna msaada wowote umeingia Gaza, na hali katika eneo hilo ni ya kusikitisha na kuporomoka.
Aidha taarifa ya UNRWA imeongeza, hakuna msaada wa chakula tena uliosalia katika maghala ya kuhifadhi chakula ili kusambaza kwa watu wa Gaza. Katika hali hii, hatari za maafa zitatokea katika siku zijazo. Tulirekodi kuenea kwa magonjwa ya kuambukiza, hepatitis, na kuongezeka kwa saratani na magonjwa sugu.

Hayo yanaripotiwa katika hali ambayo, Umoja wa Mataifa umetangaza kuwa, eneo la Ukanda wa Gaza litakabiliwa na hali mbaya zaidi ya kibinadamu katika siku za usoni na kwamba, kuna haja ya kuchukuliwa hatua kuzuia kutokea hilo.
Baraza la mawaziri la Israel limeidhinisha muswada wa kupiga marufuku kuingizwa misaada yoyote ya kibinadamu huko Gaza licha ya kwamba Umoja wa Mataifa na mashirika ya kimataifa ya haki za binadamu yameonya kuwa wananchi wa Gaza wamo kwenye mgogoro mbaya zaidi wa kibinadamu tangu utawala wa Kizayuni ulipoanzisha vita vya kikatili vya pande zote dhidi ya ukanda huo, mwezi Oktoba 2023.