Nov 12, 2022 12:40 UTC
  • Mchango wa Maulamaa wa Kishia Katika Uislamu (56)

Ni wakati mwingine tunapokutana tena wapenzi wasikilizaji katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Mchango wa Maulamaa wa Kishia Katika Uislamuambacho hutupia jicho historia ya Maulamaa na wanazuoni wa Kishia pamoja na mchango wao katika Uislamu.

 

Kipindi chetu kilichopita kilitupia jicho kwa mukhtasari historia na maisha ya Muhammad Sharif Mazandarani mashuhuri kwa lakabu ya Sharif al-Ulamaa Mazandarani. Tulieleza kuwa, Sharif al-Ulamaa ambaye jina lake kamili ni Muhammad Sharif bin Hassan Ali Amoli Mazandarani Hairi alizaliwa takribani mwaka 1200 Hijria katika mji wa Karbala Iraq. Baba yake ni Mullah Hassan Ali Amoli aliyekuwa mmoja wa wanazuoni wachamungu katika zama zake ambaye asili yake ilikuwa mji wa Mazandaran wa kaskazini mwa Iran.   Kipindi chetu cha juma hili ambacho ni sehemu ya 56 ya mfululizo huu kitamzungumzia Ayatullah Muhammad Hassan bin Baqir Sharif Najafi mashuhuri zaidi kwa lakabu ya Swahib al-Jawahir.

 

Ayatullah Muhammad Hassan bin Baqir mashuhuri kwa lakabu ya Swahib al-Jawahir ni mmoja wa Maulamaa wakubwa aliyekuwa na kipaji cha aina yake katika karne ya 13 Hiijria ambaye alichukua jukumu la Umarjaa wa Kishia katika zama hizo akiwa na sifa na ustahiki kamili. Ayatullah Muhammad Hassan bin Baqir ni mwanafunzi wa Sheikh Ja'afar Kashif al-Ghitaa na Sayyid Muhammad Jawad Amili mwandishi wa kitabu cha Miftah al-Karamah. Taathira chanya aliyokuwa nayo mwanazuoni huyu katika taaluma ya fikihi ya Kishia ni kubwa kiasi kwamba, baada yake kutokana na mbinu ya kifikihi Maulamaa wakubwa wa Kishia kufuata mtindo wake wa kifikihi iliondokea kuwa mashuhuri kwa jina la Fikihi ya Jawahiri mbinu ambayo hadi leo bado ingalipo baina ya Maulamaa na wanazuoni wa Kishia.

Babu zake Swahib al-Jawahir walikuwa na asili ya mji wa Isfahan Iran. Babu yake wa tatu kutokana na kuwa na shauku na hamu ya kuwa jirani na Haram ya Imam Ali bin Abi Twalib (as) na kujifunza elimu za kidini, aligura na kuhajiri akitokea Isfahan Iran na kwenda katika mji wa Najaf huko Iraq na kuondokea kuwa, mmoja wa shakhsia mahiri wa kielimu na Maulamaa wa kuheshimiwa wa mji huo katika zama hizo.

Ayatullah Muhammad Hassan bin Baqir mashuhuri kwa lakabu ya Swahib al-Jawahir

 

Kwa utaratibu huo familia yake ikawa ikiishi katika mji huo. Baba yake ambaye ni Muhammad Baqir Najafi na mama yake walitoka katika familia ya waumini na wacha Mungu na ambayo ilikuwa pia na wasomi na wanazuoni, familia ambayo iilikuwa imeshikamana kikamilifu na mafundisho sahihi ya dini.

 

Kwa mujibu wa wanahistoria mbalimbali, Sheikh Muhammad Hassan Baqir alizaliwa mwaka 1202 Hijria. Alisoma masomo yake ya msingi na ya awali kwa walimu kama Sheikh Hassan, Sheikh Qassim Aal Muhyiddin na Sayyid Hussein Shaqarai Amili. Baada ya hapo alianza kuhudhuria masomo ya walimu wakubwa wa zama hizo katika Chuo Kikuu cha Kidini (Hawza) katika mji wa Karbala na Najaf huko Iraq kama Sayyid Jawad Amili mwandishi wa kitabu cha Miftah al-Karamah, Sheikh Ja'afar Kashiful Ghitaa na Sheikh Mussa Aal Kashiful-Ghitaa.  Kutokana na akili, maarifa na kipaji kikubwa alichokuwa nacho Sheikh Muhammad Hassan sambamba na hima na bidii aliyokuwa katika kusoma na kutafuta elimu, aliondokea kuzingatiwa sana na walimu zake na alifanikiwa haraka mno kufikia daraja ya Ijtihad akiwa kijana wa miaka 25 tu.

