Nov 19, 2022 12:14 UTC
  • Mchango wa Maulamaa wa Kishia Katika Uislamu (57)

Ni wasaa na wakati mwingine wapenzi wasikilizaji wa kujiunga name katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Mchango wa Maulamaa wa Kishia Katika Uislamu ambacho hutupia jicho historia ya Maulamaa na wanazuoni wa Kishia pamoja na mchango wao katika Uislamu

Kwa wafuatiliaji wa kipindi hiki bila shaka mnakumbuka kuwa, juma lililopita tulianza kumzungumzia Ayatullah Muhammad Hassan bin Baqir mashuhuri kwa lakabu ya Swahib al-Jawahir ambaye ni mmoja wa Maulamaa wakubwa aliyekuwa na kipaji cha aina yake katika karne ya 13 Hijria ambaye alichukua jukumu la Umarjaa wa Kishia katika zama hizo akiwa na sifa na ustahiki kamili. Kipindi chetu cha leo ambacho ni sehemu ya 57 kitaendelea na maudhui hii. Kuweni nami hadi mwisho wa dakika hizi chache kutegea sikio yale niliyokuandalieni kwa juma hili. 

Umashuhuri mkubwa wa Sheikh Muhammad Hassan Najafi unatokana na kitabu alichokiandika cha Jawahir al-Kalam. Kitabu hiki kama tulivyoashiria juma lililopita kimemfanya mwanazuoni huyo aondokee kuwa mashuhuri kwa lakabu ya Swabih al-Jawahir. Licha ya kupita miaka mingi, lakini kitabu cha Jawahir al-Kalam kingali kinahesabiwa kuwa, moja ya vyanzo muhimu kabisa na visivyo na mithili vya wanazuoni wa taaluma ya fikihi.

Kwa hakika Swahib al-Jawahir alikuwa na taathira aali na hali ya juu ya katika kuhuisha taaluma za fikihi ya asili ya Kishia kiasi kwamba, mafakihi watajika waliokuja baada yake kama Imam Ruhulla Khomeini (ra), mwanzilishi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran waliitambulisha fikihi asili ya Shia kupitia fikihi ya Jawahiri.

Fikihi ya Jawahiri inaashiria mbinu ya kifikihi ambayo inafungamana kikamilifu na misingi na kanuni za fikihi na wakati huo huo inatoa majibu kwa masuala mapya ya kijamii yanayoibuka katika nyanja mbalimbali za mtu binafsi na kijamiii kwa kuegemea misingi na kanuni hizo hizo.

Swahib al-Jawahir

 

Usul al-Fiqh kwa maana ya misingi na kanuni ambazo fakihi na mwanazuonii wa fikihi kwa kutumia elimu hiyo anaweza kunyambua hukumu na sheria za dini kutoka katika vyanzo vyake vikuu yaani Aya za Qur'ani na hadithi.  Sehemu ya kanuni hizo ni kanuni za kiakili na kimantiki na sehemu nyingine ya kanuni hizo zimebainishwa na kuwekwa wazi katika Aya za Qur’ani Tukufu na hadithi. Mafakihi au wanazuoni wa elimu ya fikihi wa Kishia wanasisitiza juu ya kutumia misingi na kanuni hizi na wanaamini kwamba, kama fakihi ataachana na misingi na kanuni hizi kisha akataka kufanya utoaji na unyambuzi wa hukumu za dini kutoka katika Aya na hadithi kuna uwezekano wa kufanya hilo kwa utashi wake na hata pengine kungeuka katika nadharia zake. Wanazuoni wa elimu ya fikihi wa Kishia wanaamini kuwa, upuuzaji wa namna hii ni hatari kubwa kwa dini.

 

Kwa hakika Usul al-Fiqh ni katika masomo ya asili katika vyuo vikuu vya kidini (Hawza) ambalo limekuwa tangu na tangu katika historia ya fikihi ya Kishia na katika kipindi chote cha historia, Maulamaa mbalimbali waliokuja walifanya hima na idili ya kulitajirisha somo hili muhimu na kulifanya kuwa na nidhamu zaidi. Mmoja wa wanazuoni ambao alikuwa na nafasi muhimu katika kuhuisha taaluma au somo la Usul al-Fiqh na kulifanya kuwa na nidhamu isiyo na mithili, makini na ya kisomi zaidi katika kunyambua hukumu za dini ni Sheikh Muhammad Hassan Najafi Swahib al-Jawahir ambaye tumekuwa tukimzungumzia tangu juma lililopita. Kwa hakika kitabu chake cha Jawahir al-Kalam ni tabu kubwa la maarifa yaani Insaiklopidia ya fikihi ya Kishia ambayo ndani yake kumetumikka mbinu sahihi za kanuni na misingi ya fikihi kwa kuonyesha hoja na nguvu kubwa liliyonalo somo hil muhimu katika kujenga hoja na kunyambua na kutoa hukumu mbalimbali kwa njia sahihi kutoka katika vyanzo vyake vikuu. Somo hilio liko kwa namna ambayo linatoa majibu ya masuala mapya ya kifikihi na hivyo kulifanya kwenda na wakati na zama.

Umuhimu wa jambo hili unaonekana zaidi pale tunapotupia jicho historia  katika zama mbalimbalii hususan katika zama za Sheikh Muhammad Hassan Najafi au Swahib al-Jawahir kama anavyojulikana na kuona kuwa, baadhi ya makundi likiwemo la kundi la Akhbariyun. Kama tulivyoashiria katika vipindi vyetu vilivyotangulia ni kuwa, Akhbariyun ni kundi la mafakihi na wanazuoni wa fikihi wa Kishia ambao mtindo na mbinu yao ya kielimu ya kufikia hukumu za Kisheria na taklifu za Mwenyezi Mungu ni kufuata hadithi na sio mtindo wa Ijtihadi na Usul.

Kimsingi ni kuwa, mrengo wa Akhbariyun unaamini kwamba, haijuzu kumkalidi Mujtahidi. Mkabala na mrengo huo kuna mrengo wa Usuliyun ambao unaamini kwamba, ili kuainisha kwa njia sahihi hukumu za dini, ni lazima mtu awe na utaalamu na ubobezi wa kielimu na kuna haja ya kuweko watu ambao kutokana na umahiri na kutabahari kwao kwa vyanzo vya dini na kwa kutumia mbinu makini ya kielimu na kiakili wanyambue hukumu za dini kuhusiana na masuala mbalimbali. Watu wengine ambao hawana ujuzi na ubobezi huu wanapaswa kuwarejea wasomi na wanazuoni hawa yaani kuwakalidi.

Kitabu cha Jawahir al-Kalam

 

 

Suala la asiye na ujuzi kumrejea mwenye ujuzi ni kanuni inayokubalika kiakili na mrengo wa Usuliyun unaamini kwamba, kanuni hii inahusiana pia na suala la kuainisha hukumu ya kidini. Endapo kundi la Akhbariyun lingefanikiwa kushinda fikra za wanazuoni na watu wa kawaida, basi bila shakka lingeleta madhara kwa dini ya Kiislamu na Madhehebu ya Ahlul-Beiti (as) ambayo isingewezekana kuyafidia.

Kimsingi ni kuwa, Jawahir al-Kalam ni sherh na ufafanuzi wa kitabu cha Sharaiu al-Islam cha Muhaqqiq Hilli fakihi na mwanazuoni mkubwa wa Kishia aliyeishi karne ya Saba ya Hijria. Kitabu hiki kiinajumuisha milango na faslu zote za fikihi na ni kitabu ambacho kwa hakika kiinamtosheleza kila anayefanya uhakiki katika uga na uwanja huu. Katika kitabu cha Jawahir al-Kalam kuna maoni na nadhari za Maulamaa na mafakihi waliotangulia na zimechambuliwa kwa umakini na hata kukosolewa kielimu. Sifa nyingine ya kitabu hiki ni kuwa, kimeandikwa kwa lugha nyepesi na ya kawaida huku hoja na uchambuzi uliotumika kujenga hoja au kukosoa hoja ukiwa wazi na wa kueleweka.

Licha ya kuwa kitabu hiki kiliandikwa kwa ajili ya kutoa sherh na ufafanuzi wa kitabu cha Sharaiu al-Islam na hata mpangilio wake pamoja na faharasa na anuani zake zimefuata kitabu hicho, lakini wigo mpana na wa kina wa ufafanuzi huu umekuwa kwa namna ambayo umekimeza kitabu cha Sharaiu al-Islam cha Muhaqqiq Hilli. Uandishi wa kitabu hiki chenye kurasa elfu moja ulichukua miaka 30.

Kaburi la Ayatullah Muhammad Hassan bin Baqir mashuhuri kwa lakabu ya Swahib al-Jawahir

 

Hatimaye Swahib al-Jawahir baada ya kutumia sehemu kubwa ya umri wake kwa ajili ya kueneza mafundisho ya Ahlul-Beiti (as) na kulea wanafunzi ambao waliondokea kuwa Maualamaa wa kutegemewa, aliaga dunia mwaka 1366 Hijria katika mji wa Najaf, Iraq na kuzikwa katika mji huo. Kaburi lake leo limekuwa sehemu ya kufanya ziara wapenzi wa Ahl-Beiti (as).

Wapenzi wasikilizajii muda wa kipindi chetu kwa leo umefikia tamati. Tukutane tena wiki ijayo katika sehemu nyingine ya kipindi hiki. Asantebni kwa kunitegea sikio na kwaherini.