Trump, Rais wa Marekani anayechukiwa zaidi katika miaka 70 iliyopita
(last modified Tue, 29 Apr 2025 02:16:55 GMT )
Apr 29, 2025 02:16 UTC
  • Trump, Rais wa Marekani anayechukiwa zaidi katika miaka 70 iliyopita

Donald Trump, rais wa Marekani, alirejea kwa mara ya pili Ikulu ya White House akiwa na kiwango cha juu zaidi cha umaarufu tangu kuanza safari yake ya kisiasa. Hata hivyo, utafiti mpya wa mtandao wa habari wa Marekani, CNN, unaonyesha kuwa umaarufu wa Trump umeshuka hadi kiwango cha chini kabisa karibu na siku ya 100 ya kurejea kwake madarakani.

Kwa mujibu wa utafiti huo, kiwango cha umaarufu wa Trump kimefikia asilimia 41 ndani ya siku 100 za kwanza za urais wake, kiwango cha chini zaidi miongoni mwa marais wapya wa Marekani katika kipindi cha angalau miongo saba iliyopita, hata ikilinganishwa na muhula wake wa kwanza. Kuridhika kwa wananchi na utendaji wa Trump kumeanguka kwa alama nne ikilinganishwa na mwezi Machi, na kushuka kwa alama saba kutoka mwishoni mwa Februari. Utafiti huo pia unaonyesha kuwa ni asilimia 22 tu ya Wamarekani wanaoridhishwa kikamilifu na utendaji wa Trump, kiwango cha chini zaidi kuwahi kurekodiwa, huku asilimia 45 wakiwa na upinzani mkali dhidi ya uongozi wake.

Utafiti mwingine wa New York Times na Siena College umebaini kuwa wapiga kura wa Marekani wanaamini Trump amepitiliza mipaka katika jaribio lake la kupanua mamlaka ya utawala wa rais. Pia, wapiga kura wamemwona Trump kama kiongozi asiyeelewa matatizo ya kila siku ya raia wake, hali ambayo imezidisha hasira dhidi ya utawala wake. Katika karibu kila suala kuu, umaarufu wa Trump umeendelea kuporomoka, na imani ya umma katika uwezo wake wa kushughulikia masuala haya muhimu inazidi kuyumba.

Katika siku 100 za kwanza, Trump amechukua hatua nyingi zisizo za kawaida, akifanya matamko yenye utata katika masuala mengi ya ndani na ya kimataifa. Amevuruga utaratibu wa kimataifa, hasa katika biashara, mfumo ambao Marekani ilijenga baada ya Vita Kuu ya Pili ya Dunia. Miongoni mwa hatua zake ni kuzindua upya vita vya ushuru dhidi ya dunia nzima, akitaja mnamo 2 Aprili 2025 kwamba ataweka ushuru wa forodha kwa bidhaa kutoka nchi na maeneo 185. Akilenga hasa China, alitangaza ushuru wa asilimia 145 dhidi ya bidhaa zake, hatua iliyojibiwa na ushuru wa asilimia 125 uliowekwa na Beijing dhidi ya bidhaa za Marekani. Hata hivyo, baadaye Trump aliamuru kusitishwa kwa muda wa siku 90 utekelezaji wa ushuru huo kwa nchi nyingine isipokuwa China.

Wachambuzi wameonya kuwa mzozo huu wa kibiashara kati ya Marekani na China unaweza kuwa na athari kubwa kwa uchumi wa dunia.

Katika sera yake ya "Marekani Kwanza," Trump pia alipunguza misaada ya kigeni kwa baadhi ya nchi na mashirika, akisisitiza kuwa tathmini za kina zifanywe kuhusu uhusiano wa misaada hiyo na vipaumbele vya sera ya nje ya Marekani.

Aliwadhalilisha washirika wa NATO na, kwa nia ya kutekeleza ahadi yake ya kumaliza vita vya Ukraine, alikuwa tayari kutoa nafasi kubwa kwa Russia , hatua iliyopingwa na Ukraine. Hata hivyo, baadaye katika mazishi ya Papa huko Roma, Trump alikutana ana kwa ana na Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky, na kutangaza makubaliano ya kuendeleza mazungumzo ya amani.

Trump akishikilia ubao unaonyesha ongezeko la ushuru kwa bidhaa za nje

Vilevile, Trump alizua mjadala kwa madai yake kuhusu kuunganisha Greenland na Marekani, kuifanya Kanada kuwa jimbo la 51, na kurejesha udhibiti wa Mfereji wa Panama. Katika mtandao wa kijamii wa Truth Social, Trump alidai Marekani ipatiwe haki ya kupita bila malipo katika Mfereji wa Panama na Mfereji wa Suez, madai yaliyokumbana na ukosoaji mkali kutoka Panama na Misri. Wakosoaji wamesema matamshi haya ni uvamizi wa mamlaka ya kitaifa ya nchi nyingine.

Kauli mbiu ya Trump ya "Marekani Kwanza" pia imewafukuza baadhi ya washirika na kuhamasisha wapinzani wa Marekani kuchukua hatua kali zaidi. Imeibua maswali makubwa kuhusu utayari wa Trump kutekeleza ajenda hii kikamilifu.

Katika kipindi hiki kifupi, Trump ametia saini amri nyingi za kiutendaji, ikiwa ni pamoja na kampeni dhidi ya wahamiaji haramu, kuwakamata na kuwarudisha makwao. Pia ameanzisha mashambulizi ya kisiasa dhidi ya vyuo vikuu na wanafunzi wa kimataifa, akifuta viza za mamia ya wanafunzi. Serikali yake iimechukua hatua dhidi ya vyuo vikuu kama Columbia, Harvard, Princeton, Brown, Pennsylvania, Cornell, na Northwestern. Hatua zimechukuliwa dhidi ya vyuo hivyo kutokana na maandamano ya wanafunzi wanaopinga vikali vita vya mauaji ya kimbari yanayotekelezwa na utawala haramu wa Israel dhidi ya  Wapalestina  wa Gaza.

Wachambuzi wengi wanaamini kuwa madhara yaliyosababishwa na Trump kwa Marekani yanaweza kuwa ya muda mrefu, hata kama atabadilisha baadhi ya mitazamo yake. Vita vya ushuru, hasa, vinaonekana kuwa vigumu kurekebishwa kwa sababu Trump anaendelea kushikilia msimamo wake wa kuongeza ushuru kwa bidhaa za nje. Kutokana na hali hii, mataifa mengi, hasa washirika wa Ulaya, wameanza kuimarisha sekta zao za ulinzi na kutafuta njia za kupunguza utegemezi wao kwa Marekani, huku baadhi ya nchi kama Ufaransa zikisukuma kuunda muungano mpya wa kijeshi usiohusisha Marekani ambao umetajwa kuwa "NATO ya Ulaya."