Oct 30, 2022 11:42 UTC
  • Mchango wa Maulamaa wa Kishia Katika Uislamu (54)

Assalaamu alaykum wapenzi wasikilizaji popote pale mlipo. Karibuni kujiunga nami tena katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Mchango wa Maulamaa wa Kishia Katika Uislamu ili kwa pamoja tuweze kufungua ukurasa mwingine katika kurasa za historia ya Maulamaa na wanazuoni wa Kishia pamoja na mchango wao katika Uislamu bila kusahau athari na vitabu vyao mashuhuri.

 

Kipindi chetu kilichotangulia kilitupia jicho maisha ya Mirza Masih Mujtahid. Mirza Masih Mujtahid alizaliwa 1193 Hijria katika mji wa kijani kibichi na wenye mandhari nzuri wa Asterabad nchini Iran, mji ambao leo unajulikana kwa jina la Gorgan. Baba yake Kadhi Saeed Asterabad alitambulika kama mtu mwenye fadhila na mchamungu. Kipindi chetu cha wiki kitamzungumzia Ayatullah Sheikh Muhammad Taqi Baraghani mmoja wa wanazuoni aliyeishi katika karne ya 13 Hijria. Kuweni nami hadi mwisho wa kipindi hiki.

 

Mulla Muhhammad Taqi Baraghani alizaliwa mwaka 1172 Hijria katika kijiji cha Baraghan Taleghan Iran. Mwanazuoni huyu alizaliwa katika familia ya wasomi na iliyokuwa na mapenzi makubwa na Ahlul-Beiti (as). Baba yake ni Ayatullah Mulla Muhammad Malaikeh Baraghani alimu, fakihi na mwanazuoni aliyekuwa mashuhuri kwa taqwa na uchaji Mungu na aliyekuwa akiheshimiwa mno katika jamii ambapo ametoa mchango mkubwa wa kueneza madhehebu ya Ushia. Muhammad Taqi Baraghani alihajiri pamoja na baba yake akiwa angali mdogo na kuelekea katika mji wa Qazvin, Iran.

Katika zama hizo mji wa Qazvin ulikuwa moja ya vituo vya kielimu vya maktaba ya Ushia. Baba yake Muhammad Taqi alifanya hima na idili kubwa katika mji wa Qazvin kwa ajili ya kubainisha na kueneza mafundisho ya madhehebu ya Ahlul-Beiti (as) sambamba na kukabiliana na upotofu wa kifikra. Baada ya Muhammad Taqi kukamilisha masomo ya awali na ya msingi kwa baba yake, alifunga virago na kuanza safari ya kuelekea katika maeneo tofauti kwa minajili ya kutafuta elimu na akiwa katika njia hiyo alivumilia taabu na masaibu mengi. Awali alielekea katika Chuo Kikuu cha Kidini (Hawza) cha mjini Qum na kisha Isfahan na kunufaika na bahari kubwa ya elimu ya walimu stadi na mahiri wa zama hizo. Baadaye alifunga safari na kuelekea katika miji ya Karbala na Najaf huko Iraq kwa ajili ya kujiendeleza zaidi kielimu. Baada ya kuhitimu masomo yake huko Iraq aliamua kurejea Tehran. Katika safari zake hizo, Muhammad Taqi Baraghani alihudhuria masomo na kunufaika na vikao na darsa za walimu na wanazuoni mahiri wa zama hizo kama Ayatullah Bahbahani Hairi, Sayyid Ali Tabatabai na Allama Kashiful-Ghitaa. Ni baada ya hapo ndio alipoondokea kuwa mwalimu mahiri katika elimu za kiakili na nakili. Baada ya kuweko kwa miaka mingi akisoma huko Iraq, aliamua kurejea nchini Iran na kuuchagua mji wa Tehran kuwa makazi yake.

 

Muda mfupi tu baada ya kuanza kuishi Tehran, daraja yake ya elimu na tabia njema vilidhihirika na kufahamika miongoni mwa watu na wanafunzi kutoka maeneo ya karibu na ya mbali wakaanza kumiminika kwake kwa ajili ya kunufaika na chemchemi ya elimu na maarifa aliyokuwa nayo.

 

Mbali na hima kubwa aliyoifanya katika kufundisha na kulea wanafunzi, msomi huyo ambaye anajulikana pia kwa lakabu ya Mujtajid Baraghani hakuwa nyuma katika uga wa utunzi na kualifu vitabu ambapo ameviritisha vizazi vilivyokuja baada yake vitabu vingi na vyenye thamani kubwa katika uga wa fikihi, usuli, hadithi na tafsiri. Kitabu chake muhimu ni "Majalis al-Mutaqin" ambapo kuna jumla ya faslu na milango hamsini na kila mlango una mawaidha na hadithi za Imam Hussein pamoja na kueleza masaibu yaliyompata Imam Hussein bin Ali bin Abi Twalib (as). Uyun al-Usul, ni kitabu chake kingine ambacho kinazungumzia kwa mapana na marefu na kwa ukamilifu elimu ya Usul al-Fikih. Aidha Muhammad Taqi Baraghani ana kitabu kingine kinachojulikana kwa jina la Manhaj al-Ijtihad ambacho kinahesabiwa kama kitabu chake muhimu zaidi. Kitabu hiki kina jumla ya mijalada 24 na ni mjumuiko wa hukumu na sheria za Kiislamu.