Katika vipindi vilivyotangulia tulieleza kwamba, vyuo vikuu vya kidini vya Mashia katika karne ya 11 na 12 vilikumbwa na hali fulani ya kudorora na kuzorota.

Lakini katika karne ya 13 Hijria kutokana na hima na idili kubwa ya Maulamaa wakubwa na mahiri kama Allama Wahid Bahbahani na Sharif al-Ulamaa Mazandarani, kwa mara nyingine tena katika miji ya Karbala na Najaf Iraq kukarejea anga ya ustawi na ukuaji elimu katika vyuo hivyo. Baada ya kuaga dunia Sharif al-Ulamaa, alimu na mwanazuoni tuliyemzungumzia katika kipindi chetu cha juma lililopita, Chuo Kikuu cha Kidini cha Karabala kikapoteza nafasi yake ya kuwa kituo cha elimu, badala yake Chuo Kikuu cha Kidini cha Najaf al-Ashraf kikachukua nafasi hiyo. Hiyo ilitokana na kuweko katika chuo hicho, Swahib al-Jawahir na kuanzia hapo kikawa ni chenye kuzingatiwa sana.

 

Ukweli wa mambo ni kuwa, Sheikh Muhammad Hassan Najafi akawa mkamilishaji wa harakati ya kielimu na fikihi mpya ambayo jiwe lake la msingi alikuwa ameliweka katika mji wa Karbala.

 

Katika upande wa kualifu na kuandika vitabu, msomi na mwanazuoni huyo ameandika vitabu vingi. Miongoni mwa vitabu hivyo ni Kashiful Ghitaa, Miftahul-Karamah, Riyadh al-Masail na Makasib. Hata hivyo kitabu chake mashuhuri zaidi ni Jawahir al-Kalam kimemfanya aondokee kuwa na lakabu ya Swahib al-Jawahir.

Aidha mwanazuonii huyu amelea na kutoa wanafunzi wengi ambao baadaye waliondokea kuwa miongoni mwa Maulamaa mashuhuri na mahiri katika maenero mbaliimbali ya ulimwengu wa Kiislamu. Vikao vyake vya masomo vilikuwa kitovu cha mkusanyiko wa wanafunzi na watu wenye kiu ya kutafuta elimu. Inaelezwa kuwa, maelfu ya wanafunzi wamenufaika na bahari ya elimu yake na hakuna mji wa Mashia ambao haukuwa na mwanafunzi ambaye amesoma kwa alimu na msomi huyu.

Licha ya kuwa, Ayatullah Muhammad Hassan bin Baqir mashuhuri kwa lakabu ya Swahib al-Jawahir alikuwa mwalimu na ustadhi mtajika na shakhsia mkubwa kielimu, lakini alikuwa akiamiliana kwa adabu na heshima ya hali ya juu na wanafuuzni wake.

Kipindi fulani alifanya juhudi kubwa kukabiliana na fikra za mawahabi na kundi la Akhbariyun.

Taathira ya Swahib al-Jawahir kwa fiqh ya Kishia ilikuwa kubwa kiasi kwamba, mafakihi na wanazuoni wakubwa wa taaluma hiyo waliokuja baada yake kama Imam Ruhullah Khomeini muasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran anasema kuwa, taathira hiyo ni kubwa na yenye kuainisha mambo.

Muda wa kipindi chetu kwa juma hili umefikia tamati, tukutane tena wiki ijayo katika sehemu nyingine ya mfululizo huu.

Basi hadi tutakapokutana tena wiki ijayo, ninakuageni nikikutakieni kila la kheri. Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.