Putin aishukuru Korea Kaskazini kwa msaada wake wa kijeshi
(last modified Mon, 28 Apr 2025 07:58:14 GMT )
Apr 28, 2025 07:58 UTC
  • Putin aishukuru Korea Kaskazini kwa msaada wake wa kijeshi

Rais wa Russia, Vladimir Putin ametoa shukrani zake za dhati kwa wanajeshi wa Korea Kaskazini na kiongozi wa nchi hiyo, Kim Jong-un, kwa msaada na uungaji mkono wao katika operesheni ya kuzima uvamizi wa Ukraine.

Jeshi la Russia liliripoti wiki iliyopita habari ya kukomboa kikamilifu maeneo ya mpakani ya Mkoa wa Kursk, ambayo Kiev iliyatwaa Agosti mwaka uliopita, na kukiri kwa mara ya kwanza kwamba wanajeshi wa Korea Kaskazini walishiriki katika operesheni hiyo.

"Marafiki wa Korea Kaskazini walijitolea kwa moyo wa mshikamano, haki na urafiki wa kweli," Putin amesema katika taarifa.

"Tunathamini ushujaa, utaalamu wa hali ya juu na uthubutu wa wapiganaji wa Korea Kaskazini, ambao walipigania nchi yetu kama yao, wakiwa bega kwa bega na wapiganaji wa Russia," ameeleza Putin.

Ujumbe huo wa Rais wa Russia umeongeza kuwa: (Wanajeshi wa Korea Kaskazini) walitekeleza wajibu wao kwa heshima na ushujaa na wamejifunika kwa utukufu usio na wakati.

Aidha Rais wa Russia ameahidi kwamba, wanajeshi wa Korea Kaskazini ambao walipoteza maisha katika operesheni hiyo wataheshimiwa "sawa na ndugu zao (wanajeshi) wa Russia.