Maisha ya Mulla Muhammad Baraghani nchini Iran yalisadifiana na duru ya uongozi usio stahiki wa Fat'h Ali Shah Qajar. Kutokana na udhaifu wa utawala wa wakati huo wa Iran, kuliibuka vita baina ya Iran na Russia na maeneo ya kaskazini mwa Iran yakaporwa na kukaliwa kwa mabavu na jeshi la Urusi. Baada ya Iran kushindwa na Urusi, kukaibuka mashindano baina ya Ufaransa na Uingereza kwa ajili ya kupora mali na utajiri wa Iran. Waingereza walitumia vibaya udhaifu wa utawala wa wakati huo wa Iran kiasi kwamba, walikuwa wakiingilia masuala yote ya ndani ya Iran.

Katika mazingira kama haya, Mujtahid Baraghani kwa mara ya kwanza alizungumzia nadharia ya Wilayat al-Faqif (Fakihi Mtawala) mbele ya Fat'h Ali Shah Qajar kikao ambacho kilihudhuriwa pia na wanazuoni na Maulamaa mbalimbali. Aidha alitangaza kuwa, utawala wa kifalme ni haramu na sio halali na hivyo akatoa pendekezo la kunyang'anywa mamlaka mfalme pamoja na wanamfalme. Miongoni mwa waliohudhuria kikao hicho ni Maulamaa akiwemo nduguye Sheikh Muhammad Taqi Baraghani ambao walitangaza kuunga mkono fikra na mtazamo huo wa Mujtahid Baraghani. Aidha walitangaza kuwa, kwa mujibu wa dini katika kipindi cha ghaiba na kutokuweko Imam Maasumu (as), masuala ya utawala kama vita, kufanya sulhu, kufanya mazungumzo na madola ya kigeni na kadhalika, yanapaswa kufanyikka kwa idhini na ruhusa ya fakihi aliyetimiza masharti na kwamba, mfalme hana ustahiki. Fat'h Ali Shah ambaye alikuwa ameingiwa na woga wa hukumu hiyo ya alimu huyo, akiwa na lengo la kusalimika na hilo aliona kuwa, njia pekee ni kumbadishia Iraq Muhammad Taqi Baraghani pamoja na kaka zake. Baada ya kubaidishwa na kupelekwa uhamishoni huko Iraq, kwa muda fulani aliishi katika miji ya Karbala na Najaf.

Picha pekee iliyobakia ya Mulla Muhammad Taqi Baraghani

 

 

Wakati Sheikh Jaafar Kashif al-Ghitaa alipoalikwa Iran na utawala wa wakati huo, aliambatana katika safari yake hiyo ya kuelekea Tehran na Mujtahid Baraghani pamoja na kaka zake. Fat'h Ali Shah Qajar alikuwa ameruhusu Mujtahid Baraghani arejee Iran lakini kwa sharti kwamba, asiwe katika mji wa Tehran. Baada ya kurejea Iran, Mulla Muhammad Taqi Baraghani alielekea Qazvin na kuufanya mji huo kuwa kituo chake cha harakati za kielimu.

Katika zama za Shahidi Thani, kulikuwa kumeanzishwa na kuibuka harakati za kifikra na harakati mbalimbali potofu ambazo zilikuwa zimeanza kutanua wigo wake pia na endapo kusingefanyika juhudi za Maulamaa wa Kishia katika kuweka wazi mambo na kuleta welewa sambamba na kubainisha shubha na utata uliokuwa ukionyeshwa na harakati hizo, kulikuwa na uwezekano wa kutokea upotoshaji kikamilifu kuhusiana na madhehebu ya Kishia.

Hatimaye alimu huyo aliuawa shahidi akiwa katika mihrabu msikitini usiku wa tarehe 15 Dhul-Qaadah mwaka 1263 Hijra. Baada ya kuuawa katika njia ya kutetea madhehebu ya Ushia aliondokea kuwa mashuhuri baina ya Mashia kwa jina la Shahidi Thalith yaani Shahidi wa Tatu.

Mwanazuoni huyo alikuwa ameusia kwamba, mwili wake uzikwe Karbala. Hata hivyo kutokana na mazingira yaliyokuwa wakati huo, ilishindikana kutekeleza wasia wake huo. Hivyo wanawe waliamua kumzika katika mji wa Qazvin huku wakisubiri kuuhamisha mwili wa baba yao huyo endapo mazingira ya kuupeleka Karbala yatapatikana. Baada ya miaka 16 walifukua kaburi hilo kwa nia ya kuuhamishia mwili wa baba yao huko Karbala. Waliukuta mwili huo ukiwa salama salmini. Baada ya wananchi wa Qazvin kusikia tukio hilo walikusanyika kwa wingi kwa lengo la kuzuia kusafirishwa mwili huo kuelekea Karbala ambapo waliangua vilio na kuitafadhalisha familia ya alimu huyo isiusafirshe mwili huo. Hadi leo, kaburi la Shahidi wa Tatu yaani Mulla Muhammad Baraghani lipo katika mji wa Qazvin nchini Iran ambapo waumini kutoka maeneo mbalimbali hulizuru na kulitembelea.

Wapenzi wasikilizaji muda wa kipindi chetu kwa juma hili umefikia tamati, tukutane tena wiki ijayo.

Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh