Jun 07, 2023 04:00 UTC
  • Hakika ya Uwahabi 17

Mwaka 1979, wakati ambapo Umoja wa Kisovieti uliamua kutuma jeshi lake kwenda Afghanistan kwa ajili ya kusaidia na kuviunga mkono vyama vya kikomunisti, Waislamu wote wa Afghanistan, bila kujali dini, mila na madhehebu zao walisimama na kupinga vikali uamuzi huo.

Bismillahir Rahmanir Raheem. Kwa jina la Mwenyezi Mungu, Mola wa Mujahidina ambao hutoa roho, mali na watoto wao katika njia ya Mwenyezi Mungu kwa ajili ya kupata radhi zake. 

Vijana shupavu na wenye nia njema walijitokeza miongoni mwa watu na kuingia uwanjani, ambapo licha ya umri wao mdogo, waliweza kuchukua uongozi wa mapambano dhidi ya jeshi la Umoja wa Kisovieti na hivyo kuibua matumaini ya ushindi dhidi ya moja ya majeshi makubwa zaidi duniani, katika mioyo ya watu wa nchi hiyo. Mmoja wa vijana hao waliomjua Mungu na jasiri ni yule ambaye watu wa Afghanistan wanamfahamu kwa jina la "Amir Sahib". Jina lake halisi ni Ahmad Shah Massoud. Ni mzaliwa wa moja ya vijiji vya Afghanistan ambaye alitumia umri wake wa utotoni na ujanani kughani mashairi ya Saadi, Hafidh na Maulana, lakini hatima ilimpokonya vitabu vya mashairi na badala yake kumkabidhi bunduki kwa ajili ya kuendesha mapambano dhidi ya maadui wa nchi yake. Pamoja na hayo lakini bunduki hiyo haikuweza kuathiri wala kuondoa upole aliokuwa nao moyoni. Ni huruma na upole huo ndio ulimshawishi kusimama kwa ajili ya kuwatetea watu waliodhulumiwa wa Afghanistan na kumhamasisha kuchukua silaha kupigana dhidi ya dhulma na uonevu.

Ahmad Shah Masoud

Baada ya kupitia kozi fupi ya mafunzo ya kijeshi, Ahmad Shah Massoud  aliingia katika uwanja wa mapambano alipokuwa na umri wa miaka 26 tu, na taratibu akaibuka kuwa kamanda asiyeshindwa katika medani ya vita ambapo aliweza kulifanya Bonde la Panjshir na sehemu kubwa ya kaskazini mwa Afghanistan kuwa  eneo lisilofikiwa na jeshi jekundu la Umoja wa Sovieti. Ni moyo wa mapambano ulioonyeshwa na vijana kama hao shupavu na waliojitolea wa Afgjanistan ndio uliwafanya magaidi ambao hawakuwa na lengo jingine isipokuwa kugombania madaraka, nao waamue kubeba silaha na kujipenyeza katika safu za mujahidina halisi wa nchi hiyo, kwa madai ya kutetea haki za watu wa Afghanistan.

Marekani ambayo katika kipindi hicho ilikuwa na woga mkubwa wa kukabiliana moja kwa moja na jeshi la Umoja wa Sovieti, iliamua kupiga ngoma ya vita na kuongeza kuni kwenye moto wa vita vilivyokuwa vimepamba moto kati ya jeshi hilo na mujahidina wa Afghanistan, ili kulinda maslahi yake binafsi. Licha ya kuwa Marekani imekuwa ikifuatilia kwa muda mrefu suala la kuwa na ushawishi mkubwa nchini Afghanistan kwa ajili ya kupora utajiri wa nchi hiyo lakini hilo halikuwa lengo pekee la nchi hiyo katika kuingilia masuala ya ndani ya Afghanistan. Lengo jingine la uchochezi na uingiliaji huo lilikuwa ni kuiandalia Marekani fursa ya kuweza kukabiliana na hatari ya kuibuka mapambano kama hayo ya Afghanistan katika nchi ilizokuwa chini ya ushawishi na udhibiti wake.

Baada ya kumalizika Vita vya Pili vya Dunia, Marekani iliweka serikali na tawala bandia katika nchi zilizokuwa ndio kwanza zimepata uhuru na kulichukulia jambo hilo kuwa ishara ya nia njema na ukarimu wake kwa nchi hizo kwa kuzisaidia kujitawala. Kwa kawaida watawala waliopewa fursa ya kutawala katika nchi hizo walikuwa vibaraka ambao walikuwa wakifutilia umashuhuri, madaraka na utajiri wa haraka na ambao walikuwa tayari kutoa na kuuza shakhasia pamoja na maslahi ya watu wao kwa ajili ya kufikia lengo hilo la kibinafsi. Badala ya vibaraka hao kufikiria jinsi ya kutetea na kulinda maslahi makubwa ya mataifa yao waliamua kushirikiana na Marekani kwa ajili ya kulinda maslahi yake katika eneo. Katika nchi hizo zote ambazo kivitendo zilikuwa makoloni ya Marekani, kulikuwa na makundi na vyama mbavyo havikutambua rasmi tawala hizo vibaraka zilizopewa madaraka kwa ajili ya kuhudumia maslahi ya Marekani na hivyo vikaamua kuendesha mapambano dhidi yazo, jambo ambalo lilichukuliwa na Marekani pamoja na vibaraka wake katika eneo kuwa kengele ya hatari.

Kufuatia kupamba moto mapambano nchini Afghanistan na Umoja wa Sovieti kuamua kutuma kwa wingi askari wake katika nchi hiyo, Marekani ambayo katika kipindi hicho ilikuwa ni kama fisi aliyevalia ngozi ya kondoo, ilitumia hadaa kubwa kwa kujifanya kuwa mtetezi wa Waislamu ambapo iliwadanganya na kuwafanya wasahau mapambano yao dhidi ya serikali vibaraka na fasidi zilizokuwa zinaunga mkono Marekani, na kuwashawishi waelekeze nguvu na mapambano yao dhidi ya Warusi makafiri na madhalimu. Makundi mengi ya Waislamu yaliamua kuelekea Afghanistan kwa lengo hilo hilo ambapo nchi za Saudi Arabia na Afghanistan zilipewa jukumu la kuwapa mafunzo ya kijeshi kwa ajili ya kupambana na Warusi. Katika vita hivyo mmoja wa maadui wa Marekani aliweza kushindwa lakini wakati huohuo adui mwingine akawa ameibuka kuwa msindi mkubwa wa vita hivyo, jambo ambalo liliiletea Marekani changamoto nyingine mpya.

Wakati Umoja wa Sovieti uliposhindwa, si watu wa Afganistan na mujahidina wa nchi hiyo tu ndio walijiona kuwa washindi wa vita, bali makundi yote ya Waislamu yaliyoshiriki katika vita yalichukuliwa kuwa washindi. Kila moja ya makundi hayo yalikuwa na malengo yao maalumu ya kushiriki vita hivyo lakini watu waliokuwa wakiyatazama kwa mbali waliona kuwa yote yalikuwa yamepata ushindi na kuwa mashujaa katika vita hivyo. Moja ya makundi hayo ni ya vijana wa Kiarabu walioamua kushiriki vita hivyo kutokana na propaganda kubwa iliyoenezwa na vyombo vya habari vya Marekani, vijana ambao walijulikana baadaye kama Waarabu Waafghani. Sasa wakati ulikuwa umewadia kwa vijana hao kurejea katika nchi zao, lakini kutokana na kuwa walikuwa wanarejea kama mashujaa wa vita, walikuwa wamebadilika na kuwa tishio kubwa kwa watawala vibaraka na washirika wa Marekani katika nchi za Kiislamu. Vijana hao waliweza kuwashinda maadui wao nchini Afghanistan hali ya kuwa hawakuwa na uzoefu mkubwa wa kupigana vita, hawakuwa mashujaa wala kupata mafunzo yanayofaa ya kijeshi. Lakini sasa bila shaka hali ilikuwa tofauti kwa kutilia maanani kuwa walikuwa wanarejea katika nchi zao hali ya kuwa walikuwa wamepata mafunzo ya kutosha ya kijeshi na kushiriki katika vita vikubwa kwa muda wa mika tisa nchini Afghanistan. Bila shaka hiyo ilikuwa ishara ya hatari kubwa kwa maadui wao.

