SWAPO yaitaka Marekani imuachie Maduro bila masharti yoyote
Chama tawala nchini Namibia cha South West Africa People's Organization (SWAPO), kimetoa wito wa kuachiliwa huru mara moja na bila masharti yoyote Rais wa Venezuela, Nicolas Maduro na mkewe.
Katibu Mkuu wa SWAPO, Sophia Shaningwa amesema SWAPO inalaani vikali hatua ya upande mmoja inayofanywa na Marekani ikiwemo kuishambulia Venezuela na kumteka nyara Maduro, mwenendo ambao inauona ni kinyume na kanuni zilizowekwa za sheria za kimataifa na Mkataba wa Umoja wa Mataifa.
"Hatua kama hizo, ikiwa ni pamoja na uvamizi wa kijeshi wa taifa huru na kuwekwa kizuizini kwa mkuu wa nchi aliyeketi, hudhoofisha kanuni za msingi za uhusiano wa kidiplomasia na kusababisha tishio kubwa kwa utulivu wa kimataifa," ameongeza.
Shaningwa amesema kuwa kama shirika la kisiasa lililoasisiwa kutokana na misururu ya kupinga ukoloni na ubaguzi wa rangi, SWAPO inasisitiza kujitolea kwake kwa kanuni za kujitawala, uhuru, na kuheshimiana kati ya mataifa, kanuni ambazo kwa muda mrefu zimeongoza njia yake ya kujitegemea.
"Tunasisitiza kwamba kila taifa linastahili kupanga njia yake, kuhifadhi utamaduni wake, na watu wake kuwa watawala wa hatima yao wenyewe; bila kulazimishwa kutoka nje," amesema.
Katibu Mkuu wa chama tawala Namibia ameyataka mataifa yote na mashirika ya kimataifa kuheshimu uhuru wa mataifa huru na kuzingatia kikamilifu sheria za kimataifa.
Nchi za Kiafrika zimesisitiza mshikamano wao na Venezuela kufuatia uvamizi uliofanywa na Marekani karibuni, na kumteka nyara Rais Nicolas Maduro, na zimetaka kuheshimiwa sheria za kimataifa.