Kesi ya kinara wa upinzani Tanzania yaendelea kusikilizwa leo
Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam Tanzania, hii leo inaendelea kusikiliza kesi ya kusambaza taarifa za uongo katika mtandao wa Youtube inayomkabili Mwenyekiti wa chama kikuu cha upinzani nchini humo Chadema, Tundu Lissu.
Lissu anakabiliwa na kesi mbili, ya kuchapisha taarifa za uongo mtandaoni na ya uhaini. Kesi ya kuchapisha taarifa za uongo imepangwa kusikilizwa leo na Hakimu Mkazi Mwandamizi, Godfrey Mhini, kwa ajili ya Jamhuri kujibu hoja zake za kupinga kesi kuendeshwa kwa njia ya mtandao.
Alkhamisi iliyopita ya Aprili 24, Lissu aligomea kesi hiyo yake ya kuchapisha taarifa za uongo kwa njia ya mtandao wa Youtube kusikilizwa kwa njia ya video na badala yake alitaka kesi hiyo isikilizwe kwa njia ya wazi.
Awali, wakili wa Serikali Mwandamizi, Job Mrema alikuwa ameieleza Mahakama ya Kisutu mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Geoffrey Mhini kwamba kesi hiyo imeitwa kwa ajili ya mshtakiwa kusomewa hoja za awali na upande wa mashtaka upo tayari, ila mshtakiwa hayupo mahakama hapo.
Wakili wa utetezi, Peter Kibatala alipinga Lissu kusomewa mashitaka kwa njia ya video kwa madai kuwa sheria iko wazi anatakiwa kupelekwa mahakamani.
Haya yanajiri huku taasisi za kiraia na mashirika ya kutetea haki za binadamu yakiendelea kuishinikiza serikali kuwaachilia bila masharti viongozi wa kisiasa waliokamatwa kwa kudai haki, yakisisitiza kuwa hatua hiyo ni muhimu katika kulinda amani ya taifa, hasa kuelekea uchaguzi wa Oktoba.