Afrika Kusini yaiambia ICJ: Gaza imekuwa Jahannamu, Israel lazima iwajibishwe
Ujumbe wa Afrika Kusini umeiambia Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ) kwamba Ukanda wa Gaza umekuwa Jahannamu kwa Wapalestina na umetaka Israel iwajibishwe kwa uhalifu wake katika eneo hilo la Palestina.
Akizungumza katika kikao cha leo cha Mahakama ya Kimataifa ya Haki kuhusu uwepo wa Umoja wa Mataifa na mashirika ya kimataifa katika maeneo yanayokaliwa kwa mabavu ya Palestina, mjumbe wa Afrika Kusini amethibitisha kuwa Israel inakiuka mikataba ya kimataifa kama nchi mvamizi.
Amesema kuwa Israel inazuia kwa makusudi kuingia misaada ya kibinadamu katika eneo la Ukanda wa Gaza na inaliandama kwa makusudi Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi wa Kipalestina (UNRWA) ili kuwatesa Wapalestina.
Mahakama ya Kimataifa ya Haki ilianza jana vikao vyake vya kujadili ombi lililowasilishwa na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa la kutoa rai ya ushauri kuhusu wajibu wa Israel kuwezesha uwepo wa mashirika ya Umoja wa Mataifa katika maeneo yanayokaliwa kwa mabavu ya Palestina.
Awali mahakama hiyo ilisema kuwa nchi 40 na mashirika manne ya kimataifa na ya kikanda yameeleza nia yao ya kushiriki katika mashtaka dhidi ya Israel mbele ya mahakama ya The Hague, Uholanzi, na kutangaza kuwa vikao vya kusikiliza kesi hizo vitaendelea hadi tarehe 2 Mei.
Haya yanajiri baada ya Bunge la Israel (Knesset) kuidhinisha sheria ya kupiga marufuku shughuli za UNRWA, licha ya Wapalestina kuhitaji huduma zake hasa katika kipindi cha sasa cha mauaji ya kimbari yanayofanywa na Israel.