Mbali na hayo, changamoto nyingine ambayo ilitolewa na Waarabu Waafghani ni kutilia shaka madai ya ubora wa nguvu za kijeshi za Marekani dhidi ya washirika na waitifaki wake. Marekani daima ilifanya juhudi za kujidhihirisha kuwa na nguvu kubwa ya kuweza kukabiliana na hatari yoyote ile katika eneo lakini sasa kwa kudhihiri Waarabu Waafghani ilianza kuingiwa na wasiwasi mkubwa. Nguvu na ubabe huo wa Marekani ulikusudiwa kuiwezesha kupenya na kujidhihirisha zaidi miongoni mwa watu wa Afghanistan ambao walipasa kuitazama si kama adui, bali kama shujaa ambaye aliweza kuwaletea ushindi na wakati huo huo aliye na uwezo wa kuwatatulia matatizo yao yote. Ili kujidhihirisha kuwa shujaa anayeweza kukabiliana na hatari yoyote ile duniani, Marekani kwa muda wa miaka mingi nyuma ilikuwa tayari imelifikiria jambo hilo na kuanza kutengeneza filamu za kuwakubalisha kwa nguvu walimwengu ubabe wake bandia na ndio maana ikaaanzisha sekta kubwa ya utengenezaji filamu ya Hollywood. Filamu hizo zilibuni wachezafilamu bandia ambao walikuwa na uwezo na nguvu zisizo za kawaida mbazo zilikuwa nje kabisa ya mipaka ya uwezo wa mwanadamu. Jambo la kushangaza ni kuwa wote walioibuka kuwa washindi wa mwisho na mashujaa kwenye filamu hizo ni watu kutoka nchi za Magharibi na hasa Marekani. Lakini katika ulimwengu wa kweli na hakika isiyokuwa ndoto ya Hollywood, vita vya Afghanistan viliibua mashujaa wa kweli ambao hawakufanana kwa vyo vyote vile na wale bandia waliobuniwa na filamu za Marekani. Hawakuwa na rangi, nywele, macho wala mavazi yaliyofanana na mashujaa hao bandia wa Hollywood, bali walikuwa mashujaa wa kweli. Kwa mtazamo wa Marekani, mashujaa hao hawakupasa kurejea katika nchi zao wakiwa mashujaa wa kweli bali walipasa kubadilishwa kuwa watu wanyonge na duni ambao hawakuwa na uwezo wa kusimama mbele ya nguvu isiyo ya kawaida ya Marekani.

Filamu bandia za Hollywood

Kiongozi wa kwanza wa Waarabu Waafghani alikuwa Abdullah Yusuf Azzam ambaye alikuwa Mpalestina aliyezaliwa katika kijiji cha Silat al-Harithiya kaskazini magharibi mwa mji wa Jenin. Lakini muda baada ya hapo Usama bin Laden akajiunga na kushirikiana naye kwa karibu. Bin Laden alikuwa bilionea wa Saudi Arabia aliyekuwa karibu sana na wanawafalme wa nchi hiyo na ambaye mwanzoni alipewa jukumu la kuwafikishia mujahidina wa Afghanistan silaha za Kimarekani, lakini baadaye taratibu akawa kamanda wa kijeshi. Baada ya kulishinda jeshi la Umoja wa Sovieti nchini Afghanistan, Azzam alikuwa na lengo la kuwatumia mujahidina Waarabu Waafghani katika mapambano dhidi ya maghasibu wa Kizayuni huko Palestina lakini Marekani ambayo ilikuwa na ingali muungaji mkono mkubwa wa maghasibu hao ilipanga na kutekeleza njama ya kumuua pamoja na watoto wake wawili wa kiume. Baada ya mauaji hayo ya kigaidi, sasa Usama bin Laden akawa kiongozi asiye na mpinzani wa kundi hilo la mujahidina Warabu Waafghani na hivyo kuweza kuwa na nafasi muhimu katika kutekeleza matakwa na malengo ya Marekani katika eneo na hasa nchini Afghanistan. Kinyume na alivyokuwa Azzam ambaye alisisitiza juu ya kupambana na serikali fasidi katika eneo na hasa utawala wa kigaidi wa Israel, Usama bin Laden aliwataka wapiganaji wake wapambane moja kwa moja na Marekani na hivyo kuwaandalia Wamarekani kisingizio kizuri cha kutuma maelfu ya wanajeshi wake katika eneo.

Usama bin Laden

 

Kufuatia wito huo, balozi za Marekani nchini Kenya na Tanzania zilishambuliwa na wafuasi wa kundi hilo ambalo sasa lilikuwa linajiita al-Qaida. Mashambulio hayo kwa ujumla yalisababisha vifo vya watu wapatao 530 ambapo hata hivyo wahanga wengi wa matukio hayo ya kigaidi walikuwa raia wa kawaida wa nchi hizo za Kiafrika. Licha ya maafa na hasara iliyosababishwa na matukio hayo, lakini hayakuwa na ukubwa wa kuwafanya walimwengu wahalalishe hatua ya kivamizi ya 'shujaa wa mashujaa' (Marekani) kutuma wanajeshi wake nchini Afghanistan na kwa hivyo hatua nyingine bandia ya kigaidi ilipaswa kutekelezwa ili kuhalalisha uvamizi kama huo wa kijeshi, na huo ukawa mwanzo wa kulipuliwa na kundi la al-Qaida majengo pacha ya kibiashara mjini New York. Baada ya kulipuliwa majengo hayo, Marekani ikawa imepata kisingizio kizuri cha kuivamia Afghanistan na kutuma majeshi yake katika eneo. Sasa wakati ulikuwa umewadia kwa 'shujaa wa mashujaa' kukabiliana moja kwa moja na shujaa aliyeonekana kuwa mnyonge na dhaifu, sawa kabisa kama inavyofanyika katika filamu za Hollywood za nchini Marekani.